Fedha na malipo ndiyo mada nzuri kuliko zote kwenye mijadala yetu ya kila siku. Ninaposema nzuri siyo lazima uwe unaifurahia, lakini hichi ni kitu ambacho kila mtu lazima akifikiria kila siku. Kwa wengine ndiyo kitu wanafikiria siku nzima, hasa pale kipato kinapokuwa kidogo, matumizi makubwa na madeni mengi.

Lakini pamoja na kufikiria sana kuhusu fedha, dhana ambayo wengi wanayo kifedha, hasa kwa upande wa malipo ni dhana mbovu na inawapotosha sana.

Ninachoweza kusema kwa uhakika ni kwamba, mambo mengi unayoamini kuhusu fedha na malipo yako, ni uongo na hayo ndiyo yanasababisha kila siku unakuwa na changamoto za kifedha.

Labda nikuulize swali, umeshawahi kujiona kwamba umefanya kila ambacho uliambiwa ukifanya utapata fedha, halafu ukashangaa bado fedha huzipati? Lakini wakati huo huo ukiangalia wengine ambao hawafanyi kama unavyofanya wewe, hawana changamoto za fedha kama wewe?

8810e-100_75602bed1_thumb5b15d

Labda tukitumia mfano tutaelewana vizuri zaidi. Tukianza, kila mtu alishawahi kuambiwa hili, kwamba nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri, kisha utapata kazi nzuri na maisha yatakuwa mazuri. Unakuwa mtiifu kwenye hilo, unasoma kwa juhudi kweli, unafaulu, unakazana kutafuta kazi, unapata, lakini kipato hakikutoshelezi. Ukiwa kazini, ukapata tena wazo, kipato chako ni kidogo kwa sababu kiwango chako cha elimu ni kidogo, ukiongeza elimu basi kipato chako kinaongezeka. Ukaongeza elimu, na kweli kipato kikaongezeka, lakini bado changamoto za fedha hazikuisha? Wakati huo huo kuna watu ambao unaona hawana elimu kama yako, lakini maisha yao yanaenda!

Hapo ndipo unapoweza kushawishika kwamba watu wana namna, ambayo wewe huijui. Ni kweli wana namna, lakini siyo namna unayofikiria wewe, bali ni namna bora, ya mtazamo sahihi wa kifedha unaowawezesha kuwa na kipato kikubwa sana kwenye chochote wanachofanya.

Kwenye makala hii ya leo, utakwenda kujifunza namna hii, na jinsi ya kuitumia ili na wewe pia, uweze kuondoka kwenye changamoto za kifedha, ulipwe vizuri na kuondoka kwenye madeni.

Lakini kabla hatujaona mtazamo huo sahihi, kwanza tuangalie tumekuwa tunaanguka wapi kifedha na kwenye kipato. Na kwa utafiti wangu, kupitia watu ambao nimekuwa nawakochi na kuwasaidia kupiga hatua, nimegundua mitazamo mitano kuhusu kipato ambayo inawafanya wengi kuwa na kipato kidogo.

Ifuatayo ni mitazamo mitano ambayo inakufanya uwe na kipato kidogo licha ya kuweka juhudi kubwa kwenye kazi zako.

Moja; unalipwa kulingana na elimu uliyonayo.

Mtazamo ambao umewaingiza wengi sana kwenye matatizo ya kifedha ni kuamini kwamba malipo yao kwenye ajira zao na hata biashara ambazo wanafanya, yanategemea elimu waliyonayo. Kwa mtazamo huu, watu wamekuwa wanakazana kusoma na kuongeza elimu, lakini mwisho wa siku wanajikuta kwenye matatizo zaidi kifedha.

Tena kwa elimu za kutegemea mikopo au ufadhili, yeyote anayeongeza elimu kwa lengo tu la kuongeza kipato, anatengeneza matatizo makubwa sana kwenye maisha yake, hasa kifedha.

Sisemi elimu siyo muhimu, ila ninachosema unapotumia elimu kama njia ya kuongeza kipato na kuondokana na changamoto zako za kifedha, umeshapoteza njia.

SOMA; Jambo Moja La Uhakika Unalopaswa Kujua Kuhusu Mafanikio Kwenye Maisha Yako.

Mbili; unalipwa kulingana na muda unaofanya kazi.

Moja ya vitu ambavyo mfumo rasmi wa ajira umewajengea watu kuhusu ufanyaji wa kazi ni kwamba, muda ndiyo kipimo muhimu. Hivyo kama utafanya kazi masaa mengi zaidi, basi kipato chako kitakuwa kikubwa zaidi. Na hili lina ukweli, lakini kwa kiasi kidogo sana, kwa sababu, kuna masaa 24 pekee kwa siku. Hivyo hata kama utafanya kazi usiku na mchana, bado huwezi kutengeneza muda zaidi. Hivyo kwa vyovyote vile, bado utakuwa na ukomo wa kipato, kwa sababu ya ukomo wa muda.

Kadhalika hapa sisemi kwamba usifanye kazi kwa muda mrefu, lakini dhana kwamba muda pekee utakutoa kwenye changamoto za kifedha ni jambo la ajabu, na kujitengenezea matatizo zaidi.

Tatu; unalipwa kulingana na uzoefu wako.

Kwamba utaanza kazi na mshahara kidogo, halafu kadiri unavyoendelea kukaa kwenye kazi hiyo, mshahara wako unaendelea kupanda. Hivyo kama utafanya kazi miaka 20 au 30 basi mshahara wako utapanda sana. Hapa kuna ukweli kiasi, lakini uongo ni mkubwa zaidi. Je ni kweli kwamba kipato kinaongezeka sawasawa kulingana na miaka ambayo mtu amefanya kazi? Au kipato kinaongezeka kufidia mfumuko wa bei ambao huwa unatokea kila mwaka?

Kutegemea uzoefu pekee kama kigezo cha kuongezeka kwa kipato ni dhana potofu. Kwa sababu licha ya uzoefu wa muda mrefu, bado sehemu ya kipato inayoongezeka ni ndogo sana, huku ukizingatia kadiri muda unavyokwenda gharama za maisha ya mtu zinazidi kuwa kubwa zaidi. Kama alianza kazi akiwa mwenyewe, kadiri anavyokwenda anakuwa na familia sasa.

Changamoto nyingine kubwa kuhusu uzoefu ni kwamba, wengi hawana uzoefu wanaosema wanao. Wengi wanaokuambia nina uzoefu wa miaka kumi, wanachomaanisha ni kwamba, wana uzoefu wa mwaka mmoja, uliojirudia mara kumi. Kwa sababu wanakuwa wanafanya mambo kwa mazoea na hakuna wanachobadili.

Nne; unalipwa kulingana na unavyoonekana unafanya kazi.

Maajabu huwa hayaishi duniani, na binadamu sisi ni viumbe wazuri sana kwenye maigizo. Watu wengi sana wamekuwa wanaigiza kazi ili kuonekana ni wachapa kazi wakiamini hilo litaongeza kipato chao. Hapa ndipo unapokuta watu wakiahidi vitu ambavyo hawawezi kutekeleza, wakikazana kufanya mambo yanayoonekana kwa nje, lakini kwa ndani hayana maana yoyote.

Kwenye baadhi ya maeneo hili linafanya kazi kiasi, hasa kwenye siasa na taasisi za umma, lakini lina ukomo mkubwa sana wa kipato. Kwa sababu unakuwa unategemea zaidi neema ya mtu mwingine kukuona unakazana ndiyo akuongezee malipo. Mpango ambao siyo mzuri kabisa.

Tano; unalipwa kwa sababu unastahili.

Yaani kila ninapokuwa nawasikiliza watu wakilalamika kuhusu malipo madogo wanayopokea, huwa nashangaa kwa nini watu hawaoni zama zimeshabadilika sana. Zile zama za vyama vya wafanyakazi kuendesha migomo kushinikiza waajiri kuongeza malipo, kwa sababu watu wanastahili  kulipwa zaidi zimeshapita. Hakuna tena anayeweza kudai kulipwa zaidi kwa sababu anastahili kulipwa, kwa sababu hakuna tena hata ambao wanaajiri.

Hivyo kufikiria kwamba una haki ya kulipwa kwa sababu unastahili, unajidanganya. Kwa wingi wa watu wanaohitaji kazi, na uchache wa nafasi za kazi, hustahili chochote kutoka kwa anayekuajiri au kukulipa. Bali yeye ndiye anayestahili kitu kutoka kwako.

Kwenye dhana hizo tano, nina imani umeona wapi umekuwa unakwama, wapi ambapo umewekeza nguvu kubwa lakini matokeo huyaoni.

Swali muhimu sana ni je upi mtazamo sahihi wa kukuwezesha kuongeza kipato chako? Ni kipi ambacho ukikifanyia kazi kweli, kitakuhakikishia kuwa na kipato kikubwa wakati wowote?

Na jibu ni kwamba, kipo kitu ambacho ukikisimamia hicho, kikawa ndiyo mwongozo wako kwenye kazi zako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla, utashangaa namna ambavyo kipato chako kinaongezeka bila hata ya kusumbuka sana.

Ni mwandishi Jim Rhon ambaye alinukuu hili vizuri sana, akisema; You don’t get paid for the hour. You get paid for the value you bring to the hour. Akimaanisha kwamba, hulipwi kwa saa unayofanya kazi, bali unalipwa kwa thamani unayotengeneza kwenye saa unayofanya kazi.

Na mimi naweza kusema kwa kujiamini kabisa ya kwamba ukiweza kuishi kauli hii moja tu kila siku, utajiweka vizuri sana kwa upande wa kipato. Kauli hiyo ni kwamba, unalipwa kwa thamani unayozalisha, thamani unayoitoa kwa wengine. Jiambie kauli hii kila unapoamka asubuhi, jiambie kauli hii kila unapoanza kazi au biashara yako, jiambie kauli hii kila unapofikiria kuhusu fedha. Jiambie kwa sauti; nalipwa kulingana na thamani ninayozalisha, je nizalishe thamani gani sasa ili nilipwe zaidi?

Ukiweza kuiishi kauli hii kila siku, ukaweza kuifanyia kazi, iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara, una uhakika wa kuongeza kipato chako, kadiri utakavyo. Kwa sababu kitu pekee unachohitaji kufanya, ni kuzalisha thamani zaidi kwa wengine. Na kwa dunia hii ambayo kila mtu ana kitu cha kulalamika kwenye kila kitu, zipo fursa nyingi sana za wewe kuongeza kipato chako kwa kutoa thamani zaidi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Do More Great Work (Acha Kuwa Bize Na Anza Kufanya Kazi Yenye Maana)

Yafuatayo ni mambo matano muhimu sana ya kuzingatia katika kutoa thamani ili kuweza kuboresha kipato chako zaidi.

  1. Chagua tatizo au changamoto ambayo utaitatua.

Hatua ya kwanza kabisa unayohitaji kuchukua katika kuzalisha thamani kwa ajili ya wengine, ni kuchagua tatizo au changamoto ambayo wengine wanayo na wewe unaweza kuifanyia kazi. Kwa kutatua changamoto au tatizo hilo, unakuwa umeongeza thamani kwa wengine, na wao hawatakuwa na budi bali kukulipa kulingana na namna ulivyowasaidia kutatua matatizo na changamoto zao.

Sasa jambo muhimu sana ni hili, kadiri unavyotatua matatizo na changamoto ngumu, ndivyo thamani inakuwa kubwa na malipo makubwa pia. Hivyo kama hapo ulipo malipo unayopata ni madogo kuwa na uhakika na hili, kwamba changamoto au matatizo unayotatua ni madogo. Angalia makubwa zaidi na toa thamani kubwa zaidi.

  1. Jua nje ndani kile ambacho unakifanya.

Kauli kwamba unalipwa kulingana na thamani unayozalisha ni rahisi kusema, lakini utekelezaji wake ni mgumu mno. Kwa sababu unakutaka ujue kwa hakika sana kile ambacho unakifanya. Unahitaji kujua kwa kina, kujifunza sana, kwa kifupi kujua kila kinachopaswa kujulikana kuhusiana na hicho unachofanya. Ubaya ni kwamba, hakuna atakayekuongoza kipi na kipi unapaswa kujua, wala hakuna mtaala wa kujifunza, hivyo wewe unapaswa kujua kila kitu. Kuanzia historia ya kitu hicho mpaka mapinduzi na mabadiliko yanayoendelea kila siku.

Kwa kifupi unahitaji kuchagua kuwa mwanafunzi wa maisha kwenye kile ulichochagua kufanya. Hii itakuwezesha wewe kuziona fursa nzuri ambazo wengine wengi hawazioni.

  1. Unahitaji muda.

Tumesema kwamba hulipwi kwa muda bali kwa thamani, lakini pia usitegemee kwamba utaweza kuzalisha thamani hiyo ndani ya muda mfupi, unahitaji muda mpaka kufikia hatua za juu kabisa za kuzalisha thamani kubwa kwa wengi zaidi. Kama unatatua tatizo gumu, utahitaji muda mpaka uweze kuja na suluhisho ambalo linaongeza thamani kwa wengine. Hivyo kazana kuzalisha thamani, huku ukijua unahitaji muda kupata matokeo makubwa unayotarajia kupata.

  1. Kataa kabisa mazoea.

Wapo watu ambao wanaanzia chini, wanaweka juhudi, wanaanza kupata matokeo mazuri, halafu baadaye wanaanza kuporomoka. Wengi wanakuwa wameingia kwenye mtego wa mazoea. Kwa kuwa ameshapata njia ambayo inawapa wanachotaka, wanafikiri njia hiyo itadumu milele. Kwa dunia ya sasa, mambo yanabadilika haraka mno. Popote unapokuwa, angalia mbele zaidi. Kila siku kazana kuwa bora zaidi ya jana, chagua kupiga hatua zaidi ili kuweza kuziona fursa mpya na kuzitumia.

  1. Juhudi, kujitoa na kutokukata tamaa kunashinda elimu, vipaji na uzoefu.

Kuna vitu ambavyo watu wamekuwa hawavipi uzito mkubwa kwenye mafanikio kwenye kazi au biashara. Vitu hivyo ni JUHUDI, KUJITOA NA KUTOKUKATA TAMAA. Vitu hivi vitatu, kuweka juhudi kubwa, kujitoa hasa kuhakikisha unapata unachotaka na kutokukata tamaa hata kama unakutana na magumu, vinashinda elimu kubwa, vipaji vikubwa na hata uzoefu mkubwa. Hivyo kila unapojiangalia na kuona unakosa vile ambavyo wengi wanaonekana kuwa navyo, wewe rudi kwenye hivyo vitatu, JUHUDI, KUJITOA NA KUTOKUKATA TAMAA.

Rafiki yangu, tunalipwa kulingana na thamani tunayozalisha kwa ajili ya wengine. Hivyo pale ambapo tupo sasa, ni kulingana na thamani tunayozalisha, tukitaka kupiga hatua zaidi, lazima tuwe tayari kuzalisha thamani zaidi.

Je ni thamani gani zaidi upo tayari kuizalisha?

RASILIMALI YA KUKUSAIDIA KWENYE HILI.

Rafiki yangu, kama ambavyo nimejipa jukumu la kuhakikisha unapata maarifa bora ya kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi, ninayo rasilimali nzuri sana kwa ajili yako, kwenye eneo hili la fedha, rasilimali hii ni kitabu; KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, Kitabu hichi kimeeleza kwa kina, sababu 25 zinazowafanya wengi kufia kwenye umasikini. Kama bado hujakisoma, kipate na ukisome sasa, kuna mengi muhimu ya kujifunza na kuchukua hatua.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Kitabu ni softcopy, kinatumwa kwa njia ya email na unaweza kukisoma kwenye simu yako, tablet au kompyuta. Kitabu kinauzwa tsh 5,000/= na kukipata tuma fedha tsh 5,000/= kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma email yako kwenye moja ya namba hizo pamoja na jina la kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI kisha nitakutumia kitabu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog