It is not death or pain that is to be dreaded, but the fear of pain or death. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa mafanikio kwa mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kupiga hatua zaidi.
Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOUMIZA ZAIDI SIYO TUKIO BALI HOFU…
Watu wamekuwa wanaumia zaidi siyo kwa tukio fulani, bali kwa hofu ya tukio hilo kutokea.
Hofu inawafanya watu wanaumia mara nyingi kabla hata ya tukio wanalohofia halijatokea.
Mara nyingi hofu hukuza mambo na kuyafanya yaonekane ni makubwa na hayawezekani.
Kwa mfano kwenye kifo, kifo kinatokea mara moja na huenda tusijue hata wakati kinatokea. Lakini hofu ya kifo inaweza kukutesa na kukuumiza mara nyingi mno.
Kadhalika kwenye vitu kama kushindwa, mtu anaweza kuishi ma hofu hiyo ya kushindwa kwa muda mrefu kabla hata hajaanza kufanya kile ambacho anahofia kushindwa.
Dawa ya hofu hizi ni kujikumbusha usemi huu muhimu, nitavuka daraja nitakapolifikia.
Hata ulifikirie na kulihofia daraja kiasi gani, kama halipo mbele yako huna cha kufanya.
Hivyo subiri mpaka ulifikie daraja, na hapo ndipo utakapoweza kulivuka.
Mara zote unapokuwa na hofu, jikumbushe hilo muhimu, kwamba hofu hiyo haikisaidii chochote kama bado kitu hakijafanyika. Hivyo ni vyema kujiandaa vizuri ili tukio linapotokea uwe tayari, badala ya kuendelea na hofu ambayo haina maana.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha