Sometimes even to live is an act of courage. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera rafiki kwa siku hii nzuri na ya kipekee wana kwetu.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.
Pia kwa mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tutaweza kufanya makubwa kwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari KUNA WAKATI KUISHI NI TENDO LA KISHUJAA…
Umewahi kufika wakati kwenye maisha yako ukaona kama ndiyo mwisho kabisa wa maisha hayo?
Ukaona hakuna tena unachoweza kufanya na kila unachojaribu hupati matokeo mazuri?

Kila mmoja wetu huwa anafikia hatua hii kwenye maisha yake.
Wapo ambao huwa wanakatisha maisha yao kwenye hatua hiyo kwa kujiua.
Wapo ambao wanakata tamaa na kujiingiza kwenye ulevi.
Na wapo ambao wanajiambia liwalo na liwe na kuacha kuchukua hatua.

Lakini wakati kama huu, ndiyo kuishi linakuwa tendo la kishujaa.
Hapa ndipo unapohitaji ushujaa wa kuendelea kuweka juhudi kubwa, licha ya kutoona matumaini ya matokeo mazuri.
Hapa ndipo unapohitaji kuwa na uhakika wa kupata matokeo bora japo hakuna dalili zozote zinazoonesha hilo.

Ni mashujaa wachache ambao wanachukua hatua hii ndiyo wanaopiga hatua kubwa.
Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wanapitia magumu, ila wanaofanikiwa wanaishi kishujaa kwenye magumu hayo, huku walinaoshindwa wakikata tamaa kwenye magumu hayo.

Nenda kaishi kishujaa leo na kila siku ya maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha