To be able to endure odium is the first art to be learned by those who aspire to power – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nzuri na ya kipekee ketu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kuuishi leo ili kuweza kufanya makubwa.
Mwaka huu 2018 tunaongoza kwa TATUA, AMUA NA ONGOZA, ambapo tutaweza kupiga hatua kubwa kila siku kuelekea kwenye mafanikio.

Asubuhi ya leo tutafakari KUBALI CHUKI KAMA UNATAKA MAFANIKIO…
Wakati wewe unakazana kuweka juhudi kwenye kazi na biashara zao ili ufanikiwe, siyo kila mtu atakuwa anafurahia juhudi unazoweka, hata kama hazihusiani naye kwa namna yoyote ile.
Wapo watu watakaochagua kukuchukia tu, kwa sababu ya juhudi kubwa unazoweka, kwa sababu ya namna unavyopambana ili maisha yako yawe bora.

Na wapo ambao wataonesha waziwazi, wakikupinga na kukuambia utasindwa au haiwezekani na hata kukuwekea vipingamizi vya aina fulani.
Na wapo wengine ambao hawataonesha wazi wazi, wao wataweka vipingamizi vya chini chini, au watakusifia sana ili wakusukume kwenye kuanguka, na pia wanaweza kuonekana wapo kimya, lakini unapokutana na changamoto wanasema tulijua tu, asingeweza kufika mbali.

Unapokutana na watu wa aina hii, kwa hakika utakutana nao, kama bado ni swala la muda tu, jua hakuna chochote unachoweza kufanya kuwabadili. Hivyo usifikiri kuna namna unaweza kuwaridhisha au kuwafanya wakupende.
Badala yake waache wawe vile wanavyotaka kuwa.
Wewe unachotaka ni mafanikio, na unapotimua vumbi zako za mafanikio, kuna wengi ambao utawavuruga.

Utawavuruga wale ambao wamezoea kufanya kawaida na kupata matokeo ya kawaida. Sasa wewe unaweka juhudi zaidi na kupata matokeo bora, maana yake wao wataonekana ni wazembe.
Utawavuruga wale wanaoamini kwamba vitu fulani haviwezi kufanyika kamwe, wewe unapoweza kuvifanya unavuruga kabisa imani zao.

Unachopaswa kujua ni kwamba, huwezi kuwapangi watu wakupende au wakuchukue, hicho ni kitu ambcho kipo nje ya uwezo wako.
Kilichopo ndani ya uwezo wao ni kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana. Na hilo litawavuruga watu, na baadhi watakuchukia, lakini huna cha kuwafanya, hivyo waache wachukie na hilo lisikusumbue kwa namna yoyote ile.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha