Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo kwenye safari yetu ya mafanikio.
Katika makala ya leo, tunakwenda kushauriana njia bora za kukabiliana na wateja wasumbufu kwenye biashara ya mikopo midogo midogo.
Biashara ya fedha ni moja ya biashara zenye faida nzuri na uhakika, lakini pia ni biashara zenye changamoto kubwa kwa upande wa wateja. Watu wengi wamekuwa wanaona upande mmoja wa faida wanayoweza kupata kwenye biashara hii na kuingia bila ya kuangalia upande wa pili wa changamoto.
Changamoto kubwa ambayo imekuwa inawapelekea wengi kushindwa kwenye biashara hii ni watu kutokurudisha mikopo ambayo wanachukua. Na hata kama watu wameweka dhamana, bado kitendo cha wao kutokurudisha fedha au kuchelewa kurudisha kutakupa wewe usumbufu mkubwa.
Leo tunakwenda kushirikishana mbinu za kuondokana na changamoto hii ya wateja wasumbufu kwenye biashara ya fedha. Kabla hatujaangalia hatua za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;
Nilianzisha biashara ya mikopo midogo midogo ya dharura kwa watumishi wa serikali ambayo hurejeshwa punde tu mshahara unapotoka ikiwa ni mkopo na faida ambayo niliweka interest ya 25% na mwanzo ilinifanikisha sana nilikua natoa 50000/=,mpaka laki 5 kwa mteja mmoja na zote zilikua zinarudi (mwaka 2015),kwa mwezi faida ilikua inapatikana mpaka milioni mbili na ikaniwezesha kufungua biashara nyingine. Malengo ilikua ni kuisajili kabisa pakishakua na kutanuka zaidi kibiashara. Leo hii imeniingiza kwenye madeni na migogoro na watu kwani mauzo yamekua madogo na usumbufu umekua mkubwa baina ya wateja wanaopatiwa huduma. Tafadhali naomba ushauri. – Honest E. L.
Kama ambavyo rafiki yetu Honest ametuandikia hapo, changamoto ya wateja kutokurudisha fedha ni kubwa na kwa wengi wanaofanya biashara hii ya fedha.
Ili kukabiliana na changamoto hii, fanyia kazi ambo haya matano muhimu sana.
Moja; elewa wanaohitaji mkopo wana uzembe kwenye fedha.
Huwezi kutatua tatizo kama bado hujalijua, na kwenye biashara ya mikopo midogo midogo na ya muda mfupi, unapaswa kuujua ukweli huu. Kwamba yule anayetaka huduma kwako ana uzembe kwenye fedha. Kwa sababu kama angekuwa na mipango mizuri kifedha, asingehitaji kukopa fedha.
Na najua unaweza kusema mtu anaweza kuwa amepata dharura, na ndiyo, dharura ni sehemu ya uzembe pia. Kama mtu angekuwa makini na fedha zake, akajiwekea akiba ya dharura, asingejikuta kwenye dharura inayomtaka kukopa.
Hivyo elewa kwamba wateja wako ni watu ambao ni wazembe kwenye fedha zao binafsi, na hivyo hakikisha uzembe wao hauingii kwenye fedha zako pia.
Mbili; chuja sana wateja wako.
Kitu kimoja ambacho kila mfanyabiashara anapaswa kujua ni kwamba, siyo lazima ufanye kazi na kila mteja anayetaka huduma kwako. Maana wafanyabiashara wengi wamejiweka kama sheria kwamba kila anayekuja lazima apate huduma.
Ukitoa huduma kwa kila anayetaka kwenye biashara ya fedha, utatengeneza madeni mabaya sana ambayo hayalipiki. Kwa sababu hakuna asiyependa fedha, na watu wakijua wanaweza kupata fedha kirahisi kwako, basi wataambiana na kuja kuzipata. Hivyo siyo tu unatengeneza matatizo kwako, bali pia unawatengenezea wateja wako matatizo, kwa kuwapa fedha kizembe nao wanazitumia kizembe.
Tatu; weka vigezo vya mtu kupata mkopo na usipindishe hata kimoja.
Angalia mikopo yote ambayo inakusumbua sana, utagundua kuna vigezo hukufuata. Mtu anakuja kwako ana shida kweli, lakini hakidhi vigezo vya kupata mkopo, anakulilia kwa shida yake, unaingia huruma na kumpa mkopo. Akishachukua mkopo ndiyo unaijua rangi yake halisi, anakusumbua mpaka unajisikia vibaya kwa nini ulimwamini.
Unapofanya biashara ya mikopo, unapaswa kuweka hisia pembeni na kusimamia taratibu ulizojiwekea. Kama mtu hana vigezo vya kupata mkopo usimpe mkopo, hata kama ana shida kiasi gani. Kama unataka kumsaidia msaidie kwa fedha zako binafsi lakini siyo kwa fedha za biashara.
Na kumbuka namba moja hapo juu, unapomwona mtu yupo kwenye matatizo ya kifedha, jua kuna uzembe amefanya kwenye maisha yake, sasa ukiingia kwa huruma, unakwenda kununua uzembe huo na utakusumbua sana wewe.
Kuwa na msimamo kama benki zilivyo na misimamo kwenye utoaji wa mikopo, kama mtu hakidhi vigezo hapati mkopo.
Nne; dhamana anayoweka mtu inapaswa kuwa kubwa sana kuliko mkopo anaochukua.
Kitu kimoja unachopaswa kujua kwenye biashara ya mikopo ni kwamba, wewe upo kwenye biashara ya fedha, na siyo biashara ya kuchukua mali za watu na kuziuza ili kufidia fedha zako. Hivyo unapaswa kuepuka sana kufika kwenye hatua ambayo inabidi uchukue mali kufidia mkopo wako, kwa sababu inakutoa kwenye biashara yako na inakuwa kazi kwako zaidi.
Ili kuepuka hilo la kubaki na amana wanazoweka watu, unapaswa kuchukua dhamana ambayo ina thamani kubwa sana kuliko mkopo ambao mtu anachukua, ikiwezekana mara mbili ya mkopo husika. Lengo siyo wewe unufaike, bali lengo ni kumsukuma mteja kurudisha fedha aliyokopa ili asipoteze mali yake.
Kama utachukua dhamana inayolingana na mkopo mtu aliochukua, hataona shida ya kukuachia dhamana hiyo na kutorudisha mkopo aliochukua. Hivyo kuwa makini sana eneo hili.
Tano; yafanye maisha ya wale unaowadai kuwa magumu.
Udhaifu mmoja ambao nimekuwa nauona kwa wengi wanaofanya biashara ya mikopo midogo midogo ni kuogopa kuwadai wale ambao hawarudishi mikopo kwa wakati. Ninaposema kuogopa kuwadai simaanishi hawawadai kabisa, ila wanawadai kwa woga sana, ni kama wanawabembeleza hivi. Sasa kwa njia hiyo huwezi kurudisha fedha zako, hasa pale mteja anapokuwa ameamua kukusumbua.
Badala yake unapaswa kudai kwa nguvu zaidi na kwa kufuatilia zaidi. Unapaswa kumdai mteja kwa kiasi ambacho ataona wewe ni msumbufu na njia pekee ya kuachana na wewe ni kukulipa fedha zako. Yafanye maisha yake kuwa magumu hasa.
Na hapa simaanishi umtukane mteja au kumtishia, badala yake kufuata ahadi zake kama anavyoweka.
Mfano kama mteja ameshindwa kulipa kwenye tarehe aliyoahidi, wasiliana naye na muulize kwa nini hajalipa. Kisha akupe tarehe nyingine ya uhakika ambayo atalipa. Tarehe hiyo ikifika kama hajalipa mtafute kabisa na akueleze kwa nini halipi, na aweke kwenye maandishi kabisa kwamba atalipa kwa mpango gani. Kisha endelea kumfuatilia hivyo bila ya kuchoka, mpaka yeye mwenyewe akuchoke, aone njia pekee ya kuondokana na wewe ni kukulipa fedha yako. Kwa ustaarabu kabisa unaweza kuyafanya maisha ya mteja wako kuwa magumu mpaka akalazimika kukulipa deni unalomdai.
Rafiki, fanyia kazi mambo haya matano na utaweza kuchagua wateja bora wa kufanya nao kazi na pia kukusanya madeni kutoka kwa wateja wasumbufu.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog