Habari rafiki?

Karibu kwenye makala hii ya #TANO za juma ambapo ninakushirikisha mambo matano muhimu niliyokutana nayo au kujifunza kwa juma zima.

Kupitia mambo haya, wewe rafiki yangu utajifunza na kuweza kuchukua ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#NENO;

Ulianza kusemwa tangu uko darasa la tano, na mpaka sasa hakuna neno ulilosemwa likakatisha maisha yako. Nimeona watu wengi wamekuwa wakishindwa kuishi maisha yao kwa sababu wanaogopa watu watawasema vibaya, au watawachukulia kwa namna tofauti. Rafiki, kazi ya watu ni kusema na hawajaanza kukusema leo. Simamia kile unachoamini, fanya kile unachotaka kufanya kwenye maisha yako na waache watu waseme vile wanavyotaka. Hata kama una hofu kwamba ukishindwa watu watakusema, shindwa na watu wakuseme ujifunze, na siyo kutokuchukua hatua na hivyo kutokujifunza kabisa.

#1 Kitabu ninachosoma; THE CHINA STRATEGY.

China imeweza kufanya mapinduzi makubwa sana kiuchumi kwa miongo miwili iliyopita. Na pia inatabiriwa kufanya mapinduzi makubwa zaidi kwenye miongo miwili ijayo, ambapo itakuwa taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi duniani.

Mwandishi Edward Tse, kwenye kitabu chake cha THE CHINA STRATEGY amechambua kwa kina jinsi ambavyo taifa hili limeweza kufanya mapinduzi haya makubwa kiuchumi, na jinsi ambavyo nchi, makampuni na hata watu binafsi wanaweza kutumia mikakati hiyo katika kukua zaidi.

Mwandishi anatuambia kuna nguvu kubwa nne ambazo zimesukuma ukuaji wa china wa kiuchumi.

Nguvu ya kwanza ni ufunguaji wa mipaka na kukubali soko huria. Mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 China ilifungua mipaka yake na kuruhusu soko huria. Kupitia mpango huo, makampuni mbalimbali yaliweza kufungua matawi yake china na mengi yalipeleka kazi zao za uzalishaji china kutokana na unafuu wa gharama za kuzalisha bidhaa zao. hili lilichangia kazi kuwepo nyingi na hata bidhaa kuzalishwa kwa wingi pia.

Nguvu ya pili ni ushindani wa kibiashara. Mwandishi anasema, kabla ya kuruhusu soko huria, kila kitu china kilikuwa kinaendeshwa na serikali. Anatoa mfano kwamba miaka 20 iliyopita, wakati anataka kuweka simu kwenye ofisi zake, ilimchukua zaidi ya miezi sita kuwekewa huduma ya simu. Lakini baada ya ufunguaji wa mipaka na soko kuwa huria, inachukua masaa tu kupata simu. Uwepo wa makampuni na bidhaa nyingi, umefanya ushindani kuwa mkali, ubora kuwa juu na gharama kuwa ndogo.

Nguvu ya tatu ni serikali ya china. Chini ya serikali na chama cha kikomunisti cha china, china imeweza kuwa na soko huria na watu kuwa huru kufanya biashara ndani ya nchi hiyo. Lakini yapo maeneo machache ambayo yameendelea kusimamiwa na kudhibitiwa na serikali. Mfano serikali imedhibiti umiliki wa sekta za fedha, mawasiliano, nishati na vyombo vya habari. Mwandishi anasema soko huria litaendelea kukua zaidi ndani ya china kwa miaka ijayo. Pia uimara wa serikali na utulivu wa nchi umewezesha shughuli za kiuchumi kwenda vizuri.

Nguvu ya nne muunganiko wa china kuwa kitu kimoja. Kabla ya soko huria na ukuaji wa uchumi, china ilikuwa ni nchi ambayo ni kama bara. Kwa sababu maeneo tofauti yalikuwa yakijitegemea, yakiwa na lugha zao, tamaduni zao na kila kitu ambacho kinajitegemea. Lakini baada ya kuingia kwa soko huria, china yote imekuwa kitu kimoja, miundombinu imeboreshwa na mawasiliano kuwa imara zaidi. Hii imewezesha ukubwa wa china kuwa kitu kimoja na kuwa nguvu kubwa.

Ukiangalia nguvu hizi nne, kwa pamoja zinatengeneza mhimili mkubwa sana wa ukuaji wa uchumi.

Je unawezaje kutumia mikakati hii kwa maisha yako binafsi kwa ajili ya mafanikio yako?

Kwanza, hakikisha unakuwa na uhuru, usiwe chini ya utumwa wa aina yoyote ile, na moja ya utumwa wa kuondokana nao ni kutegemea chanzo kimoja cha kipato. Madeni ni utumwa mwingine unaohitaji kuondokana nao. Unahitaji kuwa huru ili kuweza kutumia kila fursa inayokuzunguka.

Pili kuwa na kitu cha kukutofautisha kwenye dunia hii yenye kila aina ya kelele. Ushindani ni mkali sana, chochote unachofanya, wapo wengine wanaofanya, hivyo kama huna cha kukutofautisha, umepotezwa.

Tatu hakikisha una usimamizi na udhibiti mkubwa kwenye chochote unachofanya. Hakikisha unajua nje ndani kila kinachoendelea.

Nne shirikiana na wengine na tengeneza timu ambayo itakuwezesha kufanya yale ambayo wewe binafsi huwezi kufanya. Huwezi kuwa vizuri kwenye kila kitu, hivyo unavyoweza kuwashawishi wengine wakashirikiana na wewe, unanufaika na maarifa, vipaji na hata juhudi zao.

#2 Makala ya wiki hii; BIASHARA 10 UNAZOWEZA KUANZA MWAKA HUU 2018.

Watu wanalalamika mambo ni magumu, fedha hakuna na hawajui wafanye nini. Wiki hii niliandika makala yenye biashara kumi ambazo mtu anaweza kuanza mwaka huu 2018 na akazifanya kwa mafanikio. Siyo biashara mpya, ila nimekupa njia mbadala ya kufikiri na kuona kile ambacho hukioni. Na pia siyo kwamba biashara za kufanya ni hizo kumi tu, bali zipo nyingi, hizi kumi zinakufanya ufikiri zaidi.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma kwa kubonyeza maandishi haya (https://amkamtanzania.com/2018/01/22/biashara-kumi-10-unazoweza-kuanzisha-mwaka-huu-2018-na-ukapata-mafanikio-makubwa/ )

#3 Nilichoona juma hili; ADHA YA AJIRA.

Juma hili nimeona watu wakiwa na taharuki, kwa upande wa walimu kutokana na tangazo la serikali la kuhamisha walimu wa shule za sekondari waliozidi kwenda kufundisha shule za msingi. Mengi yameongelewa kwenye hili, wengine wakisema ni kuwashusha hadhi walimu na itawaathiri kisaikolojia. Wengine wanasema kwa kuwa malipo yao hayatabadilika basi hakuna tatizo, wachape tu kazi.

Mimi nasema hao wote wapo sahihi, wanaosema ni sawa wapo sahihi na wanaosema siyo sawa pia wapo sahihi, wote wana sababu za msingi. Ambaye kwa upande wangu hayupo sahihi, ni yule mwalimu ambaye maamuzi haya yatamfanya afanye kitu ambacho hakipendi. Yaani kwa mfano kama wewe ni mwalimu, na maamuzi haya yametoka, na yamekufikia wewe, kwamba ulikuwa mwalimu wa sekondari na sasa unahamishiwa kufundisha shule ya msingi, na ukafanya maamuzi ambayo huyataki, yaani unalazimika tu kufanya, wewe ndiye haupo sahihi.

Hali kama hii inapokukuta maamuzi unayopaswa kufanya ni ya aina mbili tu;

Moja; kufurahia nafasi hiyo mpya, na kuona ni fursa mpya kwako kwenda kuwasaidia watoto kupata elimu bora, na kwenda kufanya kwa moyo wako wote, bila ya manung’uniko ya aina yoyote ile.

Mbili; kuachana na ajira hiyo ya serikali kwa sababu ndoto yako na malengo yako yalikuwa kuwa mwalimu wa sekondari, na kwa kuwa umelazimishwa kuondoka, basi hutaweza kufuata lazima hiyo na utakuwa na mpango mwingine wa kufanya.

Najua karibu wote waliopo kwenye hali hii hawataweza kufanya maamuzi namba moja, wataenda wakinung’unika na kulalamika, na pia hawawezi kufanya maamuzi namba mbili kwa sababu wameshaingia kwenye mtego wa maisha yao yote kutegemea ajira.

Na hapo ndipo ninaposema anayekosea ni mwalimu. Lakini sasa ana nafasi mpya ya kujipanga, ili maamuzi kama hayo baadaye yasimwathiri tena.

vitabu softcopy

#4 Huduma ninazotoa; NAFASI 2 KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

Mwanzoni mwa mwaka huu nilieleza kwamba, kundi pekee la Mafunzo ninaloendesha kwa njia ya wasap KISIMA CHA MAARIFA limejaa, na sitaweza kufungua kundi jingine. Hivyo nafasi za kujiunga na kundi hili ni mpaka pale zitakapokuwa zinapatikana.

Hivyo nachukua nafasi hii kukutaarifu kwamba zipo nafasi mbili za kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA, kila siku unapata nafasi ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Kuianza siku kwa tafakari bora, kupata makala nzuri za biashara, fedha, uwekezaji na falsafa pia.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA unapaswa kulipa ada ya mwaka ambayo ni tsh 50,000/= na hicho ni kiingilio cha kwanza. Lakini baada ya hapo kuna vitu unapaswa kufanya ili kuendelea kuwa mwanachama. Na vitu hivyo ni kuwa na biashara, uwekezaji, kujifunza kwa kusoma vitabu na kujifunza zaidi kupitia kundi na mimi pia.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, sijui nafasi hizi zitachukua muda gani, lakini unapoona taarifa hii, tuwasiliane mara moja kwa wasap 0717396253 ili uweze kupata nafasi hii.

#5 Neno la kufikirisha;

‘Wise men speak because they have something to say; Fools because they have to say something.’ – Plato

Mwanafalsafa Plato anasema Werevu huongea kwa sababu wana kitu cha kuongea, ila wapumbavu huongea kwa sababu inabidi waseme kitu.

Wakati wowote unapotaka kuongea, jiulize je una kitu cha kuongea au na wewe unataka usikike tu kwamba umeongea? Itakusaidia sana sana sana.

Uwe na wakati mwema rafiki yangu, uwe na juma bora kabisa tunalokwenda kuanza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog