Watu wamekuwa wakisema fedha au utajiri siyo mzuri, kwa sababu wakiwaangalia baadhi ya watu wenye fedha na utajiri, wamekuwa watumwa kwa fedha na utajiri wao.

Mtu anakuwa na fedha na mali nyingi, lakini bado haridhiki, anaona kuna kitu anakosa, anazidi kutaka zaidi na zaidi.

Hiyo hali ya kutaka zaidi na zaidi ndiyo inawafanya watu kuwa watumwa, na mbaya zaidi kujiingiza kwenye matatizo makubwa zaidi.

Masikini

Uhuru, uvumilivu na nguvu ni zao la kuwa na mahitaji madogo. Hata kama una fedha na mali nyingi, lakini kadiri unavyokuwa na mahitaji madogo, kadiri ambavyo ukipoteza kila ulichonacho maisha yako yanaendelea bila ya shida, ndivyo unavyokuwa huru, ndivyo unavyoweza kuvumilia mengi na ndiyo unakuwa na nguvu kubwa pia.

Kama hofu ya kupoteza chochote ulichonacho haikunyimi usingizi unapolala usiku, kama hata kila ulichonacho kikipotea maisha yataendelea kuwa bora kwako, una uhuru mkubwa, unaweza kuvumilia makubwa na nguvu zako ni kubwa pia.

SOMA; UKURASA WA 1004; Unapojishikiza Kwenye Vitu, Unapoteza Uhuru Wako…

Hii haimaanishi kwamba usiwe na fedha au utajiri, bali inamaanisha usiwe mtumwa wa vitu hivyo. Kuwa navyo kwa kujua msingi wake, kwamba vinapatikana kwa kutoa thamani, hivyo hata vikipotea, una nafasi ya kuendelea kutoa thamani na ukavipata tena.

Usione kama umepata kwa bahati na hivyo kukumbatia muda wote, utajinyima uhuru, kukosa uvumilivu na pia kukosa nguvu. Wale wanaopoteza mali zao na maisha yao kuvurugika ni wale ambao wameweka mategemeo ya maisha yao yote kwenye mali hizo. Usiwe mmoja wao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog