Ni jambo la kushangaza namna gani watu wapo tayari kuacha ndoto zao kwa sababu ya maoni au mtazamo wa watu wengine.

Au mtu anaacha kufanyia kazi ndoto zake kubwa alizokuwa nazo, kwa sababu ya watu ambao wanamhitaji afanyie kazi vitu vingine.

Cha kushangaza ni kwamba, watu wengi ambao watu wanawakubalia wawe ukomo wa ndoto zao, walikuja baada ya ndoto zao. Yaani walikutana na watu hao, wakiwa tayari wameshakuwa na ndoto hizo kubwa.

Ulinzi

Kwa mfano kama tangu ukiwa mtoto ndoto yako ni kuwa mjasiriamali mkubwa, au kuwa mwandishi au kuwa chochote unachotaka kuwa, lakini baada ya kuona au kuolewa ukatumia ndoa yako kama sababu ya kutokuendelea kupigania ndoto zako unakuwa hujitendei haki.

Au kama umekuwa na ndoto kubwa kabla hujawa na watoto, lakini baada ya kuwa na watoto ukajikuta wamekupa majukumu makubwa kiasi kwamba huwezi tena kufanyia kazi ndoto zako. Au ni ajira, ambayo uliianza ukiwa na maono ya kuifanya kwa muda mfupi na baadaye kufanyia kazi ndoto zako, lakini inakuwa imekubana kiasi kwamba huwezi tena kufanyia kazi ndoto zako.

Hapa unakuwa umejidhulumu wewe mwenyewe. Hii ni kwa sababu, watu wote hao unaowatumia kama sababu ya kutofikia ndoto zako, wamekuja baada ya ndoto zako. Hivyo hawapaswi kwa namna yoyote ile kuwa kizuizi cha wewe kufikia ndoto zako.

Ndoto za maisha yako, zinapaswa kuwa kipaumbele kikubwa kwako, kwa sababu yale ndiyo maisha yako, ndoto zile ndiye wewe na hautakuwa na maisha yenye maana na ukamilifu, kama utaacha kufanyia kazi ndoto zako huku ukijua kabisa umeacha kuzifanyia kazi.

SOMA; UKURASA WA 906; Jipe Sababu Ya Kujithamini…

Ni wakati sasa wa kusimama na kutetea ndoto zako, kwa sababu haijalishi watu wanakupenda na kukujali kiasi gani, hawana ndoto zako. Ndoto hizi ni zako, ni wewe pekee unayeweza kuzielewa, ni wewe pekee ambaye ndoto hizo zina maana kwako.

Kitakachoyafanya maisha yako kuwa na maana na kuwa na tofauti ni zile ndoto kubwa ulizonazo, ambazo haziondoki kabisa kwenye mawazo yako. Fanyia kazi ndoto hizo, ishi ndoto hizo na utaacha alama hapa duniani.

Yeyote aliyekuja baada ya ndoto zako, anapaswa kuziheshimu ndoto zako. Na ni vyema ukawa unawaambia mapema na kuwakumbusha kuhusu ndoto zako, ili pasitokee mgongano wa kimaslahi baina ya ndoto zako na ndoto zao.

Unaweza kuvumilia kukubali kubadili mambo yote kwenye maisha yako, iwe ni tabia, dini au hata kabila kwa ajili ya wengine. Lakini kamwe usikubali kubadili ndoto kubwa za maisha yako kwa ajili ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog