Tunadanganyika kwamba uhuru ni kuweza kupata kila unachokitaka kwa namna unavyotaka wewe. Na mafanikio ni kuwa na kila unachokitaka kwa namna unavyotaka wewe.
Yote hayo mawili ni uongo kwa sababu hakuna yeyote anayeweza kupata kila anachokitaka kwa wakati anaotaka na namna anavyotaka yeye. Kuna wewe kutaka na kuna dunia kutoa. Huna nguvu ya kuilazimisha dunia ifanye kile wewe unataka ifanye.
Wanafalsafa wamekuwa wakikubaliana kwenye hili; uhuru ni kutaka machache uwezavyo na mafanikio ni kuridhika na kufurahia kile ulichonacho, huku ukiendelea kuwa bora zaidi. Unaona hapo, siyo wingi wala kuwa na kila unachotaka, bali uchache na kuridhika na kile ulichonacho.

Sasa vipo vitu vitabu ambavyo ukijijengea uwezo, utaweza kuwa na maisha ya uhuru na mafanikio.
Moja; uwezo wa kufikiri.
Unaweza kuona hili ni la kawaida na unafanya kila siku, lakini ukweli ni kwamba watu hawafikiri. Kabisa yaani, watu wanafanya kwa mazoea na kuangalia wengine wanafanya nini. Lakini wao kukaa chini na kufikiri kwa kina kwa nini wanafanya au wanafanyaje kwa ubora, hawafanyi hivyo.
Mbili; uwezo wa kufunga.
Kuna watu huwa wanajiuliza tunakula ili tuishi au tunaishi ili tule? Swali hilo wala halina maana sana, ila ukweli ni kwamba watu wanakula sana. Watu wamekuwa watumwa wa vyakula. Watu hawawezi kuchukua muda bila ya kula. Na huu ulaji ndiyo umeleta matatizo makubwa sana kwa walio wengi.
Uwezo wa kufunga, kuacha kula wakati chakula unacho, unakujenga uhuru mkubwa sana. Unakufanya wewe uwe mwamuzi, uwe msimamizi wa maisha yako badala ya kusukumwa na mwili kufanya kila mwili unachotaka ufanye.
SOMA; UKURASA WA 939; Sikiliza Zaidi Ya Unavyoongea…
Tatu; uwezo wa kusubiri.
Sina haja ya kueleza hili sana, lakini zama tunazoishi ni zama za mtu kutaka kitu, lakini kukitaka jana. Yaani watu wana haraka na hakuna mwenye subira. Tumeshakuwa na mtazamo kwamba chochote tunachotaka lazima tukipate sasa, na siyo nje ya hapo.
Kwa njia hii tunalazimisha vitu ambavyo haviwezekani na mwishowe tunaishia kuumia au kukosa kabisa hata kile ambacho tulikuwa nacho.
Jijengee uwezo wa kufikiri kwa akili yako, hii itakufanya uwe huru na kujua nini unafanya na kwa nini. Jijengee uwezo w akuacha kula kwa kipindi, hii itakujengea nidhamu. Pia jijengee uwezo wa kuwa na subira, hii itakuwezesha kupata mambo mazuri kwa wakati wake.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog