Mwaka huu 2018 ni mwaka ambao moja ya malengo ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo ni malengo ya kibiashara. Kama bado hujawa na biashara basi unapaswa kuanza biashara yako mwaka huu. Na kama tayari una biashara, basi unapaswa kuikuza zaidi biashara yako mwaka huu 2018.

Kwenye makala iliyopita, niliandika sababu 10 kwa nini kila mtu anapaswa kuwa na biashara mwaka huu 2018. Wapo waliosema kwamba sababu ni nzuri lakini nyakati ni ngumu, mambo yamekuwa magumu na biashara zinafungwa.

Hivyo kwenye makala ya leo, nakwenda kukushirikisha biashara kumi unazoweza kuanza kufanya mwaka huu 2018 na ukawa na mafanikio makubwa, licha ya hali ya uchumi kuonekana kuwa ngumu.

Kabla hatujaangalia ni biashara zipi ambazo mtu unaweza kufanya mwaka huu 2018 kwa mafanikio, nataka nikupe kitu kimoja muhimu sana cha kuzingatia kwenye biashara yoyote utakayoanzisha.

Kitu  hicho ni kwamba, ingia kwenye biashara ambayo watu tayari wana uhitaji, usiingie kwenye biashara ambayo watu wanapenda au kutamani kile unachouza. Badala yake ingia kwenye biashara ambayo watu wana uhitaji wa kile unachouza. Yaani maisha yao hayawezi kwenda sawa kama hawapati kile ambacho unauza.

Kwa mfano, licha ya wengi kulalamika kwamba hali ya uchumi ni ngumu, bado watu wanaendelea kula chakula kila siku, si ndiyo? Nina uhakika hujakutana na watu wakitembea uchi kwa sababu uchumi ni mgumu, watu wanaendelea kuvaa nguo. Kadhalika watu wanaendelea kupata zile huduma ambazo ni muhimu kwa maisha yao kama chakula, malazi, mavazi, usafiri na hata mapumziko.

Hivyo unapofikiria biashara gani uanzishe, au unapokuwa na mawazo ya biashara lakini hujui uchagueje, angalia wapi uhitaji wa watu upo, na wewe toa uhitaji huo.

Nyakati zinapokuwa ngumu, usikazane kuwa na biashara ya kipekee, ambayo unahitaji kuanza kumshawishi mteja kwa nini anapaswa kununua unachouza. Ukishaona biashara unayofanya au unayotaka kufanya inakubidi uanze kumshawishi mteja kwa nini anapaswa kununua, hapo upo njia mbaya. Mteja anapaswa kujua tayari kwa nini anapaswa kununua, na avutiwe kununua kwako kwa huduma nzuri unazotoa.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Baada ya kupata maneno hayo muhimu ya utangulizi, kuhusu maamuzi ya biashara unayofanya, sasa tuliangalie biashara kumi unazoweza kuanza mwaka huu 2018 kwa mafanikio makubwa.

 1. Bidhaa za chakula.

Kwa kuwa watu bado wanakula, na wataendelea kula siku zijazo, kuanza biashara ya kuuza bidhaa za chakula ni hatua sahihi kwako kuchukua. Hapa unaweza kuuza na kusambaza bidhaa za chakula kama nafaka, mafuta na bidhaa nyingine muhimu.

Angalia uhitaji wa bidhaa za vyakula kwa wale wanaokuzunguka au unaoweza kuwafikia kisha wapatie bidhaa hizo kwa kiwango na gharama ambazo wanaweza kumudu huku wewe ukipata faidia ili biashara iweze kuendelea.

Uzuri wa biashara ya bidhaa za chakula unaweza kuanza na mtaji kidogo, ukatafuta bidhaa zilizo bora na kuweza kuwasambazia watu kule walipo.

Biashara ya mchele, mahindi, maharagwe na nafaka nyingine zina uhitaji mkubwa kwa watu.

 1. Huduma za chakula.

Biashara nyingine unayoweza kuanza kwa mafanikio mwaka huu 2018 ni biashara ya utoaji wa huduma za chakula. Hapa unatengeneza na kuuza chakula bora ambacho watu wanaweza kukimudu.

Uzuri wa biashara hii ni kwamba, watu wengi wanabanwa na kazi au biashara zao na hivyo hawawezi kuandaa vyakula vyao, hasa vya mchana. Hivyo kwa kuwajua watu wa aina hii na namna unavyoweza kuwafikia, unaweza kuwapatia chakula ambacho ni bora kwa gharama wanazoweza kulipia.

Kingine muhimu ni kwamba watu kwa sasa wanajali sana afya zao, hivyo wanakula mlo bora, unaweza kutumia nafasi hii kutoa vyakula bora kiafya badala ya vyakula vya haraka ambavyo siyo bora.

Unaweza pia kutoa huduma ya matunda, juisi na huduma nyingine za chakula kwa wale wenye uhitaji.

 1. Bidhaa za mavazi.

Kama ambavyo tumeona, watu wanaendelea kuvaa nguo, bila ya kujali mambo ni magumu au la. Hivyo unaweza kuingia kwenye biashara kwa kutoa bidhaa za mavazi. Hapa unauza mavazi kama nguo, viatu na mengineyo.

Unachohitaji hapa ni kujua uhitaji wa watu kwa wakati mbalimbali. Kwa mfano kipindi cha mwanzo wa mwaka bidhaa nyingi za mavazi zinazotoka ni zile zinazohusiana na mavazi ya shule. Pia katika kipindi cha sikukuu, watu wanajibana wawezavyo ili wavae nguo mpya.

Unapochagua kuingia kwenye biashara hii ya bidhaa za mavazi, angalia aina ya watu ambao ni wanunuaji wazuri. Mfano mavazi ya wanawake na watoto yanatoka zaidi kibiashara kuliko mavazi ya aina nyingine.

Uzuri wa biashara ya bidhaa za mavazi ni kwamba, unaweza kuianza kwa hatua ndogo sana, huhitaji hata kuwa na eneo la biashara. Unaweza kuchagua wateja unaowalenga, ukachagua bidhaa zao kisha kuwasambazia au kuwatangazia kwa njia ya mtandao.

 1. Biashara ya huduma za mavazi.

Huduma za mavazi ni aina nyingine ya biashara unayoweza kuanza, ambayo itakuwezesha kupiga hatua kubwa. Kama una ubunifu wa mavazi, au unaona uhitaji wa mavazi ya aina fulani, unaweza kutoa huduma ya kuandaa mavazi hayo.

Hapa tunazungumzia kutoa huduma ya kuwaandalia watu mavazi kwa namna wanavyoyataka. Pia kuwasaidia watu kurekebisha mavazi yao. Biashara hii unaweza kuifanya kama unao ufundi wa kutengeneza mavazi. Lakini hata kama huna, unaweza kupata mtu mwenye ufundi ukawa unampa maelekezo na wewe kuwa na kazi ya kutafuta masoko au kusambaza yale mavazi yanayotengenezwa.

Siku hizi zipo mashine ambazo ni rahisi kutumia kushona mavazi ya aina mbalimbali ambazo unaweza kuwa nazo na kuanza kiwanda chako kidogo cha mavazi.

 1. Ufugaji wa kibiashara – kuku.

Hakuna familia ya asili ya kiafrika ambayo haijawahi kufuga kuku. Na kuku ni moja ya wanyama ambao soko lake halijawahi kuyumba. Zimekuja biashara za ndege wa aina mbalimbali kama kware lakini zimepita na kuacha biashara ya kuku ikiwa imara. Huhitaji kumshawishi mtu kwamba anahitaji kula nyama ya kuku, au kula mayai, ni kitu ambacho kwa wengine ni ufahari.

Unaweza kuingia kwenye ufugaji wa kibiashara na kufuga kuku ambao utaweza kuuza mayai, kuuza vifaranga na hata kuuza kuku wenyewe. Unaweza kufuga kuku wa kienyeji, kuku chotara na hata kuku wa kisasa kabisa. Unachohitaji kuangalia ni uwezo wako na uhitaji wa soko unalolenga.

Uzuri wa ufugaji wa kuku ni kitu unaweza kuanza kwa hatua ndogo na kukuza. Pia unaweza kufanya huku ukiendelea kufanya vitu vingine. Pia itakuhitaji uwe makini ili ufugaji wako ukue.

 1. Ufugaji kibiashara – samaki.

Samaki ni chakula kingine ambacho kina uhitaji mkubwa sana kwenye jamii zetu.  Ni mboga ambayo ina uhitaji mkubwa na hivyo ukiweza kuzalisha kwa kiwango kizuri, ni biashara nzuri kwako kufanya.

Ufugaji wa samaki kwa sasa umerahisishwa kutokana na upatikanaji wa huduma muhimu za samaki. Huduma kama vyakula vya samaki, ujenzi bora wa mabwawa ya kufugia samaki zimefanya ufugaji wa kibiashara wa samaki kuwezekana.

Japo ufugaji wa samaki unahitaji mtaji mkubwa, inawezekana pia kuanza kidogo na ukafanya vizuri.

 1. Kilimo biashara – mbogamboga na matunda ya muda mfupi.

Hata kama uchumi ni mgumu kiasi gani, watu hawatakula chakula bila ya kitunguu, bila ya nyanya, bila ya bamia. Watu wataendelea kula mchicha, matembele na mboga nyingine. Na muhimu zaidi matunda kama matango, matikiti maji na hata ndizi ni vyakula ambavyo kila mtu ana uhitaji navyo.

Hivyo eneo unaloweza kuingia kibiashara mwaka 2018 kulingana na nafasi na uwezo wako ni kilimo biashara cha mbogamboga na matunda ya muda mfupi. Ninaposema kilimo biashara namaanisha ulime kwa lengo la kuuza, hivyo kulima kwa viwango vizuri na ubora ambao unakubalika na soko unalolenga.

Unaweza kulenga wanunuaji wa rejareja au kuuza kwa wanaonunua jumla, kama mahoteli au maduka makubwa.

 1. Kilimo biashara – mazao ya chakula.

Mazao ya chakula kama nafaka, mahindi, maharagwe na mpunga ndiyo mazao yanayoongoza kwa kuliwa sana kwenye jamii zetu. Hivyo hili ni eneo ambalo unaweza kuingia kibiashara na ukafanya vizuri kwa mwaka huu 2018. Unaweza kuingia kwenye kilimo moja kwa moja na ukalima kibiashara, kwa njia ambayo utazalisha kwa kiwango kikubwa na kwa ubora wa kuweza kuuza.

Lakini pia kama huwezi kulima, kwa kukosa nafasi au usimamizi mzuri, unaweza kununua mazao hayo kwa wingi kwenye msimu wa mavuno, kuyaongeza thamani na kuyauza kwa wahitaji. Mfano kununua mpunga wakati wa mavuno, kuukoboa, kuuhifadhi kwenye vifungashio vizuri na kuuza kwa watumiaji ni biashara ambayo inaweza kukupeleka kwenye mafanikio makubwa 2018.

 1. Biashara ya vyakula vya mifugo na huduma zake.

Watu sasa wanafuga, kuanzia kuku, mbuzi, ng’ombe, sungura, samaki na kadhalika. Unaweza kuingia kwenye biashara kwa kutoa huduma mbalimbali za kuwezesha wafugaji kupata mafanikio kwenye ufugaji wao.

Hapa unaweza kuingia kwenye biashara ya kuuza vyakula vya mifugo, kuuza madawa na virutubisho vya mifugo na hata kutoa huduma za vyakula mbadala kwa wafugaji.

Na kama wewe ni mfugaji au una utaalamu kuhusu mifugo, unaweza kutoa ushauri kwa wafugaji kibiashara pia.

 1. Huduma za ushauri wa kitaalamu.

Kwa jambo lolote ambalo umesomea, au umeshakuwa na uzoefu nalo, kuna watu ambao wamekwama na hawajui wafanye nini. Hapa unaweza kuingia kwenye biashara ya kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa lile eneo ambalo una utaalamu au uzoefu nalo.

Kama umesomea mambo ya afya unaweza kutoa ushauri wa kiafya kwa watu na wakakulipa. Kama umesomea au una uzoefu kwenye biashara, unaweza kuwashauri watu kuhusu biashara na wakakulipa.

Angalia kipi unajua na watu hawajui, kisha wape ushauri kwa njia ambayo watakulipa.

KIPATO KWA BLOG

Nyongeza; uza taarifa na maarifa kwa njia ya mtandao wa intaneti.

Tunaishi kwenye zama za kipekee sana, zama ambazo kila mtu anaweza kuzalisha chochote anachoweza kuzalisha bila ya kuziwa na yeyote, kama tu havunji sheria.

Hivyo kama kuna vitu unafahamu, kupitia uzoefu, kujifunza au kutafiti, ambavyo vinaweza kuwasaidia watu, unaweza kuweka kwenye njia ambayo watu wanaweza kununua.

Unaweza kuweka kwenye mfumo wa kitabu na kuwauzia watu, unaweza kuandaa kwa mfumo wa semina au kozi ambayo watu wanajiandikisha na kusoma.

Uzuri ni kwamba, yote hayo unaweza kuyafanya bila hata ya kuwa na eneo la biashara, bila hata ya kuweka shilingi mia. Unachohitaji ni kutumia vizuri mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kuwafikia wale wenye uhitaji na kuwapa taarifa na maarifa yanayoweza kuwasaidia.

Hizo ndizo biashara kumi, na nyongeza unazoweza kufanya mwaka huu 2018 na ukaweza kupiga hatua kubwa kwenye mafanikio.

Muhimu; katika makala hii, nimegusia kwa juu kuhusu kila biashara niliyotaja, kabla hujaingia kwenye biashara yoyote kati ya hizo, na hata nyingine yoyote, fanya utafiti wako, jifunze kuhusu biashara hiyo, ongea na wanaofanya biashara hiyo, ongea na wenye uhitaji wa biashara hiyo, kisha jua unaingiaje ili kutoa thamani zaidi.

Muhimu zaidi; asikudanganye mtu yeyote kwamba ipo biashara ya mkato na ya haraka ya kufanikiwa, kila biashara itakuhitaji uweke juhudi kubwa, uwe mvumilivu na uweke muda ili kufanikiwa. Hivyo unapochagua kuingia kwenye biashara yoyote, ingia ukijua hilo, itakusaidia kupambana.

Rasilimali nilizokuandalia ili ufanikiwe kwenye biashara mwaka huu 2018.

Kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha, zipo rasilimali nyingi ambazo nimeandaa kwa ajili yako. Rasilimali hizi zinakuwezesha wewe kuchukua hatua kwenye haya ninayokushauri ili uweze kuona mafanikio makubwa.

 1. Kitabu; Biashara ndani ya ajira, jina lisikupoteze, hichi ni kitabu kizuri sana katika kuanzisha na kukuza biashara yako, hata kama huna muda kabisa. kukipata tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253.
 2. Kitabu; JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG. Kama unataka kuingiza kipato kupitia mtandao wa intaneti, huku ukiendelea kufanya yale unayofanya, hicho ndiyo kitabu cha kusoma. Kukipata tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253 na utapata maelekezo ya kukipata.
 3. KISIMA CHA MAARIFA, hili ni kundi maalumu la wasap ambalo kila siku utajifunza na kuhamasika kuweza kupiga hatua kubwa kila siku. Kama unapanga kuanza biashara 2018, au tayari una biashara lakini inasuasua, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, utapata maarifa sahihi ya kukuwezesha kufanikiwa.

Karibu sana rafiki yangu, iwe utachukua hatua kwenye rasilimali hizo nilizokutajia au la, ninachokuomba ni kimoja, anza biashara mwaka huu 2018, utajifunza mengi na utanunua uhuru wako. Na kama tayari una biashara, kazana kuikuza biashara hiyo zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog