Men exist for the sake of one another. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Hii ni siku ambayo kama tukiweka juhudi kubwa, basi tutaweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa mafanikio mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kupiga hatua kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari; UWEPO WAKO NI KWA AJILI YA WENGINE…
Ni kawaida kwetu sisi binadamu kujifikiria wenyewe, kujijali kwanza kabla ya wengine. Kwenye kila jambo kuangalia tunanufaikaje.
Lakini hebu jiulize kama ungekuwa peke yako kwenye hii dunia, hata kama unapata kila unachotaka, maisha yako yangekuwa na maana gani?

Ukijiuliza swali hilo ndiyo unaona umuhimu wa watu wengine. Na kwamba hao wengine ndiyo wanayafanya maisha yetu kuwa na maana. Yale tunayofanya kwa ajili ya wengine, ndiyo yanafanya maisha yetu kuwa bora sana na kuwa na maana.

Hivyo rafiki, kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, jiulize ni kwa namna gani kinawanufaisha wengine. Angalia ni jinsi gani kinafanya maisha ya wengine kuwa bora kabisa.

Kama kila wakati umekuwa unajifikiria wewe tu, kama kila wakati unataka kushinda wewe tu hata kama wengine wanaumia, jua ushindi wako hautakuwa na maana.
Kwa sababu uwepo wako ni kwa ajili ya wengine, hivyo ushindi wa kweli kwako ni ushindi wa wengine.

Wawezeshe watu kushinda zaidi na utakuwa na maisha bora sana na yenye mafanikio makubwa.
Uwe na siku bora sana leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha