Mpendwa rafiki yangu,

Kwa dunia ya sasa natumaini kila mtu ana akaunti yake, tuna akaunti nyingi sana ambazo tumezifungua kwa ajili ya masuala ya kibeki yanayohusiana na fedha zetu. Akaunti za siku hizi tunatembea nazo na kila mtu anatembea na akaunti yake mkononi. Ni kweli tuko katika zama za taarifa kwa sababu kila kitu tunakipata kupitia taarifa, dunia imevutwa machoni sasa, hata ukiwakuta watu wengi siku hizi ni kutolea tu macho simu zao.

Licha ya kuwa na akaunti nyingi za kifedha bado tatizo la nidhamu ya fedha ni shida kwa watu wengi. Tukiweza kuwa na nidhamu ya fedha tutaweza kutawala fedha zetu vizuri na hata kupunguza matatizo mengi ya kifedha.

Shabaha yangu wala siyo kuzungumzia akaunti ya fedha kama ulivyojiandaa kujua. Shabaha yangu kubwa leo ni kuzungumzia akaunti bora kuliko zote. Akaunti bora kuliko zote ndiyo akaunti gani?

Kusoma

Wengi tuna akaunti za kibenki lakini kuna akaunti ambayo ni muhimu kuliko zote ambayo ni akaunti ya mawazo. Akaunti ya mawazo ni bora kuliko akaunti za benki, watu wana akaunti za kibenki lakini hawana akaunti za mawazo na mtu mwenyewe akaunti ya mawazo huwa ndiyo tajiri na ukiwa na akaunti ya mawazo fedha zitakuja zenyewe bila hata shida.

SOMA; Viwango Vitano Vya Kupima Afya Yako Kifedha Na Kuweza Kujua Hatua Ulizopiga Kifedha.

Mawazo ndiyo baba wa vitu vyote tunavyoviona leo hii duniani.  Dunia inakuwa bora kwa sababu ya mawazo yetu na mawazo yetu ndiyo yanazalisha fedha na tukiwa na fedha tutakuwa na akaunti nyingi za kibenki. Watu wana akaunti za kibenki lakini cha ajabu hana hata akaunti ya mawazo, hana kijidaftari kidogo kwa ajili ya kuandika mawazo mazuri yanayomjia katika akili yake.

Unatakiwa uwe na akaunti ya mawazo yaani bank ideas. Unapokuwa na akaunti hii inakusaidia sana kuzalisha mawazo mazuri yatakayokupelekea kwenye uhuru wa kifedha. Mtu ambaye hathamini mawazo yake hana tofauti na mnyama kama vile ng’ombe. Wewe ni binadamu una akili na mawazo yako ndiyo yatakayoweza kukufanya uwe masikini au tajiri na siyo kitu kingine.

Fedha ulizonazo ni matokeo ya mawazo uliyofanyia kazi, sasa kama huna mawazo ya kukupa fedha utazipataje hizo fedha?

Hatua ya kuchukua leo; kuwa na akaunti ya mawazo (ideas) ni akaunti bora kuliko hata akaunti ya kibenki. Ukiwa na mawazo bora ukayafanyia kazi utakuwa vile unavyotaka kuwa.

Hivyo basi, fedha inatusaidia kuishi maisha tunayotaka, fedha inakuja kwa njia ya mawazo bora kama huna mawazo ya kuzalisha fedha ni bora usiwe na akaunti ya kibenki.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana!