Umewahi kusikia kitu kipya kikakuhamasisha sana kuchukua hatua, na ukajiambia utabadilika, na kweli siku chache za kwanza ukawa umebadilika lakini baadaye ukarudi kwenye tabia zile zile za awali?
Umewahi kutamani sana kubadili kile unachofanya, ukataka ufanye kazi bora kabisa, utoe thamani kubwa kwa wengine lakini ukajikuta unaishia kufanya yale uliyozoea kufanya?
Yote hayo yamekuwa yanatokea kwa sababu tumekuwa tunaenda na mabadiliko kwa njia ambayo siyo sahihi. Tumekuwa tunakimbilia kubadili kile tunachofanya, kabla hatujafanya mabadiliko kwenye mizizi ya hicho tunachofanya.
Ni sawa na kuwa na mti wa mwembe, lakini wewe unataka machungwa, hivyo ukakata matawi yote ya mwembe ili ukichipua utoe matawi ya machungwa. Ni kitu kisichowezekana kwa sababu msingi bado ni mwembe na siyo mchungwa.

Hatua sahihi za kubadilika zinaenda kama ifuatavyo;
Kwanza unabadili kile ambacho unakijua. Hapa mabadiliko yanaanza na ujuzi wako, elimu na uelewa ulionao juu ya kitu unachotaka kubadili. Mengi unayojua kuhusu maeneo uliyokwama na hupigi hatua yamepitwa na wakati au siyo sahihi. Hivyo bila ya kubadili kile unachojua, huwezi kupiga hatua. Unabadili unachojua kwa kujifunza, kujisomea na hata kuwaangalia wengine wanaofanya.
Pili unabadili kile ambacho unaamini. Imani yako ndiyo inayoongoza matendo yako. Hakuna binadamu anayefanya kinyume na anavyoamini. Hivyo kama utataka kubadili kile unachofanya, kabla ya kubadili unachoamini, unajidanganya. Angalia kwanza unaamini nini kwenye kile unachobadili, na kama imani yako inakinzana na unachotaka kufanya, fanyia kazi imani yako kwanza. Uzuri ni kwamba, kadiri unavyobadili unachojua, kadiri unavyojifunza, ndivyo pia unavyobadili na kujenga imani mpya kwa yale mapya unayojifunza.
SOMA; UKURASA WA 933; Watu Wataendelea Kuhukumu Kitabu Kwa Ganda La Nje…
Baada ya kubadili hayo mawili, ndipo sasa unaweza kubadili kile unachofanya, unaweza kubadili hatua unazochukua kwa kuwa unajua vizuri na imani yako inaendana na hicho unachopanga kufanya. Hapa ndipo unapoweza kuchukua hatua ambazo zinaleta mabadiliko ya kweli kwenye maisha yako.
Unapotaka kuyabadili maisha yako, usiwe na haraka na usitafute njia ya mkato. Mabadiliko ya kweli ni mchakato na yanahitaji muda. Siyo tukio la mara moja. Ndiyo maana unahitaji kubadili mengi ya ndani kabla hujabadili yale ya nje.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog