Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; UP YOUR GAME…
Watu wengi wanapoanza kufanya kitu, iwe ni kazi au biashara, huwa wanaanza wakiwa na hamasa kubwa.
Wanaweka juhudi kubwa ili kujua vizuri wanachofanya na kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Lakini baada ya muda, wanakuwa wameshafikia kiwango cha kujua kile wanachofanya, wanakuwa wamezoea na hivyo wanaanza kufanya kwa mazoea.
Baada ya kufika hatua hii, wengi hujikuta wakifanya mambo yale yale wakati wote huku wakipata matokeo ambayo siyo mazuri.
Wanajiona wanaweka juhudi kubwa sana, ila matokeo wanayoyapata ni madogo mno.
Hii yote ni kwa sababu wanakuwa wapo kwenye ngazi ile ile, hivyo hata wakiweka juhudi kubwa, matokeo yanaendelea kuwa yale yale.
Njia pekee ya kupata matokeo tofauti, ni kupiga hatua zaidi, kwenda mbele zaidi, ku UP YOUR GAME.
Kama ambavyo wachezaji wenye mafanikio wana mitindo bora na ya tofauti kwenye michezo yao, hivyo pia ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye kile tunachofanya kwenye maisha.
Lazima upande viwango, lazima ufikiri na kufanya kwa utofauti mkubwa.
Na njia pekee ya kuweza kufanya hivyo, ni kuwa na muda wa kujitafakari na kuchambua kwa kina kila unachofanya.
Unahitaji muda wa kuweza kuona kile unachofanya kwa jicho la tatu, ili uweze kujua wapi unafanya kwa mazoea na wapi unapokosea.
Mara kwa mara, pitia kila unachofanya, na jiulize ni hatua zipi unazoweza kupiga zaidi kwenye hicho unachofanya.
Usifanye chochote kwa mazoea, mazoea ni sumu kubwa kwa mafanikio.
Uwe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha