Habari rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi nzuri tuliyoipata kwenye juma hili linalokwenda kuisha. Nina imani yapo makubwa uliyofanya juma hili, na mengi uliyojifunza pia. Kwa yale uliyoshindwa, nina imani umejifunza na utakuwa bora zaidi kwenye juma lijalo na siku zijazo pia.

Karibu kwenye makala yetu ya #TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya kuimaliza wiki yako. Mambo haya matano yanakusaidia kujifunza na hata kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Karibu ujifunze na upange hatua za kuchukua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi kupitia mambo haya matano ya juma hili la sita la mwaka huu 2018.

#NENO; Njia rahisi ya kujua kama mtu anadanganya.

Ipo njia rahisi sana ya kujua kama mtu anadanganya, na njia hiyo ni kuuliza swali ambalo linahitaji jibu la moja kwa moja na la uhakika. Kama mtu ni mkweli na anaamini kile anachosema, basi atakupa jibu la moja kwa moja na la uhakika. Lakini ukianza kuona mtu anatoa maelezo mengi na hakuna jibu la uhakika, jua hapo kuna kudanganywa ndani yake.

Kwa mfano unamuuliza mtu jana ulikuwa saa saba mchana ulikuwa wapi? Yeye anaanza kukuambia ujue jana nilibanwa kweli, nilikuwa nimeenda … nikakuta… halafu… Angalia kwa makini, swali ni ulikuwa wapi, lakini majibu hayajibu wapi. Hapo mtu hana uhakika, hajui au anadanganya.

Ukitaka kupima hilo vizuri, angalia mwanasiasa anapoulizwa swali, iwe ni wananchi au hata kwenye mahojiano. Mfano anaulizwa, umeahidi kujenga barabara eneo fulani, ujenzi huo unaanza lini? Majibu utasikia yanaanza na pale upembuzi yakinifu utakapofanyika na mchakato wa kuwashirikisha wadau ukikamilika basi mradi utaanza mara moja. Ukiangalia hapo, swali halijajibiwa, lakini aliyepokea maelezo hayo ataridhika, halafu hatakuwa na kitu cha kumshika, kwa sababu hajaahidi tarehe kamili ya kuanza, na ameweka mambo mengi ambayo hujui yatakamilika lini. Hujui mchakato na upembuzi utakamilika lini na hivyo huwezi kumdai kwenye hilo.

Siyo lazima umwambie mtu anadanganya, lakini mbinu hii itakusaidia kuwa na imani na majibu ya watu au la. Na kwa upande wa pili, unapoulizwa kitu jibu, na kama kuna maelezo ya ziada yatoe baada ya kutoa jibu la uhakika. Usizunguke na maneno mengi, wanaoelewa watajua unadanganya na hawatakupa uzito kwenye kile unachosema au kuahidi.

#1; KITABU NILICHOSOMA; The craving mind.

Hichi ni kitabu ambacho kinaongelea sayansi ya uraibu au uteja kama wengi wanavyotumia. Kwa nini watu wanaendelea kutumia kitu ambacho kina madhara kwenye maisha yao, wanataka kuacha lakini wanashindwa?

Kitabu hichi kimeenda kwenye msingi wa ujengaji wa tabia yoyote ile, ambao unakuwa na hatua tatu, ambazo ni KICHOCHEO, TENDO NA ZAWADI.

Kunakuwa na kitu ambacho kinachochea tabia kufanyika, halafu kichocheo hicho kinamsukuma mtu kufanya TENDO fulani na mwishowe anapata zawadi.

Sasa ni hiyo zawadi ndiyo inamfanya mtu kuendelea kufanya kitendo kile zaidi na zaidi.

Kwa mfano, kwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, pombe au sigara, kichocheo kinaweza kuwa kujisikia vibaya, kuwa na msongo wa mawazo, kushindwa kitu fulani au hata kuwa na mgogoro na wengine. Hali hizo zinamchochea mtu kuondokana nazo kwa haraka.

Anaamua kutumia ulevi wake, labda madawa ya kulevya, pombe au sigara. Kwa kutumia ulevi huo, kwa muda anajisikia raha, anasahau kabisa yale yaliyokuwa yanamsumbua, na kwa muda anakuwa huru, bila ya usumbufu wowote kimawazo.

Sasa hili lingekuwa bora, kama hali hiyo ingedumu kwa muda wote wa matatizo ya mtu huyo. Lakini tatizo ni kwamba, hali hiyo inadumu kwa muda mfupi mno, haizidi masaa. Hivyo hali hiyo ikipita, mtu anarudi kwenye hali yake ya awali, tatizo liko pale pale, na hilo linamchochea kutumia zaidi. Anatumia tena, anajisikia vizuri kwa muda, lakini baada ya muda inaisha, matatizo yako pale pale, anasukumwa kutumia tena. Hivi ndivyo mtu anaishia kuvuta sigara 20 kwa siku, au kunywa pombe kila siku, au kutumia madawa ya kulevya kila mara.

Kwa mwenendo huo, inafika mahali sasa mwili hauwezi tena kufanya kawaida bila ya kile kilevi ambacho mtu amezoea, na hivyo akijaribu kuacha, anajisikia vibaya zaidi na hivyo kujikuta akilazimika kuendelea, licha ya kwamba kitu kina madhara kwake. Na hapo ndipo tunasema mtu huyo amekuwa mteja.

Sasa sisi tumezoea kwamba watu wanaweza kuwa na uraibu kwenye vilevi tu, lakini mwandishi ametuonesha kwa mifano ya tafiti aina nyingine za uraibu ambazo zinawasumbua wengi mno.

Aina hizo ni kama ifuatavyo;

Uraibu kwenye teknolojia, hasa mitandao ya kijamii.

Uraibu kwa mtu mwinyewe, yaani unakuwa mteja wa mawazo yako mwenyewe kiasi kwamba inakuzuia kuziona fursa zaidi.

Uraibu kwenye kelele, hasa kwenye matumizi ya simu, hizi simu janja aka smartphone.

Uraibu kwenye mapenzi.

Mwandishi pia ameelezea kemikali muhimu sana ambayo inahusika kwenye kutengeneza uraibu ambayo ni kemikali ya dopamine.

Mwisho kabisa mwandishi ameeleza njia za kuepuka kuingia kwenye uraibu na hata kujiondoa kwenye uraibu.

Na njia kuu ni kuwa na uwepo wa kiakili (mindfullness) kwenye kila hatua ya maisha yako. Pia kufanya tahajudi kunasaidia sana kuimarisha uwepo wa kiakili.

Siku zijazo nitaandika zaidi kuhusu uwepo kiakili (mindfullness) maana ni kitu ambacho kimekuwa changamoto kwa wengi. Kwa kifupi watu wanafanya mambo, au kuchukua hatua ambazo hawawezi kuelezea kwa nini wamefanya hivyo. Wanajikuta tu wameshafanya, sasa hili ni tatizo kubwa.

#2 MAKALA YA WIKI; Mitazamo ya kipato inayokurudisha nyuma.

Hivi umewahi kujiuliza inakuwaje mtu anafanya kazi miaka 40 lakini kila mwaka kipato chake kinakuwa kidogo, matumizi makubwa na madeni mengi? Licha ya uwepo wa fursa nyingi lakini bado wengi wanasumbuka sana kifedha? Jibu ni moja, mitazamo ambayo watu wanayo linapokuja swala la fedha, ni mitazamo mibovu ambayo haiwasaidii kabisa.

Kwenye makala ya wiki hii, nimeainisha mitazamo mitano kuhusu malipo ambayo inawafanya watu wengi kuwa na kipato kidogo licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu. Pia nimeeleza hatua tano za kuchukua ili mtu kuweza kuongeza kipato chake maradufu. Kama ulisoma makala hii chukua hatua, kama hukupata nafasi ya kuisoma, isome hapa; Mitazamo Hii Mitano (05) Kuhusu Kipato Ndiyo Inakufanya Uingie Kwenye Matatizo Ya Kifedha, Ijue Na Hatua Za Kuchukua Ili Kuondoka Kwenye Umasikini. (https://amkamtanzania.com/2018/02/09/mitazamo-hii-mitano-05-kuhusu-kipato-ndiyo-inakufanya-uingie-kwenye-matatizo-ya-kifedha-ijue-na-hatua-za-kuchukua-ili-kuondoka-kwenye-umasikini/ )

#3 NILICHOJIFUNZA WIKI HII; Mpangilio mzuri wa muda wako, usijionee huruma.

Wiki hii nilisoma makala moja ya mwandishi Carl Newport, ambaye ni mmoja wa waandishi ambao wanaandika sana kuhusu matumizi bora ya muda, kuongeza uzalishaji binafsi na kuepuka usumbufu na mitandao ya kijamii.

Kwenye makala niliyosoma, ametushirikisha barua ambayo baba aliandika kwa mtoto wake kuhusu matumizi ya muda wake.

Baba huyo ni Alexander Hamilton ambaye ni mmoja wa waasisi  wa taifa la marekani, na barua aliiandika kwa mtoto wake Philip Hamilton ambaye alikuwa amehitimu mafunzo ya sheria na kuanza kufanya kazi. Barua hiyo aliyoandika mwaka 1800 aliita Rules for Mr. Philip na iliainisha matumizi ya muda wake kwa mwaka mzima.

Kwenye barua hii aliainisha yafuatayo;

Kwa kipindi cha tarehe moja April mpaka tarehe moja Oktoba, anapaswa kuamka kabla ya saa kumi na mbili asubuhi, kipindi kingine cha mwaka aamke kabla ya saa moja asubuhi. Anaweza kuamka kabla ya muda huo, lakini siyo baada ya muda huo. Muda wa kulala ni saa nne usiku, kila siku kwa mwaka mzima.

Baada ya kujiandaa asubuhi, anapaswa kusoma sheria mpaka saa tatu kamili asubuhi.

Kuanzia saa tatu asubuhi mpaka muda wa chakula cha mchana, ataenda ofisini ambapo ataandika na kuendelea na kusoma sheria.

Baada ya chakula, ataendelea kusoma sheria mpaka saa kumi na moja jioni. Saa kumi na moja jioni mpaka saa moja usiku utakuwa muda wa kufanya chochote anachojisikia kufanya. Na saa moja usiku mpaka saa nne atasoma chochote kinachompendeza kufanya.

Jumamosi kuanzia saa sita mchana, ana uhuru wa kufanya chochote anachotaka.

Jumapili atahudhuria ibada ya asubuhi, na baada ya hapo atapumzika apendavyo.

Barua inamaliza kwa kusema, hataruhusiwa kutengua ratiba hii bila ya kuomba ruhusa.

Kuna kitu kikubwa sana cha kujifunza kwenye barua hii ya ratiba ya matumizi ya muda, japo iliandikwa mwaka 1800, lakini mtu unaweza kutumia leo na ukaweza kupiga hatua kubwa sana.

Uzuri ni kwamba, ratiba hiyo haibani sana, kuna muda mwingi wa kupumzika au kufanya mengine.

Lakini kikubwa nilichoifunza kwenye barua hii ni kwamba, kujipangia na kujisimamia mwenyewe ni vigumu, lakini ukiwa na mtu anayekusimamia, inakuwa rahisi kufuata.

Hivyo kama una changamoto ya muda, hebu jitengenezee ratiba ya aina hiyo, kwa kuwa na matukio muhimu ya kufanya kila siku na muda wake, halafu mshirikishe mtu anayeweza kukusimamia kweli. Kwa mfano kama unapenda kupata muda wa kusoma vitabu ila hupati, weka kwenye ratiba yako ya kila siku na muda wa kufanya hivyo, kisha ifuate. Kadhalika kama unataka kuandika au hata kutahajudi, chochote unachojua ni muhimu kwako kufanya lakini hupati muda wa kufanya, jiwekee ratiba ya aina hiyo na mtu wa kukusimamia.

Ukikosa wa kukusimamia kabisa, basi mimi Kocha wako nipo, nipo tayari kukusimamia kwa ratiba utakayojiwekea kwa mwezi mmoja tu halafu wewe mwenyewe uone ina manufaa au la. Kama utahitaji huduma hiyo ya ukocha, tuwasiliane kwa wasap 0717396253.

#4; HUDUMA NINAZOTOA; Kitabu; ijue biashara ya mtandao.

Kama kipo kitu ambacho kinashamiri kwa sasa basi ni biashara za mtandao. Lakini pia biashara hizi zimewaumiza wengi, wapo watu ambao hawataki kusikia kabisa neno biashara ya mtandao au NETWORK MARKETING. Labda walijiunga kwa kuambiwa ukiingiza watu watano na hao watano wakaingiza watano, na wale watano kila mmoja akaingiza watu watano, utakuwa na watu zaidi ya 100 chini yako na utaanza kupata mamilioni ya fedha. Wakaoneshwa na picha za milioni pale, na magari na nyumba nzuri, wakahamasika, wakajiunga, wakapewa bidhaa au huduma, wakaingia mtaani kuanza kuwasaka watu watano, na hapo ndipo shida ilipoanza. Watu watano hawapatikani na kuna kukatishwa tamaa kwingi. Muda unaenda, milioni hawazioni na kuona wamedanganywa na hivyo kuacha.

Hapo bado kuna wale ambao wameingia kwenye biashara ambazo siyo halali na kuishia kupoteza fedha.

Kikubwa nilichojifunza kupitia utafiti wangu ni kwamba, asilimia 99 ya watu wanaojiunga na biashara za mtandao, hawajawahi kupata mafunzo yoyote, hawajawahi kusoma kitabu chochote, ila wanasukumwa kujiunga kwa zile ahadi za kutengeneza mamilioni. Na hapo ndipo matatizo yote yanapoanzia.

Hivyo nilichukua muda wa kuandika kitabu kinachoitwa IJUE BIASHARA YA MTANDAO, kitabu ambacho kinaelezea misingi ya biashara hii, kwa lugha rahisi kabisa ya kiswahili pamoja na mifano halisi.

Hichi ni kitabu ambacho kila mtu anapaswa kukisoma, hata kama hafanyi biashara ya mtandao, kwa sababu kitamsaidia sana kufanya maamuzi kwenye mfumo huu wa biashara.

NETWORK MARKETING

Kama mpaka sasa bado hujasoma kitabu hichi basi unahitaji kukisoma sasa. Kitabu kipo kwa softcopy na kinatumwa kwa email. Gharama ya kitabu ni tsh 5,000/= na kukipata tuma fedha kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; Kwa nini unafupisha maisha yako?

“So it is: we are not given a short life but we make it short, and we are not Ill-supplied but wasteful of it.” ― Seneca

Seneca, mwanafalsafa wa ustoa ni mmoja wa watu walioandika sana kuhusu kuwa na maisha bora kwa kuchagua na siyo kwa bahati. Kwenye kitabu chake cha ON THE SHORTNESS OF LIFE, Seneca anasema kwamba maisha siyo mafupi, bali sisi wenyewe tunayafanya kuwa mafupi. Anasema muda siyo mchache, ila sisi wenyewe ndiyo tunachagua kupoteza muda wetu.

Kwa haraka unaweza kukataa hili, na kusema si kweli, maisha ni mafupi, watu wanakufa wakiwa wadogo na muda hautoshi, watu wapo bize. Lakini ukichimba kwa ndani, utagundua watu wanachagua tu kufupisha maisha na kupoteza muda. Kwa mfano mtu anapokazana na kazi ambayo haipendi, inampa msongo wa mawazo kila siku, anajikuta hama mahusiano mazuri na watu, hali vizuri, anaishia kupata magonjwa sugu kama presha na kisukari, halafu anakufa mapema, si ameamua kufupisha maisha yake mwenyewe?

Vipi kwa mtu ambaye kwenye siku yake anakazana kusoma na kuangalia kila aina ya habari, kutembelea kila aina ya mtandao wa kijamii na kuhakikisha hapitwi na lolote? Huyu kweli hana muda wa kutosha au anachagua kupoteza muda wake?

Jitafakari kwa kila unachofanya kila siku kwenye maisha yako na jiulize je huchangii kufupisha maisha yako? Huchagui kupoteza muda wako? Ukipata majibu chukua hatua.

Rafiki, juma namba 6 tumelimaliza, tunakwenda kunza juma namna 7 la mwaka huu 2018. Hakikisha kila juma kuna kitu unafanya, ambacho mwisho wa mwaka huu ukiangalia, unaona kila juma linasimama. Kazana hata kusoma kitabu kimoja kwa juma, hutabaki hapo ulipo sasa. Ongeza kipato kila juma, wekeza kila juma, ongea na watu wapya kila juma. Kwa kifupi usikubali juma lako lipite kimya kimya bila ya madhara yoyote ya kimafanikio yanayoweza kuonekana kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog