Tunaishi kwenye dunia ya kutumia, dunia ambayo kila tatizo au changamoto unayopitia, kuna kitu watu wanakushawishi utumie. Kwamba ukitumia kitu hicho basi matatizo yako yote yataisha na maisha yako yatakuwa kama unavyotaka.
Kama uzito wako umepitiliza basi unahitaji kutumia dawa ya kupunguza uzito, ndivyo dunia inavyotuambia, na wengi wanakimbilia kutumia dawa hizo, na huenda uzito ukapungua kwa muda, lakini unarudi pale pale na huenda zaidi baada ya muda.

Kama muda ni changamoto kwako basi unaambiwa kuna programu ya simu janja (app) ya kutumia ambayo itakuwezesha kusimamia muda wako vizuri. Hivyo kila mtu anakimbilia kuwa na programu hiyo, akiamini itatatua matatizo yake yote ya muda. Anakuwa nayo na siku za mwanzo inaweza kuonesha matokeo mazuri, lakini baadaye changamoto za muda zinaendelea kuwepo.
Ukweli ni kwamba, matatizo na changamoto nyingi unazopitia kwenye maisha yako, hazihitaji wewe utumie chochote. Achana na dunia inayotaka kukuuzia kila aina ya kitu, na ujue ukweli halisi wa matatizo au changamoto unazotumia.
Hata kwa upande wa afya, siyo kila kinachokuuma kinakutaka wewe utumie chochote, siyo kila maumivu yanahitaji dawa.
SOMA; UKURASA WA 459; Ulaji Na Uzalishaji…
Kama huhitaji kutumia kitu kwenye kila changamoto, unahitaji nini basi?
Unahitaji kujijua wewe mwenyewe kwanza, unahitaji kujua udhaifu wako uko wapi na ubora wako uko wapi. Unahitaji kujua vitu gani unaweza kufanya kwa ubora zaidi. Na unahitaji kujua tabia zinazokurudisha nyuma na tabia unazohitaji ili kupiga hatua zaidi.
Unahitaji kuwa na nidhamu binafsi, uweze kujiambia hapana, uweze kujisukuma kuchukua hatua hata pale unaposhawishika kuacha kuchukua hatua. Uweze kufanya kila ulichopanga kufanya, bila ya kuahirisha.
Unahitaji kuwa tayari kukataa raha ya sasa ili kupata furaha ya baadaye. Uweze kujikatalia kupata kitu unachotaka sasa, ambacho kinaweza kuwa kizuri, ili uweze kupata ambacho ni bora zaidi kwa baadaye.
Na zaidi unahitaji kuweka kazi, kazi kubwa sana, ufanye kazi kwa juhudi kubwa, ujitume, uende hatua ya ziada.
Kwa haya, utaweza kutatua changamoto na matatizo mengi kwenye maisha yako, na haitakuwa imekugharimu chochote kama wale wanaokuambia utumia kitu watakavyokugharimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Ni kweli kabisa, tunadiri matokeo ya matatizo badala ya kudili sababu iliyopelekea lile tatizo. Mtu akiona ni mnene anachotaka ni kuondoa tu ule unene bila kuangalia sababu iliyopelekea unene.
LikeLike
Kabisa,
Na bila kuondoa mzizi, tatizo linaendelea kurudi.
LikeLike