Mimi siyo muumini wa mashindano, huwa ninaamini kwamba kushindana na mtu moja kwa moja ni kupoteza muda na kujiwekea ukomo. Hii ni kwa sababu unaposhindana, unaishia kwenye kiwango cha yule unayeshindana naye, huwezi kwenda mbali zaidi.
 
Hivyo ambacho nimekuwa naamini sana ni kuwa bora zaidi kila siku na hatimaye kuwa bora zaidi kuliko wote. Na hichi ni kitu ambacho kinawezekana kwa kila mtu kwa sababu kila mtu yupo tofauti hapa duniani. Unapokazana kuwa bora kila siku, una nafasi ya kuwa juu zaidi na asiwepo yeyote wa kukuzidi.
 
Lakini ukikazana kushindana na wengine, unachoishia ni kuwa kama wao, na hapo unakuwa umezika uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yako.
 
Lakini pia ninaamini vipo vitu vingi ambavyo watu wamekushinda na huna namna ya kuwafikia. Kuna watu ambao wamekushinda kiasi cha fedha ulichonacho, wao wanacho mara dufu. Wapo pia waliokushinda akili, wamezaliwa na uwezo mkubwa wa kuelewa kuliko wewe. Wapo pia waliokushinda kwa urembo na utanashati. Lakini yote haya hayana maana kubwa kama mambo kumi ninayokwenda kukushirikisha hapa.
 
Yapo maeneo kumi muhimu ya maisha yako, ambayo hapaswi mtu yeyote kukushinda, hasa kwa kile unachofanya na kwa eneo ulilopo. Haya ni maeneo kumi ambayo ukiyawekea juhudi kila siku, lazima utakuwa na maisha bora sana.
 
Karibu tujifunze maeneo haya kumi na jinsi ya kuwa bora kwenye maeneo haya zaidi ya wengine wote.
 
1. Kazi.
 
Asiwepo mtu yeyote ambaye anafanya kazi kukuzidi wewe. Hakikisha unafanya kazi kuliko wengine wote, weka juhudi kubwa kwenye kazi zako, iwe ni kwenye ajira, kujiajiri au biashara. Hakikisha watu wanapotaka kitu fulani kikamilike basi wanakuja kwako. Na hili linawezekana kama utaweka muda na umakini kwenye kila unachofanya, na kama utaacha kutafuta njia za mkato au sababu za kufunika uvivu wako.
 
2. Kujifunza.
 
Kama kuna mtu yeyote anayejua kuliko wewe tayari umeshampa nafasi ya kupiga hatua kuliko wewe. Hakikisha wewe ndiye unayejua kila kinachohusiana na unachofanya, kuliko mtu mwingine yeyote anayefanya kile anachofanya. Hakikisha una maarifa na taarifa nyingi na sahihi kwenye hilo unalofanya, kiasi kwamba unaweza kufanya maamuzi ya haraka na sahihi pale unapokuwa njia panda.
 
Hakikisha unasoma vitabu vingi zaidi kuhusiana na unachofanya na pia unashiriki kwenye mafunzo mbalimbali yatakayokufanya ujue zaidi kile unachofanya.
 
Nasisitiza, hakikisha unajua zaidi ya wengine wote, na hilo ni rahisi kama kila siku utakuwa tayari kujifunza.
vitabu softcopy
 
3. Kuchukua hatua.
 
Kama kuna mtu anachukua hatua kubwa kuliko unazochukua wewe, mtu huyo yupo mbele yako mbali sana, kwa sababu kwa hatua kubwa anazochukua, anajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa kuliko wewe. Hakikisha wewe unakuwa ndiye mtu unayechukua hatua kubwa kuliko wengine wote.
 
Ndiyo kwa kuchukua hatua kubwa kuna hatari ya wewe kushindwa, lakini pia inakuweka kwenye nafasi ya kushinda kwa kiasi kikubwa. Kuwa mtu wa kuchukua hatua kubwa ili kutengeneza mazingira ya kuweza kushinda kwa kiasi kikubwa pia.
 
4. Kutoa thamani.
 
Kuwa na mikono ya maajabu, mikono ambayo ikigusa jiwe linageuka kuwwa dhahabu. Hapa namaanisha kwamba, chochote unachofanya, toa thamani kubwa sana, thamani ambayo haiwezi kupatikana sehemu nyingine yoyote ila kwako tu. Hakikisha kwa kazi au biashara unayofanya, wewe ndiye unayetoa thamani kubwa sana, kiasi kwamba yule anayelipia, anaona kama anakuibia, anaona kama ameokota kitu.
 
Chochote unachotoa, iwe ni kwa thamani kubwa sana, hii itakusimamisha na kukutofautisha na wengine wote wanaofanya kama unavyofanya wewe.
 
5. Mapenzi.
 
Kama kuna mtu anapenda anachofanya kuliko wewe unavyokipenda, umeshapotezwa tayari. Kama kuna mtu anajipenda zaidi ya unavyojipenda wewe tayari ana manufaa zaidi yako. Na kama yupo mtu anawapenda wengine kuliko unavyowapenda wewe, umeshaachwa nyuma. Hakikisha unapenda sana kile unachofanya, kuliko mtu mwingine yeyote anayekifanya, jipende kuliko wengine wote wanavyojipenda. Na muhimu sana, wapende wale wanaokuzunguka na wanaotegemea unachofanya zaidi ya wengine wanavyowapenda.
 
Chochote unachopenda, kinakua, na inapokuja kwa watu, unapowapenda wanajua hilo na hivyo wao kukupenda pia.
 
6. Kusamehe.
 
Asiwepo mtu yeyote ambaye anasamehe zaidi yako, kwa sababu huyo atakuwa na faida zaidi yako. Kuwa mtu wa kusamehe kuliko wengine wote. Wasamehe hata wale ambao hawastahili kusamehewa, wale ambao wangepaswa kukuomba msamaha wewe, ila wewe chukua hatua ya kuwasamehe hata kama hawajafanya hivyo.
 
Kadiri unavyosamehe ndivyo unavyotunza muda na nguvu zako kwa matumizi mazuri zaidi kuliko ukiwa na vinyongo na wengine.
 
7. Kudadisi.
 
Usikubali awepo mtu ambaye ana udadisi zaidi yako, kuwa mtu wa kudadisi sana, jua kila kitu kinachohusiana na kile unachofanya. Usione vitu ambavyo hujui au huelewi halafu ukapotezea, badala yake jiulize kwa nini na anza kufuatilia kwa ukaribu ili uweze kupata majibu sahihi. Hii itakusaidia kujua na wakati mwingine hutakuwa gizani tena.
 
8. Kujiamini.
 
Wanaoaminiwa ni wale wanaojiamini. Kama kuna mtu anajiamini kuliko wewe, jua pia ataaminiwa zaidi na wengine kuliko wewe. Hivyo hakikisha hakuna anayejiamini zaidi yako, hakikisha wewe ndiye unayejiamini zaidi kwenye kile unachofanya na namna ambavyo kinaweza kuwasaidia wengine.
 
Na kujiamini haimaanishi kujisifia kwa wengine, bali namna unavyowaeleza watu kile unachofanya na jinsi gani kinaweza kuwasaidia.
 
9. Kujali.
 
Kuwa mtu ambaye unajali kuhusu wengine kuliko wengine wote. Kwenye dunia ambayo kila mtu anajiangalia yeye, kila mtu anafikiria ni kwa jinsi gani anaweza kunufaika kupitia wengine, ukiwa mtu wa kujali, utajitofautisha sana na wengi na hili litawafanya wengi kukuamini na kufanya kile ambacho unawataka wafanye.
 
Kuwa mtu wa kujali sana, chukua hatua ambazo hata kama wakati mwingine hazikuletei faida. Utakuwa umepanda mbegu ambayo baadaye itakuwezesha kuvuna zaidi.
 
10. Ung’ang’anizi na uvumilivu.
 
Kama yupo mtu ambaye ni king’ang’anizi zaidi yako, basi jua mtu huyo atavuna matunda zaidi yako.
 
Kama yupo mtu ambaye ni mvumilivu zaidi yako, jua huyo ana nafasi kubwa ya kupata makubwa kuliko wewe.
 
Unapaswa kuwa king’ang’anizi kuliko wengine wote, kuwa mvumilivu kuliko kila anayekuzunguka. Kwa sababu mambo haya mawili, ndiyo yatakayokuwezesha kuzivuka nyakati ngumu na kuweza kufanikiwa.
 
Hayo ndiyo maeneo kumi ya kuhakikisha hakuna yeyote anayekushinda, kwenye kile unachofanya. Kwa kuzingatia mambo hayo 10, unajitofautisha kabisa na wengine, unajiongezea thamani kubwa na kila mtu atataka kujihusisha na wewe.
 
Mambo hayo kumi hajahitaji uwe na fedha nyingi ndiyo uweze kuyafanya, wala hayahitaji uwe na akili kuliko wengine wote. Bali ni hatua ambazo kila mtu aliye makini, anaweza kuzichukua na kuyaboresha zaidi maisha yake.
 
Nina imani utachukua hatua za kufanyia kazi mambo hayo 10 ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio.
 
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
 
Rafiki na Kocha wako,
 
Dr. Makirita Amani,
 
Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha
 
Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
 
Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa
 
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog