Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu.
Leo tumepata nafasi bora na ya kipekee sana kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tuna kila fursa ya kupiga hatua zaidi.

Asubuhi ya leo tutafakari UTAMJUA RUBANI KWENYE DHORUBA…
Pale mambo yanapokuwa shwari, kila mtu anaweza kuwa shujaa.
Pale mambo yanapokwenda kama yanavyotegemewa kwenda, kila mtu anaweza kufanya kile ambacho anategemewa kufanya.
Pale mambo yanapokuwa kama yalivyozoeleka kuwa, kila kitu kinakwenda kwa sheria zinazojulikana na kila mtu anaweza kufuata sheria hizo na akapata matokeo mazuri.

Changamoto na matatizo huanza pale mambo yanapokwenda tofauti na yalivyotegemewa kwenda.
Pale ambapo umeshafanya unachopaswa kufanya, lakini matokeo yanakuwa tofauti na ulivyotegemea.
Pale ambapo kila kitu kinakwenda tofauti na kilivyotegemewa kwenda.
Pale ambapo hata kufuata sheria na taratibu za kufanya kitu, hakuleti matokeo ambayo mtu ulitegemea kupata.

Hapa sasa ndipo tunapowajua wale kweli waliojitoa kupata kile walichotaka.
Hapa ndipo tunapojua wazi kwamba nani walijiandaa vyema kuhakikisha kwamba wanakabiliana na kila hali kupata kile wanachotaka.
Hapa ndipo tunapojua wale ambao hawawezi kurudishwa nyuma na chochote.
Na hapa ndipo tunapowajua washindi wa kweli, wale ambao wanafanikiwa kufanya makubwa.

Dhoruba kali ndiyo inatengeneza marubani wazuri, mawimbi makali ndiyo yanatengeneza manahodha wazuri, na changamoto kubwa ndiyo zinatengeneza watu bora.

Unaweza kusema na kudai chochote unachoweza, na unaweza kutimiza hilo wakati mambo yanakwenda kawaida. Lakini ni wakati wa changamoto na matatizo, wakati wa misukosuko na shida ndipo tunapoweza kujua kama kweli upo tayari kwa makubwa.

Hivyo rafiki, usiombee maisha ambayo hayana changamoto au matatizo, badala yake kuwa tayari kukabiliana na kila tatizo au changamoto. Na hayo yatakufanya kuwa bora, hayo yataionesha dunia kwamba wewe ni imara, umekomaa na unaweza kupita kila hali.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha