If you desire to be good, begin by believing that you are wicked. – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu, nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuishi kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana.
Kwa mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA mwaka huu 2018 utaendelea kuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUJIFUNZA UNACHOJUA…
Sababu kubwa ambayo inawazuia watu kujifunza mambo mapya na mazuri kwao, ni kwa sababu wanaamini tayari wanajua kila kitu.
Ni vigumu sana KUJIFUNZA KITU AMBACHO TAYARI UNAAMINI UNAKIJUA.

Kadhalika kwenye kuwa mtu mwema, huwezi kuwa mwema kwa kuamini kwamba tayari wewe ni mwema. Bali unakuwa mwema kwa kuamini wewe ni muovu.

Huwezi kupata kitu ambacho tayari unaamini unacho, utapata kile ambacho huna, ambacho utachukua muda wako kukifanyia kazi ili kukipata.

Kwa haya tunaweza kusema kwamba chochote tunachotaka kuboresha kwenye maisha yetu, lazima tukubali kwamba tupo hovyo, lazima tukubali kwamba hatujawa bora bado.
Hii ndiyo inatupa nafasi na hata hamasa ya kupiga hatua zaidi.

Lakini kama utakuwa na mtazamo wa kwamba unajua kila kitu, umekamilika na una kila unachotaka, utafunga milango na hutaweza kupata zaidi.
Lakini pia hii haimaanishi usiridhike na chochote ulichonacho, ridhika, lakini jua kuna hatua za kupiga zaidi.

Ukawe na siku bora sana leo, siku ya kujifunza na siku ya kujiboresha zaidi ya ulivyokuwa jana.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha