Accept the things to which fate binds you, and love the people with whom fate brings you together, but do so with all your heart. – Marcus Aurelius

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nzuri ya leo, nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata mtokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwaka huu 2018 tunaongozwa na TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kufanya makubwa na kupiga hatua kubwa.

Asubuhi hii tutafakari KUBALI NA PENDA..
Asili huwa inatuweka kwenye mazingira ambayo siyo tunayoyategemea, na kutuweka na watu ambao hatuwajui na wala hawaendani na sisi.
Hili ni jambo ambalo wengi huwezi kulilalamikia na hata kuona haiwafai na kufikiria njia za kuondoka kwenye hali hizo.
Lakini njia zozote wanazotumia zinashindwa.

Njia pekee ambayo mtu anaweza kutumia na akashinda ni KUKUBALI NA KUPENDA..
KUBALI ile hali ambayo asili imekuweka, ukijua kwamba pale ndipo ulipo sasa. Hivyo kama unataka kutoka pale, utaanzia hapo na siyo pengine.
Hivyo lazima upakubali, lazima upatumie kama ngazi ya kupiga hatua zaidi.
Huwezi kutumia kitu ambacho hukikubali, na kama huwezi kupatumia vizuri pale ulipo, basi hutaweza kuondoka hapo na kupiga hatua.

PENDA wale watu ambao asili imekuletea au kukuweka nao. Hata kama ni watu ambao huwajui, au hawaendani na wewe, kwa kuwa mmeshajikuta pamoja, basi ni jukumu lako kuwapenda.
Hii itakusaidia sana kuweza kufanya mambo yako vizuri, kupata ushirikiano wa wengine na hata kuweza kupiga hatua zaidi.
Unapowapenda wale unaokuwa nao, unatengeneza nafasi ya wewe kuweza kupiga hatua zaidi.

Kwa mfano kama umepata ajira ambayo huipendi sana, kwenye eneo ambalo hukuwahi kulifikiria na ukakutana na wafanyakazi wenzako ambao hawaendani kabisa na wewe. Wanachofanya wengi ni kuchukia ajira hiyo na kutowakubali wafanyakazi wenzao. Hili linafanya kazi zao kuwa ngumu na kujikuta hawawezi kupiga hatua.
Lakini kama mtu ataikubali kazi ile kwa muda, akayakubali mazingira yale kwa muda atakaokuwa pale, na kuwapenda wafanyakazi wenzake kwa kipindi hicho, kazi itakuwa rahisi na fursa za kupiga hatua zaidi zitakuwa nyingi.

Kubali hali ambayo asili imekuweka na wapende wale ambao unakutana nao. Hii ni njia bora ya wewe kufanya kwa ubora na kuweza kupiga hatua zaidi.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha