Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye utaratibu huu mpya, ambapo kila mwisho wa wiki, siku ya jumamosi nitakuwa nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza au kukutana nayo kwenye wiki husika, ambapo kuna kitu na wewe rafiki yangu unaweza kujifunza.

Nikukumbushe kwamba kusudi kuu la maisha yangu ni kuhakikisha nawawezesha watu wengi ipasavyo kupata maarifa sahihi ya kuwawezesha kuchukua hatua sahihi na kufanikiwa.

Hivyo nimekuwa natumia kila fursa kufanikisha hilo. Kupitia makala za bure kabisa kwenye AMKA MTANZANIA, kupitia vitabu ninavyoandika, kupitia kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA, kundi la KURASA KUMI ZA KITABU na hata huduma za UKOCHA ninazotoa.

Mfumo huu mpya wa tano za juma utakuwa unagusia maeneo yafuatayo;

  1. Kitabu/vitabu ninavyosoma kwa wiki husika na kitu kimoja cha wewe kufanyia kazi.
  2. Makala moja muhimu ya wiki ambayo unapaswa kuisoma, yangu au hata ya wengine.
  3. Kitu kipya nilichokutana nacho, kujifunza au wazo jipya nililokutana nalo.
  4. Huduma zangu mbalimbali ninazotoa na nafasi zinazopatikana.
  5. Neno la kutafakari na lililonifikirisha sana.

Mambo haya matano yatakufanya umalize wiki ukiwa imara zaidi na ukiwa na maarifa bora ya kukuwezesha kuchukua hatua.

Katika juma hili la tatu la mwaka 2018, na kwa mara ya kwanza, nikushirikishe yale matano muhimu ya juma hili.

#1. Kitabu ninachosoma; 33 STRATEGIES OF WAR.

Kwanza unaweza kujiuliza kwa nini nasoma kitabu cha mbinu za kivita, kwamba napanga kupigana vita? Au kipi cha kujifunza kwenye mbinu za kivita?

Ukweli ni kwamba maisha yetu ya kila siku ni vita. Kuna watu wamejipanga kukuzia wewe usipate kile unachotaka, na wapo tayari kufanya kila jitihada kukamilisha hilo.

Ubaya zaidi ni kwamba, watu hawa huwa hawajioneshi wazi wazi, wengi ni watu wa karibu, ambao unaweza kufikiri wapo mstari wa mbele kukusaidia. Utawaona wakikusifia sana, lakini kichini chini wanafanya kila jitihada uanguke.

Hivyo kuwa macho, kwa chochote unachofanya, usifikiri kila mtu anafurahia au anakutakia mema. Lakini pia usioneshe hilo wazi wazi, ndiyo maana unahitaji kuwa na mbinu za kivita, za kuhakikisha unamjua adui ambaye amevaa ngozi ya kondoo kumbe ndani ni mbwa mwitu.

Kitabu kizuri sana kusoma, hatakama hutaishi kila mbinu, lakini utawajua binadamu vizuri, hasa kwa tabia ambazo hawaoneshi wazi wazi.

#2. Makala ya kusoma.

Wiki hii niliandika makala kuhusu sababu kumi za kila mtu kuwa na biashara mwaka huu 2018. Ni makala muhimu sana kwa kila ambaye anafikiria kuanza biashara ila hajui aanzie wapi. Unaweza kusoma makala hiyo hapa; Sababu Kumi (10) Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Biashara Mwaka Huu 2018. (https://amkamtanzania.com/2018/01/19/sababu-kumi-10-kwa-nini-unapaswa-kuwa-na-biashara-mwaka-huu-2018/ )

#3. Nilichokutana nacho; #ShitHole.

Tangu mwaka huu umeanza sipo kabisa kwenye mitandao ya kijamii. Sijatembelea kabisa facebook, linkedin, instagram na ni jana tu nilifungua twitter. Sasa ukichanganya na kwamba huwa siangalii tv, kusikiliza redio na wala kusoma magazeti, nimekuwa sipati mara moja kila kinachoendelea, na hivyo imekuwa bora sana kwangu.

Sasa wiki hii kila ninapokuwepo nasikia watu wakiongea kwa hasira huyu Trump hafai kabisa, hawezi kututukana kiasi hichi. Sasa wengi waliokuwa wanazungumza wanaonekana hata hawaelewi kwa kina wanachosema. Wanasema tu neno #Shithole.

Ndipo nilipoamua kuingia google na kusearch maneno mawili TRUMP SHITHOLE. Ndipo nilipokutana na taarifa nyingi kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump alinukuliwa akisema baadhi ya nchi ni Shitholes, yaani ni nchi za hivyo, zisizostaarabika kama lilivyo shimo la choo.

Nimekuwa namfuatilia Trump tangu mwaka 2012 nilipoanza kusoma vitabu vyake, na nimekuwa namjua kwa namna ambavyo huwa hachagui maneno wala kubembeleza watu. Sijui kama alisema hayo kweli au alisema yapi, ninachoweza kuwa na uhakika nacho ni kwamba alitumia maneno makali dhidi ya nchi zetu hizi zinazoendelea.

Sasa katika kukabiliana na hili, naona watu wamegawanyika, wapo wanaosema tupo sahihi na wapo wanaosema amekosea sana. Mimi nasema yupo sahihi na hayupo sahihi. Ninachosema ni kwamba, mtu akikutukana, angalia kama alichosema kina ukweli, kama ni kweli jirekebishe, kama siyo kweli mpuuze.

#4. Huduma ninazotoa. KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU.

Kama umekuwa unapata shida ya kusoma vitabu, na umekuwa unaona wenzako wanasema wamesoma vitabu vingi, na wewe pia unaweza. Kuna kundi maalumu la wasap ambalo nimetengeneza, kundi hili linakuwezesha kusoma kurasa 10 za kitabu kila siku.

Jiunge na kundi hili na utaweza kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi, vitabu 12 kwa mwaka. Ukiweza hilo utakuwa mbali sana mwisho wa mwaka huu 2018.

Kujiunga tuma ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 wenye maneno KURASA KUMI, nitakupa maelekezo.

Usomaji

#5. Neno la tafakari, linalonifikirisha sana.

“To be truly positive in the eyes of some, you have to risk appearing negative in the eyes of others.” ― Criss Jami

Ili uonekane chanya mbele ya baadhi ya watu, lazima uwe tayari kuonekana hasi mbele ya watu wengine.

Hii ni sawa na ile kwamba ili uonekane mzuri kwa baadhi ya watu, lazima uonekane mbaya kwa wengine.

Kwamba huwezi kumridhisha kila mtu, hivyo hata kama pamoja na kujitahidi kuna watu wanakuambia hakuna unachofanya, jua hao siyo unaowalenga. Kazana na wale unaowalenga.

Nina imani yapo uliyojifunza na hatua unazoweza kuchukua kwenye TANO ZA JUMA. Kikubwa ni wewe kuchukua hatua rafiki yangu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog