Kuna wakati kwenye maisha watu watakuonea, ni mara nyingi na inaweza kutokea kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako. Lakini huwezi kupambana na kila anayekuonea kila wakati.

Kuna wakati kwenye maisha, watu watachukua sifa kwenye kazi ambayo umeifanya wewe. Unakuwa umekazana kweli na kazi hiyo, umeweka nguvu, muda na ujuzi wako, halafu mtu anakuja kuchukua sifa kirahisi kabisa, kwamba yeye ndiye aliyeifanya. Huwezi kupambana na kila anayejibebea sifa kupitia kazi zako.

Ukiona

Kuna wakati kwenye maisha, watu watakutumia kama tambara la mlangoni, watakutumia kama ngazi ya wao kupanda juu zaidi, wakati wewe unaendelea kubaki chini. Huwezi kupambana na kila anayekutumia kama ngazi ya yeye kupanda juu zaidi.

Dhana ni kwamba, unahitaji kujua ni wakati gani sahihi kwako kupambana na aina hizi za watu kwenye maisha yako, ambao wanatafuta njia za kunufaika zaidi kupitia wewe.

Lazima ujue wakati sahihi kwa sababu kama utajaribu kupambana na kila mtu, utaishia kuchoka na kushindwa kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako. Kama utaanza kukimbizana na kila anayetaka kuchukua sifa kupitia kazi zako, utajikuta unatumia muda mwingi kukimbizana na wanaoiba kazi zako kuliko muda unaoutumia kutoa kazi nyingine bora zaidi.

SOMA; UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…

Hivyo chagua mapambano yako kwa umakini, chagua mapambano kwa kuangalia baada ya mapambano hayo unakuwa umepiga hatua kiasi gani. Usipambane tu kwa raha ya kuwashinda wengine, au kuwaonesha kwamba wamekosea. Bali pambana kama una nafasi ya kupiga hatua zaidi, pambana kama kuna manufaa zaidi kuliko tu kushinda.

Tunapaswa kuelewa kwamba, dunia ndivyo ilivyo, kila wakati watakuwepo watu wa aina hiyo, wa kutaka kutuonea, kutuibia na hata kututumia kwa manufaa yao. Ni muhimu kujua wakati sahihi wa kupambana na kuepuka kupambana na kila anayejaribu kufanya hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog