Hongera rafiki kwa wiki hii ya 5 ya mwaka 2018. Mwaka unakatika na wiki zinapungua. Nina imani kubwa kwamba kila wiki yapo mambo unayoyafanya, ili kujisogeza karibu kabisa na ndoto yako ya maisha ya mafanikio.

Katika vipimo vyote vya muda, kuanzia sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, mwaka, muongo, karne na milenia, wiki ndiyo kipimo bora kabisa kutumia kwenye mafanikio. Hii ni kwa sababu wiki siyo ndefu kiasi cha kuona ni mbali, na pia siyo fupi kiasi cha kuona huna cha kufanya. Unaweza kuipangilia wiki yako vizuri na ukaona kila wiki umefanya nini. Na mwaka una wiki 52 tu, hivyo kila wiki ukifanya kitu, unapiga hatua kubwa.

Karibu kwenye kipengele chetu cha #TANO ZA JUMA ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza, kufanya au kukutana nayo kwenye juma ambalo tunakuwa tunalimaliza. Leo tunamaliza juma namba 5 kwa mwaka huu 2018 na hapa nimekuandalia mambo matano muhimu ambayo kuna vitu unaweza kujifunza na hata kuweza kuchukua hatua ya kuboresha maisha yako.

#NENO; SIYO JUKUMU LAKO, LAKINI LITAKUWA TATIZO LAKO.

Kuna vitu kwenye maisha yetu vinatokea, na vinakuwa matatizo kwetu, wakati havikuwa majukumu yetu. Kwa mfano, siyo jukumu lako kusomesha watoto wa jirani yako, wala kuwatafutia kazi, lakini kama hawatasoma na hawatakuwa na shughuli za kufanya, wakawa wezi, basi jua upo kwenye matatizo. Kwa sababu watakuibia na wewe pia. Siyo jukumu lako kuhakikisha kila dereva anaendesha gari kwa kufuata sheria, lakini ajali inapotokea na wewe ukahusika kwenye ajali hiyo, linakuwa tatizo lako.

Hivyo basi, siyo kila tatizo ambalo tunakutana nalo tumesababisha sisi wenyewe, lakini sisi wote kama binadamu, tunasaidiana kutengeneza matatizo. Kwa maana hiyo, kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha hutengenezi matatizo kwa wengine. Hili halimaanishi kwamba wengine hawatatengeneza matatizo kwa ajili yako, lakini litasaidia kupunguza matatizo. Vipi na wengine nao wakakazana kupunguza matatizo kwa namna hiyo? Tutakuwa na jamii bora na hata dunia salama pia, lakini inaanza na wewe, kwa kuhakikisha huwatengenezei wengine matatizo.

#1 KITABU NINACHOSOMA; THE SECRET OF SUCCESS.

Juma hili nimesoma vitabu viwili na kumaliza, na viwili sijavimaliza, naendelea kuvisoma. Lakini kitabu ninachokwenda kukushirikisha leo hapa ni THE SECRET OF SUCCESS, kilichoandikwa na William Atkinson. Ni kijitabu kidogo sana, kina kurasa 120 na nimeona nikushirikishe mambo muhimu sana kwenye kitabu hichi.

Kwanza kabisa nikuambie kwamba, HAKUNA SIRI YA MAFANIKIO, hivyo yeyote anayekuambia ana siri ya mafanikio, anakudanganya, au yeye mwenyewe hajui au kuna kitu anataka kukuuzia. Hivyo hata kama mimi nimewahi kukuambia nina siri za mafanikio, nilikuwa sijui. Iliyopo ni misingi ya mafanikio.

Lakini pia huhitaji kusoma kitabu chochote kinachohusu siri za mafanikio. Mwandishi mmoja amewahi kusema, ukishasoma kitabu cha THINK AND GROW RICH, huhitaji tena kusoma kitabu chochote kuhusu mafanikio, kwa sababu vitabu vyote vinaelezea misingi ya kwenye THINK AND GROW RICH kwa lugha tofauti tu.

Na hichi ndiyo nilichoona kwenye kijitabu hichi, kimeeleza vizuri na kwa lugha rahisi sana misingi kama DESIRE, LAW OF ATTRACTION na ATTRACTIVE PERSONALITY hizi zote zipo kwenye THINK AND GROW RICH.

Lakini kipo kitu kikubwa sana nimejifunza kwenye kitabu hichi, ambacho mwandishi amekisisitiza sana ambacho ni INDIVIDUALITY yaani UTU. Mwandishi anasema kwamba, linapokuja swala la mafanikio, wengi huangalia sheria na misingi ya mafanikio kwa ujumla wake, lakini wanasahau kwamba UTU unachangia sana kwenye mafanikio. Kwamba pamoja na kuwepo kwa misingi ya mafanikio, lakini siyo kwamba kila mtu akiifuata atapata kile ambacho wengine wamepata.

Tabia za mtu, mazingira ya mtu, ujuzi na hata uwezo uliopo ndani yake unachangia sana kiasi cha mafanikio ambacho anaweza kufikia. Watu wawili, waliopo mazingira sawa, wanaweza kufuata misingi sawa ya mafanikio lakini wote hawatakuwa na mafanikio sawa.

Hivyo ambacho nataka wewe rafiki yangu ujifunze ni kwamba, sheria na misingi yoyote ya mafanikio unayojifunza, angalia namna gani unaichanganya na sifa ambazo tayari wewe unazo. Usibebe kila unachoambiwa kama kilivyo, badala yake angalia kinaingilianaje na hali uliyonayo wewe.

Na hapo ni pagumu kwa wengi kwa sababu wengi hata hawajijui wao wenyewe vizuri, hawajui uwezo mkubwa ulipo ndani yao, na hivyo wamekuwa wakienda tu kwa mazoea. Mwandishi ameelezea hili la uwezo wa mwili na akili, na kuonesha namna ambavyo kila mtu anaweza kwenda zaidi ya anavyofikiri anaweza kwenda.

Mwisho mwandishi ameongelea kwa kina jinsi HAIBA ilivyo muhimu kwenye mafanikio ya mtu yeyote yule. Anasema watu wanavutiwa kushirikiana na mtu mwenye haiba nzuri. Na haiba nzuri haimaanishi tu utanashati na uzuri, badala yake kuna vitu vinne ambavyo mtu anapaswa kuwa navyo ili kuwa na haiba inayowavutia wengine;

Moja; kuwa mchangamfu. Ukiwa mtu ambaye umezubaa na mwenye aibu hakuna atakayevutiwa kushirikiana na wewe. Unahitaji kuwa mchangamfu, kuwa na tabasamu mara zote na kuwafanya watu wajisikie vizuri kuwa na wewe.

Mbili; kujiamini. Kama hujiamini mwenyewe, hakuna anayeweza kukuamini. Jiamini wewe mwenyewe, amini kile unachofanya na amini kile ambacho unamwambia mtu, na mtu hatakuwa na sababu ya kutokukuamini.

Tatu; kujali wengine. Kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, tunajali mambo yetu zaidi ya wengine. Na hivyo ukiweza kwenda kinyume na hili, ukajali ya wengine, unawafanya wavutiwe kuwa karibu na wewe. Na mwandishi anatuambia sehemu rahisi ya kuanzia hilo la kujali wengine ni kuwa msikilizaji mzuri. Unapompa mtu nafasi ya kumsikiliza, akakueleza mambo yake, anajisikia vizuri sana.

Nne; kujidhibiti. Mwandishi amezungumzia hili hasa kwenye hasira, na anasema hasira ni alama ya udhaifu na siyo ushujaa, anasema hasira ni ukichaa, hivyo ukiruhusu kuingia kwenye hasira, unapoteza heshima yako mbele ya wengine. Na sidhani kama kuna mtu anapenda kukaa karibu na mtu mwenye hasira.

Na hayo rafiki, hakuna siri, huenda ulikuwa unayajua na hivyo umejikumbusha, au huenda hukuwa unayajua na hivyo umejifunza, kikubwa sana ni KUCHUKUA HATUA.

#2 MAKALA YA WIKI; MAENEO KUMI YA KUSHINDA.

Huwa sipendi mashindano, lakini napenda kushinda. Nikiwa na maana kwamba, chochote ambacho nataka kuwa nacho au kukifikia, basi nakazana nikipate au kukifikia kwa ubora wa hali ya juu sana, ubora au viwango ambavyo havijaweza kufikiwa na mwingine yeyote.

Kwenye makala ya wiki hii, nimekushirikisha maeneo kumi ambayo unapaswa kushinda kwenye maisha yako, maeneo ambayo hupaswi kabisa kuruhusu mtu mwingine akushinde. Kama hukusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Usikubali Mtu Yeyote Akushinde Kwenye Maeneo Haya Kumi(10) Muhimu Kwa Mafanikio Ya Maisha Yako. (https://amkamtanzania.com/2018/02/02/usikubali-mtu-yeyote-akushinde-kwenye-maeneo-haya-kumi10-muhimu-kwa-mafanikio-ya-maisha-yako/ )

Shinda kwenye maeneo hayo kumi, kwa kushindana na wewe binafsi na maisha yako yatakuwa bora kabisa.

#3 NILICHOONA JUMA HILI; FAO LA KUJITOA.

Wiki hii nimeona watu wakiwa na mijadala mingi kuhusu muswada wa sheria ya mifuko ya jamii wa mwaka 2017 ambao umejadiliwa na kupitishwa bungeni. Wengi wameeleza namna ambavyo sheria hiyo itakavyowaumiza wafanyakazi, wengine wameeleza namna ambavyo ni manufaa kwa wafanyakazi.

Sasa kama unavyonijua rafiki yangu, sipo upande wa wanaosema ni nzuri au ni mbaya, kila kitu huwa kina pande mbili, uzuri na ubaya, faida na hasara, kila kitu, hata uwepo wako hapa duniani.

Sasa nirudi kwa yule muhimu kabisa ambaye ni mfanyakazi, na kama wewe rafiki yangu unayesoma hapa ni mfanyakazi, basi neno langu kwako ni moja, IZIDI AKILI SERIKALI PAMOJA NA MIFUKO HII.

Turudi kwenye msingi wa mifuko hii, kazi ambayo mifuko hii inafanya, ni kuchukua sehemu ya kipato chako ambacho unakatwa kwenye mshahara, kisha inakiwekeza na baadaye inakuja kukulipa pamoja na riba kutokana na muda uliokatwa na kuchangia, ambao pia ndiyo muda fedha hizo zimewekezwa.

Sasa ninachokushauri mimi ni hichi, izidi mifuko hii akili, kwa kujikata sehemu ya 10 ya kipato chako cha kila mwezi, halafu kuwekeza kwenye njia ambazo unaweza kuzisimamia wewe mwenyewe vizuri. Hata kama kipato chako ni kidogo kiasi gani, hata kama mahitaji ya maisha yako ni mengi kiasi gani, kila unapopokea mshahara, ondoa asilimia kumi na wekeza. Fanya hivyo kwa miaka yote ambayo utakuwa kwenye kazi, huku ukiendelea na mipango yako mingine ya kuongeza kipato kwa njia za pembeni, halafu siku ukiona sasa umeshafika nafasi ya kuachana na ajira, unaweza kuondoka, halafu ukawa na fao lako la kujitoa, kupitia uwekezaji unaofanya kwenye ile asilimia kumi uliyokuwa unajikata wewe mwenyewe. Halafu sasa itakapofika muda wa kulipwa ile uliyokatwa kwenye mifuko hiyo kulingana na sheria, basi utapata, lakini hutakuwa na haraka wala kutegemea kama mafao pekee ya maisha yako.

Ninachosema ni hichi, tengeneza mfuko wako mwenyewe wa mafao, na uweze kuudhibiti uwezavyo. Ndiyo utaendelea kukatwa kwenye hiyo mifuko ya serikali, lakini haitakuwa tumaini pekee kwako.

Halafu naendelea kukukumbusha, kamwe usitegemee ajira pekee kama njia pekee ya kipato kwako, kama leo sheria kama hiyo imepitishwa, unajua ni sheria gani itakuja kupitishwa huko mbeleni? Tengeneza uhuru wako mapema, na unapoona yanayoendelea ni tofauti na ulivyotegemea, siku zote mlango utakuwa wazi kwako. Lakini ukishakuwa huna namna, utanyanyasika kwenye kazi, na utanyanyasika kwenye kipato kidogo, na hatimaye sasa unapofikia kustaafu utanyanyasika na mafao yako. Yaani maisha yako yote yatakuwa ya kunyanyasika, kitu ambacho hupaswi kuruhusu kitokee.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KITABU CHA BIASHARA NDANI YA AJIRA.

Kwa mambo yanayoendelea kwenye ajira kwa sasa, kama umeajiriwa na njia pekee ya kipato unayotegemea ni ajira yako, basi hakikisha umesoma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA. Kama mpaka sasa hujasoma kitabu hicho, hakikisha unakisoma na unachukua hatua mara moja, ili uweze kujitengenezea msingi mzuri wa fedha na kipato kwenye maisha yako.

Kitabu kinapatikana kwa softcopy na hardcopy. Softcopy inatumwa kwa email na gharama yake ni tsh 10,000/= kukipata tuma fedha kwa namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu. Hardcopy inapatikana kwenye duka la vitabu HOUSE OF WISDOM lililopo Dar, posta mtaa wa samora jengo la NHC karibu na makao makuu ya TTCL.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; WAIBIE WENGINE KIRAHISI.

“Employ your time in improving yourself by other men’s writings so that you shall come easily by what others have laboured hard for.” – Winston Churchill

Winston Churchill aliyekuwa waziri mkuu wa uingereza na mmoja wa watu waliowahi kuwa na mamlaka makubwa duniani anasema kwamba, tumia muda wako kujiboresha kwa kusoma maandiko ya wengine ili yale ambayo wengine wamejifunza kwa nguvu na ugumu, yaje kwa urahisi kwako.

Ukweli ni kwamba, watu wanapoandika vitabu, wanashirikisha yale ambayo wao wamejifunza kwa kazi, maumivu na hata kushindwa. Pia wanakuwa wamefanya utafiti mkubwa mpaka kuja na kitu walichoandika. Lakini wewe unaposoma kitabu, unapata maarifa hayo kwa urahisi, huhitaji kuteseka kama yule ambaye ameandika kitabu.

Je huoni kama hii ni fursa nzuri sana kwako kuwaibia wengine uzoefu wao kwa njia rahisi? Neno ni moja rafiki, soma vitabu.

Uwe na wakati mwema rafiki yangu, na hakikisha unajipanga vyema kwa juma la sita tunalokwenda kuanza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog