Kuna kutawaliwa kwa nguvu, halafu kuna kutawaliwa kwa hisia. Kutawaliwa kwa nguvu au mabavu kunaweza kuumiza, lakini kunafanyika na mtu mwingine, hivyo angalau unaweza kuwa na mtu wa kumlaumu na hata kupambana kupata uhuru wako.
Lakini kutawaliwa kwa hisia, kunaumiza zaidi, ila ubaya ni kwamba, unakuwa umejiweka wewe mwenyewe kwenye hali ya kutawaliwa. Mwingine anaweza asijue hata kama anakutawala, ila kwa hisia zako wewe, ukawa umejiweka chini ya utawala wa mtu mwingine.
Mfano wa hisia ambazo zinasababisha watu watoe nafasi ya kutawaliwa na wengine ni hisia hasi kama hasira, chuki, vinyongo na hata wivu. Unapokuwa unamfikiria mwingine katika hali hasi, labda unamchukia, au una hasira naye, au una kinyongo naye, unakuwa umempa nafasi ya kukutawala wewe.

Hii ni kwa sababu, kila wakati unapomwona mtu huyo, lazima ujikumbushe kile ambacho unafikiria kwa uhasi kuhusu yeye. Lazima ujikumbushe kwamba unamchukia, na kwa nini unamchukia. Lazima ukumbuke kile alichokufanyia ili ujidhihirishie kwamba anastahili kinyongo chako. Yote haya ni kujitafutia kutawaliwa na wengine.
Wakati mwingine inabidi ujikumbushe haya yote hata kama mtu huyo hayupo karibu. Hapa ndipo unapotoa nafasi ya utawala wa watu kwako hata kama wapo mbali. Mtu anaweza kuwa yupo na maisha yake, ana furaha kwa kile anafanya, na wewe upo mbali kabisa lakini unajikumbusha namna unavyomchukia, au namna alivyokukosea na hivyo huwezi kumsamehe kamwe.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kwa Nini Hisia Bado Zinatushinda Kudhibiti Na Namna Ya Kuzidhibiti.
Muda wowote ambao mtu utatumia kwa hisia hasi kwa wengine, iwe ni chuki, hasira, kinyongo na hata wivu, ni muda ambao unakuwa umechagua kuupoteza kwa mtu ambaye hata hastahili. Unakuwa umechagua kuwa chini ya utawala wa mtu ambaye hata hajui kama amekutawala.
Hatua muhimu sana ya kuhakikisha maisha yako yanakuwa huru, ni kuhakikisha katika wakati wowote wa maisha yako, huna hisia zozote hasi juu ya watu wengine. Hata kama mtu amefanya mabaya na kukukosea kiasi gani, hata kama amekuumiza na haoneshi kujali, kuwa na hisia hasi juu yake kunakuumiza zaidi wewe kuliko yeye.
Hivyo hebu jitendee haki, hebu jipe uhuru, hebu achana na kila aina ya hisia hasi inayoweza kuwa ndani yako na uweze kuwa na maisha huru.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog