Ramani ya nyumba ni dira muhimu sana kwa wahandisi na wanasayansi wa ujenzi duniani kote. Ni nguzo na ngao za maamuzi na utekelezaji katika kufikia lengo kabla na wakati wa ujenzi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kutokea duniani kote ikiwemo Tanzania yamechangia kwa kiasi kikubwa mapinduzi ya uhandisi ujenzi wa nyumba za kisasa. Lengo kuu la wahandisi na wanasayansi wa ujenzi ni kuifanya dunia kuwa mahali safi na salama kwa viumbe vyote akiwemo mwanadamu. Ingawa wahandisi ujenzi wanahusika na majengo na miundombinu kama vile barabara, reli, madaraja, viwanda, viwanja vya michezo, viwanja vya ndege, minara na mengine mengi lakini leo nitazungumzia sifa pekee za nyumba bora na za kisasa kutokana na kuwepo na mkanganyiko wa kimtazamo miongoni mwetu. Nyumba bora na ya kisasa ni nyumba ambayo inakidhi mahitaji yote ya watumiaji pasipokuleta kadhia ya aina yoyote na kuwa sehemu salama na yenye hamasa kwa mtumiaji au wakazi husika. Zifuatazo ni sifa kadhaa zinazopaswa kuzingatiwa kwenye ramani pale unapokutana na wataalamu wa ramani za majengo.


  1. LAZIMA IWE RAFIKI WA MAZINGIRA

Ramani bora ya nyumba ni rafiki wa mazingira, ni ramani ambayo lazima ikidhi viwango kuendana na mazingira ya nyumba itakapojengwa. Msanifu na mbunifu majengo huzingatia sana usalama wa makazi jirani, aina za udongo, milima, mabonde, miundombinu na zaidi hufikiria kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujenzi unapofanyika na baada ya ujenzi kukamilika. Yamkini unaweza kuwa umeipenda ramani ya aina fulani lakini ikawa si rafiki wa mazingira halisi ya kiwanja chako. Ni vema ukapata ushauri wa kimazingira kutoka kwa mtaalamu wa ujenzi, kutofanya hivyo kutakusababishia gharama za marekebisho kwa siku zijazo.

  1. LAZIMA IWE NA UWEZO WA KUPAMBANA NA HALI YA HEWA

Wataalamu wa ujenzi huzingatia sana taarifa za mamlaka ya hali ya hewa katika kuandaa mpango kazi wa kuhakikisha wanafikia viwango husika vya ubora wa nyumba mahali itakapojengwa. Mabadiliko ya hali ya hewa na viwango fulani kuhusu mvua, joto, baridi, mwelekeo wa pepo na matetemeko ya ardhi ni mambo muhimu sana yanayozingatiwa wakati wa ubunifu na uchoraji wa ramani za nyumba. Nyumba bora lazima iwe na uwezo wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ili iweze kuhimili kwa muda mrefu na kuwa sehemu salama yenye usawazo wa mwili na akili za wakazi na wageni husika. Ni muhimu sana ukamshirikisha mtaalamu wa ujenzi ili akupe msaada zaidi ili ramani ya nyumba yako iwe nzuri na yenye uwezo wa kumudu changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

  1. LAZIMA IWE NA MUONEKANO WA KUVUTIA

Kama ilivyo kwenye utofauti wa kimtazamo kwenye mambo mengine, hata mwonekano wa nyumba huwa na mtazamo tofauti kulingana na haiba ya mtu mmoja na mwingine. 

Mwonekano wa nyumba hutegemea sana mtazamo wa mteja na mbunifu wa ramani za nyumba ili kuendana na mazingira itakapojengwa. Hivyo uzuri na mvuto wa nyumba ni utashi wa mtu mwenyewe anapenda nini. Nyumba bora ni lazima iwe na uwezo wa kuvutia na ikushawishi wewe na wengine kuendelea kuitazama na ikutie hamasa zaidi ili uendelee kuishi kwenye nyumba hiyo. Kuifanya nyumba iwe na mwonekano mzuri kunahitaji fikra na mtazamo wa wahusika kufikisha mawazo kwa mtaalamu wa mambo ya urembo wa nyumba kwa hali ya umakini sana, naamini utapata ushauri mzuri na kuipenda nyumba yako milele yote.

  1. LAZIMA IZINGATIE GHARAMA YA MTEJA

Ramani nzuri ni ile ambayo inazingatia hali ya uchumi wa muhusika, ramani bora ni lazima izingatie gharama za ujenzi dhidi ya uwezo wa muhusika. Unapofikiria kuwa na nyumba ya aina fulani ni vema ukajitathmini na kumshirikisha mtaalamu wa ujenzi kuhusu uwezo wako wa kifedha kwenye ujenzi wako, kwa kufanya hivyo utamuwezesha akupatie ramani unayoitaka na inayoendana na uwezo wako kifedha. Watanzania wengi hupata hofu ya kujenga nyumba bora kwa kuhofia gharama. Lakini napenda nikueleze kwamba uzuri wa nyumba ni ubunifu ambao unafanywa na mtaalamu wa ujenzi ili kuonesha ubora na ufanisi wake wa kitaalamu dhidi ya wengine, hivyo usikutishe ukahisi itakuwa ni gharama kubwa sana, hata wewe unapaswa uwe na ramani ya nyumba.

  1. LAZIMA IZINGATIE TAMADUNI ZA MAHALI HUSIKA

Tanzania ni miongoni mwa nchi yenye watu wenye tamaduni tofauti. Utofauti wa tamaduni husababisha kuwa na utofauti wa mitindo ya maisha kwenye jamii. Kwenye fani ya uhandisi mila na desturi huzingatiwa sana, utofauti wa utamaduni huzingatiwa ili kuhakikisha ramani inakidhi ubora unaoendana na mfumo wa maisha yako na kwenye jamii ambayo nyumba yako itajengwa. Yamkini umeipenda ramani kutoka nchi au jamii fulani na ukapenda ujenge kama hiyo ni vema ukamuona mtaalamu wa ujenzi, naamini atakushauri vizuri ili ramani yako iendane na tamaduni na mazingira halisi ya ukanda wetu. Wengi tunachukua ramani kwenye mitandao pasipokufikiria tofauti zetu za kimazingira na mfumo wa maisha, hali ambayo itakufanya uboreke kwa muda mfupi sana endapo utakutana na kasoro kadhaa.

  1. LAZIMA IZINGATIE MATUMIZI HUSIKA

Ramani ya nyumba bora ni lazima izingatie ufanisi wa matumizi halisi ya wakazi, mtaalamu wa ujenzi huzingatia sana uwezo na haiba za wakazi kwenye nyumba itakayojengwa. Makundi maalumu kwenye jamii kama vile wazee, watoto, wajawazito, walemavu na wagonjwa hupewa kipaumbele zaidi kuwafanya waweze kuishi katika hali ya furaha na usalama wa mwili na afya. Ramani ya nyumba bora ni ile ambayo inakidhi matumizi na mahitaji halisi ya wakazi hasa yale yenye ulazima. Mfano choo cha kukaa huwa msaada sana kwa wagonjwa, walemavu na wajawazito lakini idadi ya watumiaji huzingatiwa sana tofauti na choo cha kuchutama.

  1. LAZIMA IZINGATIE TEKNOLOJIA ILIYOPO


Maendeleo ya sayansi na teknolojia kwenye taaluma ya ujenzi imechochea sana ubunifu na ushindani wa hali ya juu kwa wataalamu wa ujenzi duniani kote. Hivi sasa wabunifu na wasanifu majengo wana uwezo mkubwa sana wa kubuni na kusanifu nyumba katika mfumo na mwonekano wa aina yoyote. Wataalamu wa sasa wana uwezo wa kubuni na kusanifu ramani za majengo yenye ukubwa na maumbo yoyote, changamoto kubwa ni kutoweza kujengeka kutokana na kutokuwepo kwa mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kuendana na majengo marefu duniani kutokana na hali ya uchumi tuliyonayo. Maendeleo ya ardhi na majengo hutegemea sana hali na mwenendo wa uchumi wa nchi husika. 

Ramani bora ya nyumba lazima izingatie uwezekano wa kujengwa kwa teknolojia zilizopo, na muhimu zaidi ni uwezekano mkubwa wa upatikanaji wa malighafi zitakazo tumika kujengea nyumba hiyo.

  1. LAZIMA IZINGATIE SHERIA NA TARATIBU ZA MAMLAKA HUSIKA

Ubunifu na usanifu wa majengo ya kisasa unazingatia sana sheria, sera na taratibu zote za kitaaluma na mamlaka zinazohusika na uratibu wa ardhi na majengo. Ramani bora za nyumba zinapaswa kuwa safi na zinazokidhi mahitaji yote ya muhusika na sheria zote za mamlaka ili kuifanya nyumba itakayojengwa kuwa mahali salama kwa wakazi. 

Kutozingatia sheria ni kuongeza gharama kutokana na adhabu au kuihatarisha nyumba yako dhidi ya kuangamizwa endapo itagundulika kuwa haipo sehemu salama au imeleta athari hasi kwenye mazingira ilipojengwa.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888


Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com