Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha kwamba, kwenye jamii yoyote ile, kuna asilimia 5 ya watu ambao wanakuwa na mafanikio makubwa, huku asilimia 95 ya watu wakiwa na maisha ambayo ni ya kawaida, hawajafanikiwa. Sheria hii ya 95/5 ipo kwenye kila eneo, kuanzia dunia nzima, nchi, mkoa, wilaya, mtaa na hata familia.

Kila eneo kuna watu wachache sana ambao wana mafanikio makubwa, huku wengi wakiwa wana maisha ya kawaida na wengine wanateseka mno.

Kwa namna mgawanyo huu wa mafanikio ulivyo, unaweza kusema kwamba kuna watu wachache ambao asili imewachagua wafanikiwe huku wengi wakiwa wameandaliwa kushindwa.

Lakini sasa unapoingia ndani na kuwaangalia kwa umakini wale wachache waliofanikiwa na wengi ambao wameshindwa, unaona wazi wazi kwamba zipo tofauti kubwa sana kati ya makundi haya mawili. Tofauti hizi zinaanzia kwenye mtazamo, kwenye maarifa waliyonayo, kwenye hatua wanazochukua na hata kwenye tabia zao.

Ni kwa kuangalia hili ndiyo tunajifunza kwamba, watu waliofanikiwa sana, kuna vitu wanajua na wanafanya, ambavyo wengine hawajui na hata kama wanajua hawapo tayari kufanya.

Unaweza kufikiri pia kwamba yale wanayofanya waliofanikiwa ni ya utofauti mkubwa mno, lakini ukiangalia kwa kina, unagundua ni ya kawaida sana, ambayo hata ambao hawajafanikiwa wangeweza kuyafanya. Lakini sasa, changamoto inakuja kwamba, mambo hayo pia ni magumu kufanya, na ndiyo maana wachache pekee ndiyo wanakuwa tayari kuyafanya, huku wengi wakiyakwepa na kuishia kuwa kawaida.

Kwa mfano, njia pekee ya kuelekea kwenye utajiri ni matumizi kuwa madogo kuliko mapato, kuwa na vyanzo vingi vya kipato na kuweka akiba na kuwekeza. Kila mtu anajua hilo, lakini ni wachache sana wanaoweza kutekeleza. Kuweka akiba haihitaji uwe na shahada yoyote, ni kiasi tu cha kuweka pembeni asilimia 10 ya kipato chako, usiitumie kabisa, lakini wengi wanashindwa kutekeleza hilo, na wanabaki kuwa watumwa wa fedha maisha yao yote.

Unaona sasa namna mambo yanavyokwenda rafiki yangu?

Leo nataka nikushirikishe neno moja, ambalo wale waliofanikiwa sana wanalitumia vizuri, linawapa uhuru mkubwa na mafanikio pia. Neno hili siyo jipya, kila mtu analijua, na kila mtu anaweza kulitumia.

Ila sasa, ni neno gumu sana kutumia, ni neno ambalo wengi huona aibu kulitamka, na ndiyo maana wachache pekee ndiyo wanaoweza kulitumia na kufurahia uhuru na mafanikio yanayotokana na neno hili.

Leo utakwenda kujua neno hili, jinsi ya kulitumia vizuri na hata maeneo kumi ambayo unapaswa kutumia neno hili.

Neno moja ambalo ukilitumia litakuletea uhuru na mafanikio makubwa ni neno HAPANA.

Ndiyo, kusema hapana, kwa watu, mambo na hata kwako binafsi, ndiyo njia pekee itakayokuletea wewe uhuru na mafanikio makubwa.

Neno HAPANA lina nguvu kubwa ya kukupa wewe muda wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako, kukuzuia kuishia njiani na hata kukuwezesha kupanga vipaumbele vyako.

SOMA; Tofauti Hizi Tano Za Matumizi Ya Muda Kwa Matajiri Na Masikini Ndiyo Zinawatofautisha Matajiri Na Masikini.

Wengi wamekuwa wakishindwa kutumia neno hili HAPANA kwa sababu hawapendi kujiumiza wala kuumiza wengine. Watu wanapenda kumfurahisha kila mtu na kinachotokea kwenye kutaka kumfurahisha kila mtu ni kutokumfurahisha yeyote na mambo kuzidi kuwa magumu.

Jinsi ya kutumia neno hapana.

Kuna maeneo makuu matatu unayopaswa kutumia neno HAPANA kwenye maisha yako.

Eneo la kwanza; kwako binafsi.

Kama huwezi kujiambia HAPANA wewe mwenyewe, basi jua ya kwamba huwezi kuwa na uhuru. Kwa sababu kuna wakati mwili wako utakuwa unataka vitu ambavyo vinaenda kinyume na maono na malengo yako. Kama utauambia mwili ndiyo, hutaweza kufika kule unakotaka kufika.

Lazima uwe tayari kusema HAPANA kwa mambo mazuri, ili uweze kupata yale ambayo ni bora zaidi.

Eneo la pili; kwa watu wengine.

Hili ni eneo gumu zaidi, kwa sababu huwa tunaogopa kuwaambia wengine hapana, tukiona tutawaumiza au kufikiria watatuchukuliaje, labda watatuona tuna roho mbaya na hatujali.

Unahitaji kuwaambia wengine hapana, hasa pale wanapokuja na mambo ambayo wanataka wewe ufanye na unajua kabisa siyo muhimu kwako wala kwao.

Na watu ambao unahitaji kutumia neno hapana zaidi ni wale ambao mmeshazoeana kuishi maisha ya kawaida, wataendelea kukutaka ufanye yale ya kawaida, hivyo ili kusonga mbele kuwa tayari kuwaambia watu wako wa karibu sana HAPANA.

Eneo la tatu; kwa vitu na hali mbalimbali.

Kila siku, kuna vitu na hali mpya utakazokutana nazo, vitu vitakavyokuwa na ushawishi mkubwa kwako kuona kwamba vinakufaa au usipochukua hatua utavikosa. Lakini pia kwa kufanya vitu hivyo, unajitoa kwenye malengo na maono yako makubwa.

Hivi ni vitu ambavyo unahitaji kusema hapana, hata kama unaona kuna manufaa utayakosa. Kwa sababu huwezi kufanya kila kitu, hivyo lazima uwe na maeneo machache unayoweka nguvu zako na kusema hapana kwenye mengine ambayo siyo muhimu sana kwako.

Mambo kumi ya kusema HAPANA ili uweze kufanikiwa.

Kama unataka uhuru na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, sema hapana kwenye maeneo na mambo haya kumi.

  1. Sema hapana kwa uvivu na tabia ya kukata tamaa na kuahirisha mambo. Kila unapoanza kufikiria kwamba unaweza kufanya kesho, au haiwezekani, sema hapana na endelea kufanya.
  2. Sema hapana kwa tabia ya kutafuta njia ya mkato ya mafanikio, hata kama kila mtu anafanya hivyo, hata kama unaona wengine wananufaika, kama ni njia ya mkato na kama haiendani na misingi yako sema hapana.
  3. Sema hapana kwa watu wanaokunyonya nguvu zako, hawa ni watu ambao ukikutana nao unaondoka ukiwa umechoka na kukata tamaa. Hawa ni watu ambao ukiwa na jambo lolote kubwa unalotaka kufanya, huwa hawakosi njia ya kukuonesha kwamba utashindwa.
  4. Sema hapana kwa maarifa na taarifa hasi, taarifa ambazo zinakatisha tamaa na hazina mchango wowote kwenye kuelelea kwenye malengo na mipango yako.
  5. Sema hapana kwa usumbufu unaouita burudani, usumbufu unaokutoa kwenye juhudi unazoweka. Usumbufu wa habari, mitandao ya kijamii na hata maongezi yasiyo na manufaa kwako.
  6. Sema hapana kwa fursa mpya zinazoibuka kila siku, jua nini unataka kwenye maisha yako, kuwa na maono makubwa, kisha chukua hatua kufikia maono hayo. Kingine chochote ambacho utakutana nacho njiani na kuambiwa ni fursa kubwa, sema hapana.
  7. Sema hapana kwa watu ambao wanataka ufanye vitu ambavyo havina mchango wowote katika kufikia malengo yako, na hicho wanachotaka ufanye hakina mchango mkubwa kwao pia.
  8. Sema hapana kwenye tabia ya kuwasema watu vibaya, tabia ya kuwasema watu ambao hawapo, tabia ya majungu na umbeya. Chochote unachomsema mtu vibaya, jua kitamfikia.
  9. Sema hapana kwenye tabia ya kutaka kuwaonesha wengine kwamba una kitu fulani au unaweza vitu fulani. Sema hapana kwa tabia ya kufanya mambo ili uonekane. Fanya yale ambayo ni muhimu, na acha kutaka kuonekana.
  10. Sema hapana kwenye tabia ya kufanya mambo kwa kawaida, kufanya ili umalize au uonekane umefanya. Sema hapana kufanya kitu ambacho huwezi kukiboresha zaidi. Kila siku, kwenye kila unachofanya, boresha zaidi, piga hatua zaidi.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Jinsi ya kusema HAPANA kistaarabu.

Ni kweli neno HAPANA linauma, hasa pale unapowaambia wengine. Na hivyo wengi wamekuwa wanaogopa kulitumia. Lakini ipo njia ya kusema HAPANA kistaarabu, njia ambayo itawafanya watuwa kuheshimu licha ya kuwakatalia kile wanachotaka.

Njia hii ni kuwapa watu sababu ya kukataa au kutoweza kufanya. Waoneshe watu vipaumbele vyako na waeleze kwa nini hutaweza kufanya kile ambacho wanakutaka ufanye.

Pia wape njia mbadala ya wao kufanya, au njia mbadala ya wewe kufanya ili waweze kupata kile wanachotaka. Hii itakufanya uwe umewasaidia zaidi ili waweze kunufaika pia. Kwa sababu mara nyingi watu wamekuwa wanakazana na mambo ambayo hayana manufaa kwao.

Na kama itatokea mtu hakuelewi hata baada ya kumpa sababu na njia mbadala, basi mwache mpaka atakapoona matokeo ya kile unachofanyia kazi. Usitoe tena sababu, bali wewe kazana kufanya kile ambacho ni muhimu na matokeo yataongea yenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog