Kuna mambo ambayo tunakuwa tumepanga au kupangiwa kufanya, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, tunashindwa kuyafanya. Haya hutuletea msongo wa mawazo na kutuzuia hata kufanya mambo mengine kwa utulivu na amani ya moyo.
Watu wengi wamekuwa wakishindwa kufanya makubwa kutokana na msongo walionao kwa yale waliyoshindwa kufanya au waliyofanya na wakashindwa. Hivyo kama kila mtu akiweza kuondokana na msongo, kwa kutua ile mizigo ambayo ameibeba, atajipa nafasi kubwa ya kuweza kufanya makubwa.

Zipo njia mbili rahisi sana za kuondokana na msongo wa mawazo, njia hizi zitakuwezesha kusafisha kabisa ule mlolongo wa mambo unaojiambia inabidi ufanye japokuwa huna muda wa kuyafanya.
Njia ya kwanza; SIWEZI KUFANYA.
Njia ya kwanza ya kuondokana na msongo wa mawazo ni kujiambia SIWEZI KUFANYA. Hapa unaangalia yale mambo unayotaka kufanya, ambayo yanakupa msongo wa mawazo kwa sababu umekuwa unasema unafanya kwa muda mrefu. Kisha kuchambua yale ambayo huwezi kuyafanya kwa sasa, labda kutokana na muda au uwezo wa kuyafanya. Jiambie wazi kwamba HUWEZI KUYAFANYA na hutayafanya.
Hata kama ni watu wengine wanakutaka ufanye, na unaona kabisa huwezi kuyafanya, waambie wazi huwezi kufanya. Hili linakupa uhuru na linakuondolea msongo wa mawazo wa kuwa na mambo mengi ya kufanya.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Dawa Ya Msongo Wa Mawazo Ni Hii.
Njia ya pili; KUFANYA.
Njia ya pili ya kuondokana na msongo wa mawazo ni KUFANYA. Hapa unaangalia yale ambayo unaweza kuyafanya na kuanza kuyafanya mara moja. Chochote ambacho kipo ndani ya uwezo wako kufanya, anza kukifanya mara moja. Usisubirie wala kuahirisha, anza kukifanya sasa hivi.
Hii itaondoa mlolongo wa mengi unayopanga kufanya ambayo yanakujengea msongo zaidi na kupunguza yale yanayosubiria kufanya.
Njia zote hizi mbili zinakamilisha kitu kimoja, kupunguza mrundikano wa mambo ya kufanya ambao ndiyo unakuletea msongo wa mawazo. Hivyo ukitenga yale ambayo HUWEZI KUFANYA, na kuachana nayo mara moja kisha ukabaki na yale unayoweza kufanya na ukaanza KUYAFANYA, siyo muda utajikuta huna tena mlolongo wa mengi ya kufanya na hivyo msongo wa mawazo unapungua. Njia hizi mbili zinakuweka huru na majukumu ambayo yamekuwa mzigo kwako na kusababisha msongo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog