The best revenge is to be unlike him who performed the injury. – Marcus Aurelius

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni siku mpya ambayo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari; NJIA BORA YA KULIPA KISASI…
Mtu akikutukana, na wewe ukamtukana, inakuwa umejitofautishaje na yeye?
Mtu akikusema vibaya na wewe ukamsema vibaya, si wote mnakuwa kwenye kundi moja?
Mtu akikuibia na wewe ukamuibia, wote mnakuwa ni wezi.

Kumfanyia mtu kile ambacho amekufanyia na hakikupendeza, ni kuamua kuwa kama yeye, hivyo haitakuwa na msaada kwa yeyote yule, wewe au yeye.

Njia bora ya kulipa kisasi ni kuwa kinyume na yule aliyekufanyia ubaya, kufanya kinyume na kile alichokufanyia.
Kwa kufanya hivi, wewe unakuwa na nguvu zaidi, unajitofautisha na yeye anakuwa dhaifu.

Ni rahisi kuona kwamba kumjibu mtu kwa kile alichokufanyia ni kumfundisha somo, lakini ukweli ni kwamba huwezi kumfundisha yeyote somo, badala yake unakuwa umechagua kufanana na yeye.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya iuwa bora zaidi kuliko changamoto yoyote utakayokutana nayo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha