Whatever fortune has raised to a height, she has raised only to cast it down. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera sana rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana na ya kipekee kwetu.
Ni siku mpya, ambayo tumeianza na nguvu na hamasa mpya za kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; KINACHOINULIWA KITAANGUSHWA…
Moja ya makosa ambayo tumekuwa tunayafanya kwenye maisha, ni kujitambulisha kwa vitu ambavyo siyo vyetu.
Tunasema nyumba yangu, gari langu, mali zangu, fedha zangu, watoto wangu na kadhalika.
Vitu vyote hivyo siyo vyetu, bali tumepewa jukumu la kuvitumia na kuvitunza vizuri kwa manufaa ya wengine na dunia kwa ujumla.
Hiyo ikiwa na maana kwamba, wakati wowote tunaweza kunyang’anywa vitu hivyo na tukabaki mikono mitupu.
Hivyo kama umekuwa unajitambulisha kwa vitu hivyo visivyo vyako, lazima utaumia na kuanguka pale vitu hivyo vinapochukuliwa kutoka kwako.
Chochote ambacho asili au dunia imetupa, kuna siku itatunyanganya.
Chochote ambacho kimeinuliwa, kuna siku kitaangushwa.
Unapaswa kujua hili, siyo kwa ajili ya kukata tamaa, bali kwa ajili ya kufanya mambo haya mawili muhimu;
Moja; kutojishikiza na vitu na kutokuweka furaha yako kwenye kitu chochote ila wewe. Kama unaweza kupoteza kila ulichonacho sasa, na maisha yako yakaendelea bila ya kukata tamaa na kuumia, basi una uhuru mkubwa, unayatawala maisha.
Kama kuna chochote ambacho unaona ukikipoteza basi maisha yameharibikanna hayafai tena, basi wewe ni mfungwa na mtumwa wa maisha.
Mbili; kutumia vizuri kitu wakati bado kipo chini yako. Kwa wakati ambapo umepewa kitu, basi kitumie vizuri, kitumie kwa ukamilifu, kiasi kwamba hata kama kesho utakikosa, basi hutajiambia ningejua jana ningefanya hivi au vile.
Kila nafasi unayopata ya kuwa na kitu, itumie kama ndiyo nafasi yako ya mwisho kuwa na kitu hicho, kwa sababu nafasi ya mwisho inakuja, ambayo huijui, na huenda inaweza kuwa hiyo uliyonayo leo.
Usishikize maisha yako na furaha ya maisha yako kwa kitu chochote au mtu yeyote, kila kinachokuzunguka umekopeshwa kwa muda, kitumie ukiwa na maandalizi ya kukirudisha kwa mwenyewe.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha