Watu wanajifunza sana, watu wanakutana na vitu vipya, ambavyo vinaweza kubadili sana maisha yao, iwapo watachukua hatua.

Lakini wanasubiri, wanasubiri kwa sababu hawajapata uhakika wa kile wanachokwenda kufanya. Hawajajua kama ni hatua sahihi kuchukua. Wanajiona hawajakamilika, hivyo wanasubiri.

Kwa namna hii, wanajikuta hawachukui hatua yoyote, au wanapokuja kufikia hatua ya kujiona wapo sahihi kuchukua hatua, wanakuwa wameshachelewa sana.

wp-image--1138462510

Rafiki, kuchukua hatua yoyote ni muhimu kuliko kuwa sahihi. Unapochukua hatua unatoka pale ulipo sasa na kwenda mbele zaidi. Hata kama hatua uliyochukua siyo sahihi, utajifunza mengi kwa kuchukua hatua kuliko kutokuchukua hatua.

Na muhimu zaidi, kwa kuchukua hatua unakuwa kwenye mwendo, na ni rahisi kuchukua hatua nyingine zaidi unapokuwa umeshachukua hatua. Ni rahisi kuchukua hatua nyingine ukiwa umeshachukua hatua kuliko kuanza kuchukua hatua kwa mara ya kwanza.

Unapojifunza kitu chochote kipya, unapokutana na kitu ambacho hukuwa unajua, chagua kuchukua hatua mara moja. Usijali sana kama ni hatua sahihi au la, kama umeshawishika ni kitu kinachoweza kukutoa hapo ulipo, chukua hatua. Utaendelea kujifunza mengine wakati unaendelea kwenda.

SOMA; UKURASA WA 1073; Darasa La Kushindwa Kwako….

Wakati mwingine hatua unazotaka kuchukua zinaweza kuwa na hatari ndani yake, lakini pia kitu kisicho na hatari kabisa kinaweza kisiwe na manufaa kabisa pia. Hivyo hatari isikuzuie kuchukua hatua, badala yake angalia unapunguzaje madhara ya hatari hiyo. Lakini kuchukua hatua ni LAZIMA.

Maisha yako hayawezi kubadilika kama utaendelea kuwa hivyo ulivyo, lazima uchukue hatua za tofauti. Na siyo kila hatua utakayochukua itakuletea matokeo unayotarajia kupata, wakati mwingine utakuwa unajifunza.

Chukua hatua kila unapokutana na fursa ya kuchukua hatua, na usiogope kwamba siyo hatua sahihi, muhimu ni kuchukua hatua kwanza, kisha kujifunza na kusonga mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog