Rafiki yangu mpendwa, juma namba 41 kwa mwaka huu 2018 hatunalo tena, linaisha kama lilivyoanza. Na kadiri majuma yanavyoisha, ndivyo mwaka unavyokatika na ndivyo siku zetu za kuwa hapa duniani zinavyozidi kupungua.
Kwa kuwa tunajua ni kwa jinsi gani muda wetu ulivyo na ukomo hapa duniani, tunapaswa kuweka kipaumbele kikubwa sana kwenye muda wetu. Tusipoteze hata dakika yetu moja kwa mambo ambayo hayana uhusiano na kile tunachofanya na hayachangii kufikia mafanikio makubwa tunayopigania.
Muda ni zaidi ya fedha, poteza milioni unaweza kupata nyingine, lakini poteza dakika yako moja na huwezi kuipata tena, ndiyo imetoka moja kwa moja. Hivyo rafiki, kama kuna kitu unapaswa kuwa na ubahili mkubwa nacho ni muda wako. Lakini cha kushangaza, wengi wana ubahili wa fedha, lakini wanapoteza muda wao kwa watu na vitu visivyokuwa na mchango kwao, kama kufuatilia habari mbalimbali na hata kufuatilia maisha ya wengine.
Rafiki, karibu kwenye tano za juma, nimeanza na hili la muda kwa sababu kila mtu anatamani kupata muda zaidi. Na wote tunajua, muda hautaongezeka, ila kila mtu anaweza kutengeneza muda zaidi kwa kuacha yale ambayo siyo muhimu.
Tano za juma hili nimekuandalia vitu muhimu sana vya kwenda kufanyia kazi kwa ajili ya mafanikio yako makubwa. Karibu usome, utafakari kwa kina, uweke kwenye mipango yako ya juma linalokwenda kuanza na kisha uchukue hatua mara moja.
#1 KITABU NILICHOSOMA; KANUNI TANO ZA MAFANIKIO MAKUBWA SANA.
Moja kati ya vitabu nilivyosoma juma hili ni kitabu kinachoitwa GO-GIVER kilichoandikwa na Bob Burg na John David.
Ni kitabu ambacho kinaelezea hadithi fupi, lakini yenye mafunzo makubwa sana kuhusu mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Kwenye kitabu hichi tunapewa hadithi ya kijana aitwaye Joe, alikuwa mpambanaji hasa, kwa jina jingine GO- GETTER. Hakukubali kushindwa na chochote, lakini alifika mahali na kujikuta anakwama. Licha ya kuweka juhudi kubwa, hakuweza kupata kile alichokuwa anataka.
Na hapo ndipo alipoomba ushauri kwa mfanyakazi mwenzake, ambaye alikuwa ana sifa ya kutokuonekana akifanya kazi sana, lakini alilipwa zaidi ya wengine. Wengi walizusha maneno kwamba alikuwa anapendelewa au analipwa kwa sababu ya kazi kubwa alizofanya huko nyuma. Lakini Joe alijua kuna kitu kinamfanya alipwe zaidi.
Alimwomba ushauri kuhusu hali yake ya kukwama na kukumbuka aliwahi kumwambia kuhusu mtu anayetoa mafunzo ya mafanikio. Hakuwa akiamini sana watu wanaotoa mafunzo ya mafanikio, lakini kwa kuwa alikuwa amekwama, aliona hakuna ubaya kujaribu.
Basi aliunganishwa na mwalimu wake wa mafanikio makubwa, na alimpa kanuni tano za kuweza kufikia mafanikio makubwa. Mwalimu huyo alimpa sharti moja, kwamba lazima aifanyie kazi kila kanuni anayojifunza, siku hiyo hiyo. Na kulikuwa na mkutano wa kila siku muda wa chakula, ambapo kila siku alijifunza kanuni moja kwa kumtembelea mtu aliyefanikiwa sana kwa kutumia kanuni hiyo.
Joe alikubali sharti hilo na kuanza darasa lake la siku tano, darasa la kujifunza na kufanyia kazi kile ambacho amejifunza siku hiyo hiyo, hata kama ni kidogo kiasi gani.
Na zifuatazo ni kanuni tano za mafanikio makubwa ambazo Joe alifundishwa, zisome na uzitumie kwako pia.
KANUNI YA KWANZA; THAMANI.
Kanuni ya kwanza ya mafanikio makubwa inasema; kiwango chako cha utajiri kinatokana na thamani kubwa unayotoa kuliko malipo unayopokea.
Hii ni kanuni muhimu sana kwenye mafanikio yoyote yale, unapaswa kutoa thamani kubwa kuliko malipo unayopokea. Hii ndiyo njia pekee itakayowafanya watu wawe tayari kufanya kazi na wewe kwa sababu wanajua watapata zaidi.
Na hakuna kipindi ambacho kanuni hii inaweza kukusaidia kama kipindi hichi ambacho kila mtu anakazana kufanya kidogo na kutegemea kulipwa zaidi. Wewe ukifanya zaidi, iwe ni kwenye kazi au bishara yako, ukitoa thamani zaidi ya unavyolipwa, utafika hatua utalipwa kuliko unavyofanya.
Unapaswa kuwa mtu wa kutoa zaidi, kuliko kuwa mtu wa kutegemea kupokea tu. Na kadiri unavyotoa, ndivyo utakavyopata zaidi. Na usifanye makosa ya kutoa kwa sababu unategemea kupokea, wewe toa, na kupokea kutafanya kazi kwenyewe.
KANUNI YA PILI; FIDIA.
Kanuni ya pili ya mafanikio makubwa inasema; kipato chako ni matokeo ya idadi ya watu unaowahudumia na kwa ubora kiasi gani unawahudumia. Kwa maneno mengine, kipato chako kinalingana na idadi ya maisha unayoyagusa.
Hii ni kanuni nyingine muhimu sana kwenye mafanikio yako, kanuni ambayo inaondoa ukomo kwenye kipato chako na hata mafanikio yako. Kwa sababu kama inavyosema, ukomo pekee ni idadi ya watu unaowahudumia na ubora wa huduma zako.
Hii ina maana kwamba kama kipato chako ni kidogo, unawahudumia watu wachache au unawapa huduma ambayo siyo bora. Hivyo basi, kuongeza kipato chako, kwa hapo hapo ulipo, bila ya kubadili unachofanya, badili vitu viwili tu; ongeza idadi ya watu unaowahudumia na ongeza ubora wa huduma unazotoa.
Je unafikiri hilo linakuhitaji uwe mtu wa tofauti na ulivyo sasa? Unafikiri linahitaji uwe na mtaji zaidi au uwe na elimu zaidi? Majibu ni hapana. Ongeza mteja mmoja leo, ongeza ubora wa huduma zako na utaona jinsi ambavyo wengi zaidi wanakuwa tayari kukulipa. Na hata kwa wale walioajiriwa, ongeza ubora wa huduma zako, fanya kile unachofanya kwa namna ambayo hakuna mwingine anafanya, na kwa hakika kipato chako kitaongezeka, kama siyo hapo ulipoajiriwa sasa, basi nje ya hapo.
KANUNI YA TATU; USHAWISHI.
Kanuni ya tatu ya mafanikio makubwa inasema; ushawishi wako ni matokeo ya jinsi gani unaweka mbele maslahi ya wengine kabla ya maslahi yako. Hii ni kanuni inayohusu mtandao wako, wale watu wanaojua kuhusu wewe, wanaokuamini na ambao wanapenda kukuona wewe unafanikiwa. Hawa ni watu ambao watakutetea kwa lolote na kwa yeyote.
Kadiri unavyokuwa na ushawishi mkubwa, kadiri mtandao wako unavyokua, ndivyo mafanikio yako yanavyokuwa makubwa. Na njia pekee ya kukuza mtandao wako na kuongeza ushawishi wako, ni kuweka mbele maslahi ya wengine, kabla ya maslahi yako binafsi. Jukumu lako linapaswa kuhakikisha wengine wanapata kile wanachotaka, na wao wakishapata, hakika na wewe utapata kile unachotaka.
Mwandishi anasema kanuni ya win-win au 50-50 huwa haifanyi kazi kwenye mafanikio makubwa. Kanuni ya mafanikio makubwa ni kumfanya mwingine ashinde kadiri anavyotaka kushinda, kumfanya mwingine apate kwa asilimia 100 na siyo asilimia 50. Anasema wewe usijali unapata nini, jali kwanza wengine wanapata nini, na kwa hakika utapata unachotaka.
Na kanuni hii nimeielewa sana kwa sababu inaendana na msingi ninaoishi wa KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA, WAWEZESHE WENGINE KUPATA KILE WANACHOTAKA. Kuna uboreshaji mkubwa sana ninaokwenda kufanya kwenye huduma zangu, kuhakikisha napeleka nguvu zangu zote kuwafanya watu wapate kile wanachotaka, ili na mimi nipate ninachotaka.
KANUNI YA NNE; UHALISI.
Kanuni ya nne ya mafanikio makubwa inasema; zawadi ya thamani uliyonayo unayoweza kuwapa wengine ni wewe mwenyewe. Hii ni kanuni ya kuwa halisi, kuishi uhalisia wako. Kujua asili yako na kuiishi, kujua uwezo wako mkubwa na kuutumia. Kuacha kuigiza maisha ya wengine na kuishi maisha halisi kwako na kwa njia hii watu watanufaika sana.
Kwenye chochote kile unachofanya kwenye maisha yako, kifanye kama wewe, weka utu wako ndani yake. Na hata kama kila mtu anafanya, hata kama huna cha tofauti cha kufanya, kifanye kama wewe, na utaweza kujitofautisha na kuwanufaisha wengine pia. Yaani hapa ni kama unauza soda ambazo huna cha kuongeza na umezungukwa na wengine wanaouza soda pia, wote bei zinafanana, kitakachokutofautisha wewe ni kuuza soda kama wewe, kuweka utu wako kwenye biashara yako.
Usijiambie biashara au kazi unayofanya haina cha kukutofautisha, wewe ndiye kitu pekee cha kukutofautisha, usikazane kushindana na yeyote, kazana kuwa wewe, na watu watakupokea wewe na watakuwa tayari kufanya kazi na wewe.
KANUNI YA TANO; UPOKEAJI.
Kanuni ya tano ya mafanikio makubwa inasema; ufunguo wa utoaji sahihi ni kuwa tayari kupokea. Hii ni kanuni ya kukufanya wewe uwe mpokeaji mzuri, uwe tayari kupokea na ushukuru kwa kupokea.
Wapo watu ambao wapo tayari kutoa, lakini hawapo tayari kupokea. Wanaona kupokea ni kama kutengeneza deni, kuwa tegemezi au kuonekana una uhitaji sana.
Lakini ukweli ni kwamba unapaswa kuwa tayari kupokea kama ambavyo unatoa. Na usikatae chochote kinachokuja kwako. Pia kuwa mtu wa shukrani kwa chochote unachopokea, iwe ni kidogo au kikubwa. Usizie kupokea, kuwa tayari kupokea na mafanikio makubwa sana yatakuja kwako.
Rafiki, hizo ndiyo kanuni tano za mafanikio makubwa sana.
NIAHIDI KITU KIMOJA.
Rafiki, naomba uniahidi kitu kimoja, niahidi kwamba utakwenda kufanyia kazi kanuni hizi kwenye kila eneo la maisha yako kuanzia leo. Kwanza kabisa ziandike kanuni hizi na kisha jikumbushe kila unapoianza siku yako.
Kisha kwenye kila siku yako, angalia fursa za kutumia kanuni hizi.
Kila siku angalia fursa ya kutoa thamani zaidi, na hizi zipo kila mahali. Angalia fursa ya kutoa huduma bora sana na kwa wengi. Angalia fursa ya kuweka mbele maslahi ya wengine kabla ya maslahi yako. kila siku kazana kuwa wewe, ishi uhalisia wako na usiige au kushindana na yeyote. Na kila siku, kuwa tayari kupokea na shukuru kwa kila unachopokea.
Rafiki, najua hakuna ugumu wowote kwenye kuishi kanuni hizi tano, ni wewe uamue na kisha uanze kuvuna matunda, ya mafanikio makubwa sana.
Niahidi kuishi kanuni hizi, na kila matokeo unayoyapata, nitumie kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz naahidi nitasoma email yako na hata kukushauri zaidi pale unapohitaji hivyo, kwa sababu nimeweka maslahi yako mbele kuliko chochote kingine kwangu.
#2 MAKALA YA WIKI; PIMA AFYA YAKO KIFEDHA.
Rafiki, watu wengi kwenye fedha wamekuwa wanaenda kimazoea, hivyo hawajui afya zao kifedha zipoje. Ni mpaka pale wanapojikuta kwenye ugonjwa kifedha, labda madeni au kuishiwa kabisa, ndiyo wanashtuka. Kumbe kuna dalili zilikuwepo kwa muda mrefu ila wao hawakuziona kwa sababu walikuwa hawapimi afya yao kifedha.
Juma hili nilikuandikia makala yenye viwango vitano vya kupima afya yako kifedha. Ni makala muhimu sana ya kusoma ili kuepuka kuanguka kifedha. Kama hukusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Viwango Vitano Vya Kupima Afya Yako Kifedha Na Kuweza Kujua Hatua Ulizopiga Kifedha.
Pia juma hili nilikuandikia makala kuhusu kitu kimoja kitakachokuwezesha kuuza zaidi hata kama unajiambia wewe siyo muuzaji mzuri. Kisome hapa; Kitu Hichi Kimoja Kitakuwezesha Kuuza Zaidi Kwenye Biashara Yako Hata Kama Wewe Siyo Muuzaji Mzuri.
#3 TUONGEE PESA; WASAIDIE WENGINE KUPATA FEDHA ZAIDI.
Rafiki, makosa makubwa sana ambayo wengi wanayafanya kwenye kutaka kupata fedha zaidi, ni kuangalia ni fedha za nani wanaweza kuzichukua. Ndiyo maana tumekuwa na wezi, matapeli na hata wapokeaji wa rushwa, kwa sababu msingi wao kuhusu fedha ni kwamba ili upate fedha, lazima uzichukue kwa wengine.
Sasa nataka nikupe msingi wa tofauti, msingi ambao utakuwezesha kupata fedha zaidi, huku sifa yako ikiwa nzuri na usiwe na hofu ya kupoteza fedha ulizopata.
Msingi huu; kila unapokuwa unahitaji kupata fedha zaidi, jiulize swali hili, ni mtu gani naweza kumsaidia apate fedha zaidi? Ukipata jibu, hapo ndipo unapoweza kupata fedha zaidi.
Ninachomaanisha ni kwamba, utaweza kupata fedha zaidi pale tu utakapomwezesha mtu mwingine kupata fedha zaidi.
Hivyo anza kwa kuangalia kazi unayofanya au biashara unayofanya, na jiulize ni kwa namna gani huduma unayotoa, au bidhaa unayouza, inamwezesha mtu kupata fedha zaidi? Angalia kile unachotoa au kuuza, kinamwezeshaje mtu asipoteze fedha zaidi au aongeze kipato chake zaidi. Na ukishawajua unaowahudumia, wape huduma nzuri sana na kipato chako kitaongezeka.
Acha sasa kuangalia fedha kwa mtazamo wa pata potea, balia angalia fedha kwa mtazamo wa kila mtu kupata. Na hili linawezekana kwa kila mtu, wewe angalia tu nani anayetegemea kile unachofanya, kisha mpatie kwa ubora wa juu zaidi, unaomfanya asipoteze fedha nyingi au aongeze kipato chake, na kwa hakika kipato chako kitaongezeka.
#4 HUDUMA NINAZOTOA; SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
Rafiki, tunakaribia kabisa kwenye ile siku kubwa kabisa na ya kipekee kwa mwaka huu 2018, siku ambavyo tunakwenda kukutana kwa pamoja na kuweka mipango na mikakati ya mwaka mmoja unaokuja, ili tuweze kupiga hatua kubwa zaidi.
Siku ninayoizungumzia hapa ni SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ambayo mwaka huu itafanyika tarehe 03/11/2018. Ada ya kushiriki semina ya mwaka huu ni tsh laki moja (100,000/=) ambayo itahusisha mambo yote ya siku nzima ya semina mpaka vyakula vya siku nzima.
Rafiki, mwisho wa kulipa ada ili kushiriki semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018 ni tarehe 31/10/2018, hivyo chukua hatua ili usikose nafasi hii. Pia nafasi za kushiriki semina hii ni chache, hivyo kama unatarajia kushiriki, tuma majina yako na namba ya simu kwenda namba 0717 396 253 leo hii ili ujihakikishie nafasi ya kushiriki.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; JIULIZE SWALI HILI MARA TATU KWA SIKU.
“At least three times every day take a moment and ask yourself what is really important. Have the wisdom and the courage to build your life around your answer.” – Lee Jampolsky
Angalau mara tatu kwa siku, jiulize swali hili, ni kitu gani muhimu zaidi kwako. Kuwa na hekima na ujasiri wa kuyatengeneza maisha yako kwenye jibu hilo.
Rafiki, huwa tunapanga mambo mengi makubwa, huwa tunapangilia miaka yetu, miezi yetu, wiki zetu na hata siku zetu. Lakini siku inaisha na huoni umefanya nini, wiki inaisha huoni kikubwa ulichofanya, mwezi unaisha na unajiuliza mbona siku zinaenda sana. Mwaka unamalizika na unajiuliza mwaka wako umepotelea wapi.
Yote haya ni kwa sababu hupati nafasi ya kujiuliza swali la kipi ni muhimu sana kwako, hivyo unapokea yale ambayo dunia inakuambia ni muhimu, ambayo kwako hayawezi kukuambia ni muhimu.
Mfano, unaweza kuwa umeianza siku yako kwa mipango yako, lakini kabla hata muda haujaenda, unasikia kuna habari mpasuko, kitu fulani kimetokea, unajikuta unaanza kufuatilia habari baada ya habari, kutaka kujua kwa undani, na kuingia kwenye mijadala ya habari hiyo ambayo dunia inakuambia ni muhimu. Hapo unasahau yale ambayo ni muhimu kwako, siku inaisha na hujafanya chochote kikubwa.
Lee, niliyemnukuu hapo juu anatuambia tujiulize swali hili mara tatu kwa siku, lakini mimi nataka nikushauri tofauti, nakuambia ujiulize swali hili kila baada ya saa moja. Ikiwezekana weka alamu kwenye saa au simu yako, na kila saa inapoisha, weka kikubusho cha kujiuliza swali hilo. Hii itakusaidia kujikamata pale unapokuwa umeondoka kwenye yale muhimu.
Mfano umeianza siku yako na ratiba zako, kwenye muda fulani ukawa umeingia kwenye mitandao ya kijamii. Ukiwa kwenye mitandao hiyo unapaswa kujiuliza kipi muhimu zaidi kwenye maisha yako? je matumizi hayo ya mitandao ya kijamii kwa muda huo ndiyo kitu muhimu na bora kabisa unachopaswa kufanya na muda wako kwa wakati huo? Kama jibu ni hapana, fanya kilicho sahihi, maana unajua kipi sahihi.
Rafiki, nimekupa mengi ya kufanyia kazi kwa juma unalokwenda kuanza, niahidi kile nilichokuomba uniahidi na nimejitoa kukufuatilia kwa karibu mpaka uweze kufanikiwa. Maana najua mafanikio yangu ni mafanikio yako, kama wewe hutafanikiwa, mimi pia sitaweza kufanikiwa.
Muhimu zaidi, kama bado hujadhibitisha kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, fanya hivyo siku hii ya leo, yapo mengi sana kwa mafanikio yako kwenye semina hii, usipange kuikosa kwa namna yoyote ile.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu