Ili dawa ifanye kazi, inahitaji kuwa na sifa mbili.

Sifa ya kwanza lazima dawa iume au iwe chungu.

Na sifa ya pili lazima iwe ngumu kupatikana.

Hivi ndivyo jamii yetu ilivyotengenezwa tangu enzi na enzi, hata kabla ya kuja kwa dawa za kisasa. Dawa za mizizi zilikuwa zikitafutwa mbali kabisa porini, na zilikuwa chungu sana.

Na hata baada ya kuja kwa dawa za kisasa, imani hiyo imeendelea. Wapo wanaoamini kwamba kama hawajachomwa sindano basi hawajapata dawa ya uhakika.

Kwa bahati mbaya sana, hilo haliishii kwenye dawa pekee, bali linakwenda kwenye kila eneo la maisha yetu, na hasa kwenye mafanikio na fedha.

wp-image--1475273682

Ili mafanikio yawe ya kweli na tunayoyajali, lazima yawe magumu kwetu na yapatikane kwa shida.

Hii ndiyo sababu watu wanaopata fedha kiurahisi, bila ya kuweka kazi sana na kuumia, huwa wanapoteza fedha hizo bila kufanya la maana. Lakini wale ambao wamepata fedha zao kwa uchungu, kwa kuumia na kwa kuteseka, wanazijali na kuzitumia vizuri.

SOMA; Hizi Ni Sababu Kwa Nini Baadhi Ya Watu Wanaopata Fedha Nyingi Huishia Kufa Masikini, Na Hatua Za Wewe Kuchukua.

Sasa hayo yote unayajua, lakini je unawezaje kuyatumia?

Mambo mawili hapa;

Moja; chochote unachopata, iwe ni kwa urahisi au ugumu, kithamini. Ifundishe akili yako kuthamini kila unachopata. Unapookota fedha, jua ile ni fedha, elfu kumi ya kuokota na elfu kumi ya kulipwa baada ya kazi ya mateso ni elfu kumi ile ile. Usikubali akili yako ikudanganye kwamba uliyookota haina maana sana kwako na hivyo kuitumia hovyo.

Mbili; chochote unachotaka wengine wakithamini, fanya kiwe kigumu kupatikana, watu waweke juhudi kukipata na watakithamini sana. Lakini kama kinapatikana kwa urahisi, wengi watakichukulia ni cha kawaida.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog