Kila mtu anapenda kufanikiwa, lakini mwisho wa siku ni wachache sana ambao wamekuwa wanafanikiwa kwa uhakika. Wengi wamekuwa wanaishia kutamani kufanikiwa, lakini hawajui kwa hakika ni jinsi gani ya kufikia mafanikio wanayoyataka.

Wapo marafiki wengi kwenye safari ya maisha, marafiki watu, marafiki vitu na marafiki tabia. Chochote kile ambacho unakubaliana nacho na unaenda nacho kwenye maisha yako, ni rafiki yako. Iwe ni mtu, vitu au hali fulani, ukishakubaliana na kitu, kinakuwa rafiki kwako.

Sasa imeshasemwa sana kwamba pale ulipo sasa ni wastani wa wale wanaokuzunguka, hasa wale watu watano wa karibu zaidi kwako. Na leo naongeza pia kwamba pale ulipo ni matokeo ya mazingira yanayokuzunguka na hata tabia ulizonazo.

Kwenye makala ya leo, nakwenda kukushirikisha rafiki mmoja ambaye ukiambatana naye kwa umakini, ninakuhakikishia utafanikiwa sana kwenye maisha yako. Rafiki huyu si mtu bali kitu, lakini ni rafiki anayeweza kukupa chochote unachotaka kwenye maisha yako. Ninaposema kila kitu, namaanisha kila kitu kweli.

Rafiki ninayemzungumzia hapa ni KAZI. Kazi ni rafiki mzuri, rafiki ambaye hana ubaguzi, rafiki ambaye anampenda yeyote anayempenda na kumpa kile ambacho anataka. Rafiki huyu pia huwa habembelezi, kama mtu hamtaki basi na yeye anamkataa na kumtenga na kuhakikisha maisha yake yanakuwa magumu ipasavyo.

work hard

Najua hukutegemea kwamba rafiki niliyekuwa nampamba kiasi hichi anaweza kuwa kazi, kitu ambacho kimekuchosha, kitu ambacho kinakuumiza kichwa kila siku ya jumatatu asubuhi, na ikifika ijumaa mchana unajisikia vizuri kwa sababu una siku mbili ambazo siyo za kazi, au hata kama ni za kazi, basi siyo kazi ngumu,

Lakini mimi nakuambia, rafiki yako namba moja kwenye maisha anapaswa kuwa kazi. Asikuambie yeyote chochote dhidi ya kazi, wewe penda kazi, weka muda wako kwenye kazi, weka juhudi za kutosha, na rafiki huyu hatakutupa, atakulipa ipasavyo.

Sasa najua yapo mengi ya kukukatisha tamaa kwenye kazi, yapo maneno mengi yanayokufanya uone kazi ni utumwa na inapaswa kukimbiwa.

Hapa nakupa mambo kumi kuhusu kazi, ambayo kwa kuyasimamia na kuyaishi, utakuwa na urafiki mzuri na kazi na utafanikiwa zaidi kwenye maisha yako.

  1. Ipende kazi.

Kazi yoyote unayoifanya, ipende, ipende sana. Hata kama kazi unayofanya siyo ya ndoto yako, hata kama umeajiriwa na unalipwa kidogo, hata kama unaowafanyia kazi hawakujali, huna sababu ya kutokuipenda kazi. Kumbuka mtu wa kwanza unayemfanyia kazi ni wewe, na urafiki wa kazi unaangalia wewe mfanyaji na siyo unayemfanyia.

Ipende kazi yako, ipende sana, ifanye kwa hamasa na jitoe kuifanya kwa viwango vya ziada, sahau mengine yote na penda ile kazi unayoifanya, hutabaki pale ulipo.

  1. Kuwa wa kwanza kufika na wa mwisho kuondoka.

Kazi yoyote unayofanya, iwe ni kazi yako binafsi au umeajiriwa, ishi msingi huu mmoja, kuwa wa kwanza kufika eneo lako la kazi, na kuwa wa mwisho kuondoka. Hata kama ukifika hakuna kazi kubwa ya kufanya, kwamba lazima uwasubirie wengine wafike, wewe kuwa wa kwanza kufika, na kuwa wa mwisho kuondoka.

Dhana hiyo itakupa majukumu mengi zaidi na pia itakutofautisha na wengine wote. Hata wale wanaohitaji mtu wa kuwasaidia, wataangalia nani anayepatikana zaidi ya wengine, na wewe utakuwa namba moja. Usiwe kama wengi, wanaochelewa kufika na kuwahi kuondoka, wewe nenda kinyume na itakulipa.

SOMA; Usikubali Mtu Yeyote Akushinde Kwenye Maeneo Haya Kumi(10) Muhimu Kwa Mafanikio Ya Maisha Yako.

  1. Unapofanya kazi fanya kazi.

Una muda mfupi wa kufanya kazi kwenye siku, maana masaa yenyewe ni machache, halafu tena unapoteza muda huo kufanya mambo yasiyo ya msingi. Rafiki, unapofanya kazi, fanya kazi, akili na mawazo yako yote yanapaswa kuwa kwenye kazi unayofanya.

Usiruhusu muda wako wa kazi, hata dakika moja iende kwenye mambo yasiyo muhimu kama majungu, mitandao ya kijamii na kufuatilia habari. Usijenge utamaduni wa kupokea simu na kuwasiliana na watu unapokuwa kwenye kazi. Heshimu muda wa kazi, na kazi itaheshimu muda wako kwa kuhakikisha unalipwa vizuri.

  1. Fanya kazi mara mbili ya muda ambao wengine wanafanya kazi.

Watu wa kawaida huwa wanafanya kazi kwa wastani masaa nane kwa siku, siku tano au sita kwa wiki na hivyo kwa kiwango cha juu kabisa, wanafanya kazi masaa 50 tu kwa wiki. Lakini wiki ina masaa 168, sasa sijui hayo masaa mengine zaidi ya 100 wanayapeleka wapi.

Sasa wewe ambaye ni rafiki wa kazi, fanya kazi mara mbili zaidi ya wanavyofanya wengine. Hakikisha kila wiki unafanya kazi masaa yasiyopungua 100. Ndiyo, chini ya masaa 100 hujui unachofanya, huna urafiki na kazi na unajiumiza wewe mwenyewe, kwa kuwa katikati ya kundi la wanaofanya kwa ukawaida.

Fanya kazi mara mbili ya watu wa kawaida, na utapata matokeo mara mbili ya wanayopata watu wa kawaida. Fanya kazi angalau masaa 15 mpaka 16 kwa siku, na siku zote saba za wiki.

  1. Wanaokuambia unafanya kazi sana hawafanyi kazi.

Wapo watu watakaokuambia unafanya kazi sana, unajitesa, unahitaji kupumzika na maneno mengine kama hayo. Wewe usiwajibu chochote, bali angalia ufanyaji wao wa kazi, angalia mafanikio yao, halafu angalia ufanyaji kazi wa wale waliofanikiwa, utakachoona kitakushangaza. Wale ambao hawafanyi kazi na hawajafanikiwa, ndiyo vinara wa kusema wengine wanafanya kazi sana.

Wanaokusema unafanya kazi sana, wana wivu, wangependa kufanya kazi ila hawawezi, hivyo wanawasema wale wanaofanya kile wasichoweza kufanya.

SOMA; Biashara Kumi (10) Unazoweza Kuanzisha Mwaka Huu 2018 Na Ukapata Mafanikio Makubwa.

  1. Usiseme siyo jukumu langu au siwezi kufanya.

Kama umeajiriwa, basi kuna maneno ambayo huruhusiwi kabisa kumwambia mwajiri au bosi wako. Pale unapopewa jukumu lolote kwenye kazi, iwe linaendana na wewe au la, iwe unaweza au la, kamwe usiseme siyo jukumu langu au siwezi kufanya. Badala yake sema nitafanya, halafu jifunze namna gani ya kufanya. Au sema unahitaji maelekezo jinsi ya kufanya kwa ubora na utaelekezwa.

Kama umejiajiri au unafanya biashara, kamwe usimwambie mteja huwezi kufanya kile anachotaka, bali mwambie unaweza kufanya kisha jifunze namna ya kufanya. Iwe tu inaendana na kile unachofanya.

Ukienda kwa mtazamo huu, utajifunza mengi na utapewa nafasi kubwa zaidi na zaidi.

  1. Kila siku ni siku ya kazi.

Kuna wale wanaosema jumatatu ni siku mbaya kwa sababu ni mwanzo wa siki ya kazi,na ijumaa ni siku nzuri kwa sababu ni mwanzo wa mapumziko. Wengine wanaangalia sikukuu ni lini ili wapumzike. Hivi ndivyo wanavyofikiria wale ambao wameshindwa.

Wewe kila siku kwako ni siku ya kazi. Hupaswi kujua hata ni siku gani, wewe jua ni siku ya kazi. Iwe ni jumatatu, ijumaa au jumapili, kama jua limechomoza basi ni siku ya kazi. Na kila siku amka na hamasa ya kazi bila ya kujali ni siku gani.

  1. Usilalamike kwamba una kazi nyingi.

Sijawahi kuelewa pale unapokuta mtu analalamika ana kazi nyingi, au majukumu yake ni mengi. Hivi unajua kuna ambao hawana kazi kabisa, na hawajui hata wapateje kazi?

Unapokuwa na kazi nyingi, unapokuwa na majukumu yanayokuzidi, shukuru, shukuru kwa sababu ni kiashiria kwamba watu wanakuamini, watu wanaona thamani yako na usiwaangushe, tekeleza majukumu yako vizuri.

  1. Usijidanganye kwamba unamfanyia mtu kazi.

Mtazamo ambao umekuwa unawapoteza waajiriwa wengi ni kuona kwamba wanamfanyia mtu mwingine kazi. Ni kweli kwamba kazi kubwa unayofanya anayefaidi matunda yake ni mtu mwingine, lakini ile kazi unajifanyia wewe mwenyewe. Hivi unafikiri unapokaa kwenye kazi moja kwa miaka kumi, ni nani anayenufaika au kuumia? Ni wewe.

Kama utaitumia miaka hiyo kumi kufanya kazi bora, utajijengea thamani kubwa ambayo haipatikani popote. Kama utatumia miaka hiyo kumi kufanya kawaida, kwa sababu siyo kazi yako, utaishia kuwa kawaida na hakuna atakayeona thamani yako.

SOMA; Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Cryptocurrency Na Bitcoin (Fedha Za Kidijitali) Na Kwa Nini Siyo Uwekezaji Mzuri Kwako Kwa Sasa.

  1. Kufia kazini ni ushujaa.

Japani ni taifa ambalo limeweza kupata mafanikio makubwa sana licha ya kutokea chini kabisa kwa sababu watu wamejengewa msingi mkubwa sana kwenye kazi. Kwa Japani, kufia kazini ni ushujaa. Hivyo watu wapo tayari kufanya kazi usiku na mchana, na wanajua ukifia kwenye kazi ni ushujaa. Na zipo ripoti za wengi kufia kazini, wengine kufa kwa sababu ua uchovu wa kazi na pia wengine kupata magonjwa ya akili kama sonona kwa sababu ya kazi.

Najua utakuwa unajiambia kwa nini nifie kazini, kwa nini kazi iniue? Sikia rafiki, kuna kitu kitakuua kwenye haya maisha, huo ni uhakika. Landa ngono itakuua, kwa kufanya ngono hovyo ukapata magonjwa ya zinaa na UKIMWI kisha ukafa, au ajali itakuua, au pombe itakuua, au ujinga utakuua. Kuna kitu ambacho kitachangia kwenye kifo chako, sasa kwa nini usichague kazi, ambayo itakuja na manufaa makubwa kabla hata hujafa?

Fanya kazi rafiki, fanya kazi. Tenga muda wako wa siku kwenye majukumu matatu tu, kazi, kupumzika na kuwa na wale wa karibu kwako. Na katika kupumzika hapo weka jukumu la kuimarisha afya yako ya mwili, akili na roho. Zaidi ya hapo, weka kazi, kazi ni rafiki ambaye hatakutupa kamwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

vitabu softcopy