Siku za nyuma kidogo, watu walikuwa wanasema matajiri wana fedha ila hawana muda, wakati masikini wana muda ila hawana fedha. Kauli hiyo ilikuwa na uhalisia fulani, na ndiyo maana matajiri wanawaajiri masikini ili kutumia muda wao.

Lakini siku hizi mambo yamebadilika, matajiri wana fedha na muda, wakati masikini hawana fedha na kibaya zaidi hawana muda pia. Yaani ni hasara mara mbili, kwa sababu fedha hakuna na muda pia hakuna.

Kwa kukosa muda, mtu anashindwa hata kuongeza kipato chake na kuondoka kwenye umasikini.

Lakini je huu muda unakuwaje hasa, kama kila mmoja wetu amepewa masaa 24 kwa siku, inakuwaje baadhi ya watu wana muda na wengine hawana muda kabisa?

masikini na muda

Iweje matajiri na waliofanikiwa wanaonekana kuwa na muda mwingi, wakati masikini na walioshindwa wanaonekana kuwa wamevurugwa, wanaona siku zinaisha, miaka inaanza na kuisha lakini hawaoni kabisa muda wao unaishia wapi na hawawezi kupata muda zaidi?

Nilichojifunza ni kwamba, jinsi ambavyo masikini wanatumia muda wao, ni tofauti kabisa na matajiri wanavyotumia na kuchukulia muda wao. Na tofauti hii ndiyo inawafanya matajiri kuwa matajiri na masikini kuendekea kubaki kwenye umasikini. Japo mwisho wa siku kila mtu anaona yupo bize na amechoka kweli, kuna ambao wapo ‘bisy for nathing’ na ambao wapo ‘busy for something’ kama wanavyosema vijana.

Baada ya kuchambua kwa kina tabia hizi za matumizi ya muda baina ya matajiri na masikini, nimegundua hizi tano ndiyo kubwa na zenye madhara makubwa. Jifunze tabia hizi tano hapa na zifanyie kazi ili uweze kutumia muda wako vizuri kwa mafanikio yako.

  1. Kwa masikini muda ni fedha, kwa tajiri muda ni zaidi ya fedha.

Niambie kama umewahi kusikia au kusema kauli hii; muda ni fedha. Kama umewahi kuisema wewe mwenyewe na ndivyo unavyoamini nina habari mbaya kwako, umeshakolea kwenye njia ya umasikini, na kama hutabadilika haraka, mambo yatakuwa magumu kwako.

Hebu tuangalie muda na fedha kwa undani.

Muda tuna masaa 24 pekee kwa siku, ambayo ni sawa na dakika 1440. Ukipoteza dakika moja kwenye siku yako, ndiyo imepotea moja kwa moja, hutakuja kuipata tena hiyo dakika kwenye maisha yako. Muda ukishapita ndiyo umepita moja kwa moja.

Lakini tukiangalia fedha, unaweza kupoteza fedha leo lakini kesho ukapata fedha nyingine zaidi. Unaweza kutengeneza fedha zaidi kadiri muda unavyokwenda kama una mipango mizuri na unaweka juhudi.

Unaweza kutengeneza fedha zaidi, lakini huwezi kutengeneza muda zaidi, sasa unawezaje kusema muda ni fedha?

Muda ni zaidi ya fedha na hivyo unapaswa kupewa heshima kubwa sana. Muda unapaswa kulindwa na kutumiwa kwa uangalifu kwa sababu ukishapotea, hauwezi kupatikana tena.

  1. Masikini wanataka kufanya kila kitu, matajiri wanafanya machache na muhimu.

Kuna kitu kikubwa sana kinawatofautisha matajiri na masikini kwenye muda, kitu hicho ni KIPAUMBELE.

Matajiri wana vipaumbele kwenye matumizi yao ya muda, wanajua ni mambo gani muhimu kabisa wanapaswa kufanya na wanaweka muda wao mwingi kwenye mambo hayo. Hawakubali kabisa kufanya jambo jingine kama hawajafanya yale muhimu.

Kwa upande wa pili, masikini hawajui kitu kinachoitwa kipaumbele, wao wanafanya chochote ambacho kinatokea mbele yao. Wanayapa mambo yote uzito sawa na wanaweza kuacha kufanya kitu muhimu kwa sababu kuna kitu kingine kimejitokeza mbele yao.

Bila ya kuwa na kipaumbele, mtu unamaliza siku ukiwa umechoka kweli lakini huoni kikubwa ambacho umefanya.

  1. Masikini wanapangilia muda kichwani, matajiri wanapangilia muda kwa kuandika.

Kuna nguvu kubwa sana ambayo ipo kwenye kuandika, ndiyo maana mambo mengi makubwa yanafanyika kwa mikataba, ambayo watu wanaweka sahihi zao. Kuandika na kuweka sahihi ni ishara ya kujitoa na kuhakikisha kweli unafanya.

Msimamishe masikini yoyote popote alipo na muulize ana mipango gani kwa siku hiyo, atakuambia kwa juu juu. Muulize kila mpango anaufanya saa ngapi ya siku hiyo, macho yatamtoka.

Lakini matajiri wana mipango iliyoandikwa, wanajua wanafanya nini na kwa wakati gani. Masaa yao ya siku yanakuwa yameshapangiliwa kabisa kwa kuandikwa, wanachofanya ni kufuata mipango hiyo. Na hicho ndiyo kinawaepusha na usumbufu au kupoteza muda.

Ni muhimu upangilie matumizi ya muda wako kwa maandishi.

  1. Matajiri wanaepuka usumbufu, masikini wanakaribisha usumbufu.

Mpigie masikini simu muda wowote atapokea na mtaweza kuongea kadiri utakavyo wewe.  Mwangalie kwenye mitandao ya kijamii, kila dakika yupo, kila kinachoendelea huko anakijua. Muulize kuhusu timu zote za ulaya atakutajia wachezaji wote na magoli waliyofunga. Muulize kuhusu vipindi vya TV na atakueleza kila kitu. Lakini muulize matumizi yake ya muda kwenye kujifunza au maono yake kwa miaka 20 mpaka 50 ijayo, macho yatamtoka.

Masikini wamekuwa wanakaribisha kila aina ya usumbufu ambao unachukua muda wao. Kila wakati wanapatikana na hawataki kupitwa na lolote. Hali hiyo unawafanya kupoteza muda mwingi bila ya wao wenyewe kujua.

Matajiri wanaepuka kila aina ya usumbufu, wanalinda sana muda wao, wanakaa mbali na usumbufu hasa pale wanapofanya kazi muhimu kwao, kama walivyopanga kwenye ratiba zao. Matajiri wanajua kitu pekee kinachoweza kuwapita ni kuchelewa kutekeleza mipango yao na siyo habari, simu au mitandao ya kijamii.

  1. Masikini wanatumia muda, matajiri wanawekeza muda.

Kila mtu huwa ana muda unaoitwa ‘down time’ huu ni muda ambao unaweza kupotea wenyewe, ambao mtu huna cha kufanya kwa hakika. Labda umetoka nyumbani ukitegemea kuwahi mahali, ukakutana na foleni ndefu barabarani, ambayo inakuzuia kufika haraka, na wakati huo huwezi kurudi. Au upo kwenye foleni kusubiri huduma fulani, labda unasubiri gari iondoke, au upo safarini au unasubiri kikao au mkutano kuanza.

Muda wa aina hii ndiyo unawatofautisha zaidi masikini na matajiri. Masikini wanapopata muda wa aina hii, wanakazana kuona watautumiaje. Watakimbilia kwenye simu zao, kuanza kuangalia mitandao ya kijamii nini kinaendelea, wataanza hata kufikiria nani wampigie simu au kumtumia ujumbe, bila hata sababu za msingi. Yaani raha yao ni kuona muda huo umepita, na hawataki ‘kuboreka’.

Kwa upande wa pili, matajiri wanapopata muda wa aina hii, huwa hawautumii kabisa, badala yake wanauwekeza. Wanachofanya kwenye muda huo, ni kujifunza zaidi, wanajua wanachojifunza leo, kitawasaidia siku zijazo, na hivyo wanakuwa hawajapoteza muda, badala yake wanakuwa wameuwekeza.

Popote wanapokuwa, matajiri huwa wanatembea na vitabu, vilivyoandikwa na hata vya kusikiliza. Wakipata nafasi wanasoma, na kama nafasi hairuhusu kusoma basi wanasikiliza vitabu vilivyosomwa ‘AUDIO BOOKS’.

Usikubali kabisa kuendelea kupoteza muda wako, bali wekeza muda wako unaoweza kuupoteza.

NYONGEZA; Matajiri wanauthubutu wa kusema HAPANA, masikini wanaogopa kusema hapana.

Kama una marafiki wawili, mmoja tajiri na mmoja masikini, fikiria kitu chochote ambacho kinaweza kuwa ni cha kupoteza muda, halafu wapigie simu mmoja baada ya mwingine. Anza na masikini, mpigie simu na mwambie unahitaji kukutana naye au msaada wake kwenye jambo hilo(isiwe tu hela), ambalo hata siyo muhimu na atakujibu ndiyo, na huenda atapendekeza mfanyeje kwa ubora zaidi. Baada ya hapo mpigie tajiri na mwombe kitu hicho hicho, kwanza wewe mwenyewe utaanza kujishuku, hivi atakubali kweli, au nimwambieje. Halafu utakapopata ujasiri wa kumwambia, cha kwanza atakachokuambia ni HAPANA, halafu atapima umuhimu wa jambo hilo na kukupa njia mbadala za kuweza kufanya.

Rafiki yangu, wote tuna masaa 24 kwa siku, lakini ndani ya muda huu, wapo wanaofanya makubwa na wapo ambao wanajiuliza muda umeenda wapi. Uamuzi ni wako unachagua kuwa upande gani. Mimi nimeshatimiza jukumu langu la kukuonesha pande hizo mbili kwenye matumizi ya muda.

Kujifunza zaidi jinsi ya kutumia muda wako vizuri na kwa mafanikio, kuweza kufanya makubwa hata kama umebanwa sana, soma kitabu nilichoandikwa kinaitwa PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU. Kitabu ni softcopy, unaweza kusomea kwenye simu, tablet au kompyuta. Gharama ya kitabu ni tsh 5,000/= na kinatumwa kwa email. Kukipata kitabu tuma fedha kwa namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma ujumbe wenye email yako na utatumiwa kitabu.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog