Njia rahisi na ya halali kabisa ya kuiba ujuzi na uzoefu wa watu wengine ni kusoma vitabu. Vitabu vina maarifa mengi ambayo yanaweza kutusaidia sana kwenye maisha yetu ya kila siku.

Lakini pamoja na umuhimu huu wa vitabu, wengi hawasomi vitabu. Ni watu wachache sana ambao wanaweza kusoma kitabu na kukimaliza baada ya kuwa wamehitimu masomo. Wengi hufikiri ukishahitimu masomo basi kusoma ndiyo umeweka pembeni.

Watu hawa wasiosoma vitabu unakuta wanateseka na changamoto ambazo wangeweza kuzitatua kirahisi sana iwapo wangekuwa na maarifa sahihi ya kufanya hivyo.

Sababu kubwa ya wengi kushindwa kusoma vitabu imekuwa ukosefu wa muda, lugha na ukosefu wa fedha. Baada ya kufanya utafiti wangu binafsi, nimegundua sababu hizi zote ni za uongo, ni sababu za kujifurahisha tu na siyo sababu halisi.

Sababu ya muda unaweza kuitatua iwapo utapanga muda wako vizuri, au kupanga usomaji wako vizuri. Kwa mfano kama utasoma kurasa 10 za kitabu kila siku, ndani ya mwezi mmoja utamaliza kitabu. Sababu ya lugha nayo ni ya kujifurahisha, kwa sababu vipo vitabu vingi kwa lugha rahisi ya kiswahili,

Sababu ya gharama au ukosefu wa fedha za kununua vitabu, sijawahi kuona kitabu ambacho ni ghali. Kwa hakika vitabu vingi vinauzwa kwa bei ya chini sana ukilinganisha na maarifa ambayo mtu unayapata kwenye vitabu hivyo. Na muhimu zaidi, kama hakuna mtu anayetembea uchi kwa kukosa fedha za kununua nguo, iweje mtu akose fedha za kununua kitabu? Ni mpangilio tu wa vipaumbele.

Kila mwezi nimekuwa nakushirikisha kitabu cha kujisomea, lengo likiwa ni wewe rafiki yangu uweze kupata maarifa sahihi ya kukuwezesha kupiga hatua zaidi. Katika vitabu vingi ninavyokuwa nimevisoma, nachagua vile ambavyo najua vitakuwa na msaada kwa wengi na kisha kuwashirikisha.

Tumeuanza mwaka 2018 na huu ni wakati ambapo wengi wanaweka malengo na mipango ya mwaka huu mpya 2018. Ni wakati ambao wengi pia wanajidanganya na kupoteza muda kupanga vitu ambavyo watavisahau baada ya mwezi mmoja.

Katika mwezi huu wa Januari 2018 nakushirikisha usome kitabu cha BORN TO WIN cha ZIG ZIGLER.

born to win

Zig Zigler alikuwa akifahamika kama baba wa hamasa kwa kizazi cha sasa, ni mmoja wa watu ambao walikuwa wana uwezo wa kutoa mafunzo yanayowasukuma watu kuchukua hatua na kuboresha maisha yao.

Katika kipindi cha hai wake, Zigler alifanikiwa kutoa mafunzo mengi kwenye maeneo ya Mafanikio, Mauzo, Hamasa na Malezi pia.

Zig Zigler ni mmoja wa waandishi walionipa hamasa kubwa sana wakati naanza uandishi, nimekuwa nasikiliza programu zake za mafunzo mara kwa mara na nimekuwa najifunza mengi zaidi kila mara.

Moja ya vitu vikubwa nilivyojifunza kwa Zig Zigler ni falsafa yake ya maisha ambayo inasema ‘unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, kama utawasaidia watu wengi kupata kile wanachotaka’. Ni falsafa inayokupa sababu ya kuwa wa msaada na huduma kwa wengine. Na nimekuwa naishi falsafa hii kwenye huduma zote ninazotoa, haijawahi kuniangusha.

Kwenye kitabu hichi cha BORN TO WIN, Zigler anatukumbusha kwamba kila mmoja wetu amezaliwa kama mshindi. Kila mtu ana ushindi ambao upo ndani yake, kila mtu anaweza kupiga hatua na kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

Lakini jamii imetufundisha kinyume. Malezi ya kwenye familia na mafunzo ya shuleni yamechangia kuondoa ile hali ya kujiamini na kutumia ushindi uliopo ndani yetu.

Hivyo Zigler, kupitia kitabu hichi anatuonesha siri hii ya mafanikio ambayo ipo ndani ya kila mmoja wetu. Kama umewahi kufikiri kwamba wewe huwezi kufanya makubwa, basi soma kitabu hichi cha BORN TO WIN, Zigler hatakuacha kama ulivyo.

Pamoja na kwamba umezaliwa kushinda, Zigler anakuambia ushindi hautakuja tu kwa sababu upo. Zigler anasema ili kuweza kufikia ushindi na mafanikio makubwa yaliyopo ndani yako, unahitaji kufanya mambo matatu;

Moja; kupanga kushinda. Huwezi kushinda kama huna mipango inayokupeleka kwenye ushindi.

Mbili; kujiandaa kushinda. Baada ya mipango, lazima uwe na maandalizi, kwa sababu safari ya ushindi haitakuwa rahisi, maandalizi ni muhimu.

Tatu; Tegemea kushinda. Baada ya kupanga na kujiandaa, lazima mawazo yako yawe na mategemeo ya ushindi, lazima uwe na mtazamo chanya wa kwamba unakwenda kupata kile unachotaka. Na huu utakuwezesha kuvuka vikwazo na changamoto.

Kitabu BORN TO WIN ni kitabu sahihi sana kwako kukisoma katika kipindi hichi cha mwanzo wa mwaka. Tena kabla hujaendelea na zoezi lako la kuweka malengo, soma kwanza kitabu hichi.

KITABU CHA NYONGEZA; TEN COMMITMENTS TO YOUR SUCCESS.

Lengo langu la kukushirikisha wewe rafiki yangu kitabu kimoja cha kusoma kila mwezi, ni usome angalau kurasa 10 kila siku. Kwa mwezi utakuwa umesoma kurasa 300 ambao huo ni wastani wa kitabu kimoja. Lakini baadhi ya vitabu ni vifupi, vina kurasa chini ya hapo.

Kwa mfano kitabu cha BORN TO WIN nilichowashirikisha kwa mwezi huu, kina kurasa chini ya 200. Hivyo kama ukisoma kurasa 10 kila siku, ndani ya wiki mbili mpaka tatu utakuwa umekimaliza. Hivyo utakuwa na siku ambazo huna kitabu cha kusoma, na kwa kuwa hukupanga tangu mwanzo, utajikuta unapoteza muda wa kufikiria kitabu gani usome.

Ili kuepuka hilo, nakushirikisha pia kitabu kingine cha nyongeza, kitabu ambacho kitakusaidia sana katika kipindi hichi cha mwanzo wa mwaka.

Kitabu cha nyongeza ninachokupa ni TEN COMMITMENTS TO YOUR SUCCESS kilichoandikwa na STEVE CHANDLER.

Kwa kifupi tunaweza kusema kitabu hichi ni amri kumi unazopaswa kuzifuata na kuziishi kama kweli unataka kuwa na mafanikio yanayodumu. Ni kitabu kizuri sana na rahisi kusoma.

Kitabu hichi kimegusa maeneo yote muhimu ya maisha yako, kuanzia mwili, akili, roho, fedha, mahusiano, kazi na biashara.

Ni kitabu kifupi pia, chenye kurasa 101 pekee. Kisome kitabu hichi pia na utauanza mwaka 2018 ukiwa na moto wa kipekee sana wa kukufikisha kwenye mafanikio.

Soma vitabu hivi viwili kwa kuuanza mwaka huu 2018 na fanyia kazi yale ambayo utajifunza kwenye vitabu hivi, na kwa hakika, mwaka 2018 utakuwa mwaka bora sana kwako.

JINSI YA KUPATA VITABU HIVI.

Kupata vitabu hivi na hata kuweza kuvisoma kwa utaratibu mzuri wa kurasa 10 kila siku, unapaswa kujiunga na kundi la KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU.

Usomaji

Hili ni kundi maalumu ambalo lipo kwenye mtandao wa wasap, ambalo ukijiunga kila siku unasoma kurasa kumi na kushirikisha yale uliyojifunza na unayokwenda kufanyia kazi.

Ili kujiunga na kundi hili, unapaswa kulipa ada ya mara moja pekee ambayo ni tsh 10,000/=. Kwa kulipa ada hii utaweza kupata vitabu hivi na vya miezi inayokuja, na pia kujifunza kupitia wengine.

Kujiunga lipa ada tsh 10,000/= kwa mpesa 0755 953 887 au tigo pesa 0717 396 253 kisha tuma ujumbe kwa njia ya wasap 0717 396 253 wenye maneno KURASA KUMI na majina yako kamili na utaunganishwa kwenye kundi hili bora kabisa la kujisomea.

Wito wangu kwako rafiki yangu ni huu, kila mwezi, kazana usome angalau kitabu kimoja, mwanzo mpaka mwisho. Na njia bora ya wewe kuweza kufanya hivyo ni kujiunga na kundi hili la KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU.

Karibu sana kwenye mwaka wetu wa mafanikio 2018, karibu kwenye usomaji wa vitabu, uweze kufaidi maarifa bora sana kwa njia rahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog