While we are postponing, life speeds by. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Leo tunakwenda kuishi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana.
Pia kwa TATUA, AMUA NA ONGOZA, tutaweza kupiga hatua kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Asubuhi hii tubatafakari MAISHA HAYAKUSUBIRI WEWE…
Hakuna kitu rahisi duniani kama kuahirisha mambo.
Kuna kitu ulipanga kufanya, muda uliopanga kufanya unafika lakini unajiona hujawa tayari, hivyo unaahirisha.
Unajiambia nitafanya kesho, nitakuwa tayari zaidi kesho, au mambo yatakuwa mazuri zaidi kesho.

Ukweli ni kwamba, wewe unaweza kuahirisha utakavyo, lakini maisha hayaahirishi, wala maisha hayakusubiri. Maisha yanaendelea kusonga mbele, na hivyo kama wewe unaahirisha, unakuwa umechagua kupoteza.

Unaposema leo haupo tayari na hivyo utafanya kesho, jua unaiba muda wa kesho, hivyo chochote bora ambacho ungeweza kufanya hiyo kesho hutakifanya, badala yake itabidi ufanye kile ulichoahirisha.
Na hapo ni kama pia utafanya kama ulivyopanga kwenye kuahirisha, lakini kama utaahirisha tena, tatizo litakuwa kubwa zaidi na zaidi.

Hivyo rafiki, kila wakati jikumbushe kwamba maisha hayasubiri, jikumbushe kwamba maisha hayasimami, maisha yanaendelea kusonga mbele. Hivyo unapoahirisha jambo lolote, unajiibia maisha yako, unajirudisha nyuma.
Panga kufanya kitu na kifanye kweli, au usikifanye kabisa na songa mbele. Kuendeleza tabianya kuahirisha mambo kutakuwa kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa.

Chochite ulichopanga kufanya, tenga muda na kifanye, usikimbilie kuahirisha, maisha hayakusubiri wewe mpaka uwe tayari, maisha ni zile hatua unazoweza kupiga kwenye maisha yako.

Nenda kachukue hatua leo bila ya kuahirisha,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha