Kwenye zama hizi za taarifa, wateja wanapaswa kuwa na taarifa sahihi za biashara yako ili waweze kuchukua hatua ya kuja kununua kwako.
Na moja ya njia rahisi za kutoa taarifa za biashara yako ni kupitia mitandao ya kijamii. Kwa sasa karibu kila mtu mwenye simu, yupo kwenye mitandao hii ya kijamii.
Hivyo hili limefanya usambazaji wa taarifa kuwa rahisi na kuweza kuwafikia wengi zaidi.
Hivyo wafanyabiashara wengi wamehamasika kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wao, na hata kuuza moja kwa moja kwa wateja wao.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa na mategemeo makubwa sana kwa mitandao hii, wakiamini ina manufaa makubwa sana kwenye biashara zao, lakini wamekuwa hawaoni manufaa hayo moja kwa moja, hasa kwenye mauzo.
Ukweli ni kwamba, mitandao ya kijamii ina manufaa kibiashara, lakini si kwa kiwango ambacho watu wanafikiri.

Na hii ni kwa sababu, kila mtu anatumia mitandao hii kutoa taarifa za biashara yake, na huo unakuwa usumbufu mkubwa. Kwa upande wa pili, watu hawana kabisa muda wa kufuatilia kila kitu.
Hivyo pamoja na kuweka juhudi kubwa, bado wanaopata taarifa ambazo mtu unatoa kuhusu biashara yako kupitia mitandao ya kijamii ni wachache.
Kadhalika, kuuza moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii ni kugumu, hivyo wale wanaotegemea wauze moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wanakutana na changamoto hiyo ya kuuza kidogo kuliko walivyotarajia.
Hivyo rafiki, unapotumia mitandao hii ya kijamii kibiashara, usiweke matumaini yako yote na kuamini ndiyo umeshamaliza eneo la masoko la biashara yako. Mitandao hii ni sehemu ndogo, ambapo unahitaji kuendelea kutumia njia nyingine kuwashawishi wateja kununua. Mfano kutoa huduma bora kwa wateja wako, kupata shuhuda za wateja wako na kuwaomba wateja wako kuwaambia wengine kuhusu wewe ni njia zenye nguvu ya kuongeza wateja wanaonunua kwenye biashara yako.
SOMA; BIASHARA LEO; Wateja Wako Wanatamani Sana Kitu Hichi Kimoja Kutoka Kwako…
Na matumizi yako ya mitandao ya kijamii kibiashara, hakikisha unaifanya kwa ufanisi wa hali ya juu, kwa kutengeneza jumbe nzuri ambazo zinawafanya watu wazipende na kuvutiwa nazo na wasukumwe kuwashirikisha wengine na pia watake kukutafuta zaidi.
Kitu ambacho unapaswa kuepuka kwenye mitandao ya kijamii, ni kukazana kuuza moja kwa moja, kuweka picha nyingi za bidhaa au huduma zako ukitegemea wateja wanunue moja kwa moja kupitia mitandao hiyo. Matokeo ya hili ni madogo sana.
Tumia mitandao ya kijamii kwa manufaa kwenye biashara yako, lakini kuwa makini isiwe sehemu ya kupoteza muda wako na nguvu pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog