Ipo dhana kwamba watu wenye ufanisi mkubwa, watu wanaozalisha kwa kiasi kikubwa ni watu ambao wapo ‘bize’ muda wote, watu ambao wanaweza kukamilisha mambo mengi zaidi, watu ambao wanaweza kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Yote hayo ni uongo. Yote hayo yanawazuia wengi kufanya yale muhimu na kuyafanya vizuri na hatimaye kujikuta wakishindwa kupiga hatua kwenye maisha yao.

Kama

Ufanisi na hata uzalishaji bora siyo kwenye wingi wa vitu ambavyo mtu anaweza kufanya ndani ya muda fulani. Bali ni kwenye ubora wa vitu ambavyo mtu anafanya kwa ukamilifu ndani ya muda fulani.

Kama umefanya vitu kumi, lakini vyote umeishia katikati, hujakamilisha hata kitu kimoja, ni bora aliyefanya vitu vitatu na kuvikamilisha kabisa. Kwa sababu yule aliyekamilisha ana vitu vitatu vya kuonesha amefanya ila wa vitu kumi hana chochote cha kuonesha.

SOMA; Tabia Saba (07) Za Watu Wenye Ufanisi Mkubwa, Na Wanaofanikiwa Sana.

Hivyo unapotaka kuongeza ufanisi wako, unapotaka kuwa na uzalishaji wenye maana, unapotaka kutumia muda wako vizuri, usikazane kufanya kila kitu, wala usitake kuonekana upo ‘bize’, wala usitake kufanya mengi kwa wakati mmoja.

Badala yake jua mambo yapi ni muhimu zaidi kwa kile unachotaka kufikia kisha fanya hayo. Katika mambo mengi unayotaka kufanya, kuna machache ambayo ni muhimu kabisa, ambayo kwa kukamilisha hayo, inakusogeza karibu zaidi na kile unachotaka.

Jukumu lako ni kujua mambo hayo muhimu na kuweka juhudi kwenye kuyafanya ili kuhakikisha muda wako unautumia vizuri. Hayo mengine ambayo siyo muhimu utashangaa yanakamilika bila hata ya wewe kuyafanya, au yanapotea yenyewe.

Usikazane kufanya kila kitu, usikazane na wingi, kazana na ubora, kazana na yale ambayo ni muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog