Rafiki yangu mpendwa,
Linapokuja swala la fedha, kila mtu ana namba na viwango vyake. Kwa sababu tunatofautiana ndoto, kazi/biashara, kipato, mitindo ya maisha na hata mazingira, matokeo yetu ya kifedha hayawezi kulingana.
Hivyo kujipima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia wengine ni kujiumiza na hata kujirudisha nyuma, kwa sababu kuna namba nyingi ambazo utakuwa huzijui kuhusu wengine. Kwa mfano unaweza kumwona mtu kwa nje anaonekana kuwa na vitu vinavyoashiria ana fedha nyingi, lakini kumbe vitu vyote hivyo amepata kwa mkopo ambao ataulipa maisha yake yote.
Pia unaweza kumwona mtu ukafikiri hayupo vizuri kifedha kwa mwonekano wake wa nje, kumbe anafanya uwekezaji ambao baadaye utamwezesha kufikia uhuru wa kifedha.
Kwa kuwa ni vigumu kupima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia watu wengine, unahitaji kujitumia wewe mwenyewe. Lakini swali ni je unajipimaje kwenye hatua ulizopiga kifedha?
Jibu ndiyo makala niliyokuandalia leo, vipo viwango vitano au kwa maneno mengine namba tano muhimu za kuangalia ili kujipima afya yako kifedha na kujua umepiga hatua kiasi gani.
Viwango hivi vitano vinakupa mwanga wa ulikotoka, ulipo na unapokwenda kifedha. Ni viwango ambavyo vitakuonesha wapi unafanya vizuri na wapi hufanyi vizuri ili uweze kuchukua hatua sahihi kufika pale unapotaka kufika kifedha.
Viwango vitano vya kupima afya yako kifedha.
Moja; kiwango cha akiba.
Hichi ni kiwango kinachoonesha maandalizi yako uliyonayo sasa kwa upande wa fedha. Kadiri unavyokuwa na akiba kubwa kifedha, ndivyo unavyoweza kujilinda na dharura mbalimbali zinazoweza kukutokea. Akiba unayokuwa nayo ndiyo itakukinga usiingie kwenye madeni mabaya pale unapokutana na changamoto ambazo hukuzitegemea.
Kiwango sahihi cha akiba unayopaswa kuwa nayo ni ile inayoweza kutosheleza kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka mwaka mmoja hata kama utakuwa huna kipato kabisa katika kipindi hicho.
Kuza kiwango chako cha akiba na hili litakupa pumziko na kukuondolea wasiwasi kuhusu fedha kitu ambacho kitakuwezesha kufanya mambo yako kwa utulivu na ufanisi mkubwa.
Mbili; kiwango cha madeni.
Kiasi cha fedha unachodaiwa na wengine kutokana na vitu ulivyonunua bila ya kuwa na fedha ni kipimo cha maamuzi yako ya kifedha kwa siku za nyuma. Kadiri madeni yako yanavyokuwa makubwa, ndivyo sehemu kubwa ya kipato chako inavyoelekea kwenye kulipa madeni hayo na wewe kubaki na kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukutosheleza.
Unahitaji kutokuwa na deni binafsi kabisa, na madeni mazuri unayopaswa kuwa nayo ni yale yanayojilipa yenyewe. Madeni yanayojilipa yenyewe ni yale ambayo yanazalisha faida na faida hiyo unatumia kulipa deni. Haya ni madeni ambayo hayakuumizi.
Lakini madeni ambayo unalipa kwa fedha zako unazopata kwenye shughuli zako binafsi, ni utumwa ambao utakutesa kwa muda mrefu. Kama upo kwenye madeni ya aina hii kazana kuondoka na usiingie tena ili kuepuka kujiweka kwenye wakati mgumu kifedha.
Tatu; kiwango cha uwekezaji wa baadaye.
Kiwango ambacho umekiwekeza kwenye maeneo ambayo yanazalisha riba au faida ni kipimo muhimu kwa maandalizi yako ya kifedha ya baadaye. Kama hapo ulipo hujafanya uwekezaji wote kwa ajili ya baadaye, kama hujawa na maandalizi ya kukuwezesha kuingiza kipato bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja, huna maandalizi ya kifedha ya baadaye, na haupo eneo zuri kifedha.
Unahitaji kufanya uwekezaji kwa ajili ya baadaye, kwa sababu utakuja wakati ambapo huna uwezo wa kufanya kazi kama unavyofanya sasa, lakini una mahitaji muhimu kwa maisha yako. Unapokuwa umewekeza na uwekezaji unazalisha, maisha yako yanakwenda vizuri.
Kiwango sahihi cha uwekezaji unachopaswa kuwa nacho ni kile ambacho kinazalisha faida au riba ambayo inakuwezesha wewe kuendesha maisha yako kwa kadiri ya mahitaji yako.
Nne; kiwango cha utoaji.
Kiasi cha fedha unachotoa kwa wengine bila ya kutegemea kupata chochote ni kiwango kingine muhimu sana cha kupima afya yako kifedha na kujua hatua ulizopiga. Kwa kadiri unavyotoa zaidi ndivyo unavyoonesha kwamba unaitumia fedha na siyo fedha inakutumia wewe.
Unahitaji kuwa na utaratibu wa kutoa fedha kuwasaidia wengine bila ya kutegemea kulipwa fedha hizo. Kwa sababu tunatoshelezwa zaidi na utoaji kuliko upokeaji.
Pia unapotoa fedha kwa wengine, unatengeneza pengo ambalo itabidi lizibwe, hivyo unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kuongeza kipato chako zaidi.
Tano; kiwango cha utoshelevu.
Hiki ni kiwango ambacho kinajumuisha viwango vyote vinne hapo juu. Ni kiwango ambacho kinapima afya yako ya kifedha na kwa kiasi gani umetosheka na kiasi cha fedha unachopata na ulichonacho.
Japokuwa hupaswi kukaa na kujiambia umeshafika kilele cha kifedha na huna haja ya kutafuta tena, unapaswa kuwa na utoshelevu, ambao unakufanya uyafurahie maisha yako. Utaendelea kuweka juhudi ili kuboresha zaidi hali yako ya kifedha, lakini hilo halikufanyi ujione kila wakati hujakamilika.
Fanya tathmini ya kifedha kwenye maisha yako, jipime kwenye kila kiwango katika viwango hivyo vitano kisha angalia ni kiwango kipi ambacho wewe upo. Angalia ni hatua zipi umepiga au kushindwa kupiga kifedha kwenye maisha yako na anza kuchukua hatua mara moja.
Kama umekwama kifedha, nina zawadi nzuri kwako ya mafunzo ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Haya ni mafunzo ya kila unachopaswa kujua kuhusu fedha, utaweza kuyapata kwa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Tuma ujumbe kwenye wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapewa maelekezo ya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL