Kitu kimoja ambacho sisi binadamu tunacho ni kusahau, tunasahau mambo haraka sana. Na hili siyo baya, bali ni jambo zuri kwa sababu yapo mambo ambayo kama siyo kusahau basi maisha yetu yatakuwa hovyo.

Kuna mambo makubwa, magumu na mabaya tunakutana nayo kwenye maisha yetu ambayo kama siyo kusahau, tunaweza kukata tamaa na maisha. Misiba ya watu wa karibu, ajali mbalimbali na hata magumu ambayo tunaweza kuwa tumeyapitia kwenye maisha.

Changamoto kubwa ni kwamba, akili zetu zinasahau na hazijui kuchagua lipi la kusahau na lipi la kuacha. Hivyo kwa yale mambo ambayo sisi hatutaki kuyasahau basi tunahitaji kuchukua hatua ili tusiyasahau.

Muda tulionao

Njia bora ya kutosahau yale muhimu ni kujikumbusha. Tena kujikumbusha kila siku kuhusiana na yale muhimu sana unayohitaji kwenye maisha yako.

Hii ndiyo maana ni muhimu sana kuandika ndoto zako, maono yako, malengo yako na mipango yako kila siku. Unapoamka, chukua kalamu na kijitabu chako na andika picha kubwa ya maisha yako na jinsi unavyotaka siku yako iende.

SOMA; UKURASA WA 947; unapopata shida ya kuamka asubuhi, jikumbushe hili…

Kwa kujikumbusha huku, mawazo ya kile unachotaka yanakuwa kwenye akili yako mara zote na hivyo inapojitokeza fursa ya kukuwezesha kuchukua hatua unaiona na kuweza kuitumia haraka.

Jikumbushe kila siku, na tena jikumbushe kwa kuandika, hii ndiyo njia pekee ya kujihakikishia kwamba hutosahau yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog