Aliyekuwa raisi wa Marekani, John F. Kennedy aliwahi kunukuliwa akisema, usiulize nchi yako inakufanyia nini, bali jiulize wewe unaifanyia nini nchi yako. Ni kauli muhimu sana kwenye uwajibikaji na uzalendo, kwa sababu matendo ya kila mtu ndiyo yanaishia kuwa matendo ya taifa.

Mimi nakuletea kauli kama hii, lakini kwa upande wa biashara ambapo nakuambia usijiulize wewe unataka nini, bali jiulize dunia inataka nini.

Chochote kile ambacho unakitaka hapa duniani, utakipata kutoka kwa wengine, lakini sasa, wengine hawahangaiki sana na kile unachotaka wewe. Bali kila mtu anahangaika na kile anachotaka yeye.

unaifanyia nini nchi

Hivyo kupata chochote unachotaka, usikazane kujiuliza unataka nini, bali kazana kujiuliza wengine wanataka nini. Jiulize dunia inataka nini, na ipe dunia kile ambacho inataka, hapo utapata nafasi ya kupata kile unachotaka wewe.

Dunia haijali kama unataka kuwa bilionea, kuwa na mali, kuwa maarufu au chochote. Dunia inachotaka ni kutimiziwa mahitaji yake. Watu wana shida, watu wana changamoto na hayo ndiyo wanayofikiria kwa muda mrefu.

SOMA; UKURASA WA 930; Dunia Haihitaji Mwongeaji Mwingine…

Jiulize wewe unawezaje kuisaidia dunia kwa matatizo na changamoto ambazo watu wanapitia. Jiulize ni kwa namna gani uwezo ulionao, vipaji ulivyo navyo, ujuzi, uzoefu na muda wako unaweza kuutumia kuisaidia dunia kupiga hatua.

Jiulize ni kitu gani unachoweza kutoa wewe, ambacho watu hawawezi kupata sehemu nyingine yoyote. Jiulize ni kitu gani unachoweza kufanya, ambacho kompyuta yoyote haiwezi kufanya zaidi yako, ambacho hata kama kuna maroboti yanakuja, hayataweza kukuondoa wewe.

Kwa njia hii, utakuwa na uhakika wa kupata chochote unachotaka, kwa kukazana kuipa dunia kile inachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog