It is not he who reviles or strikes you who insults you, but your opinion that these things are insulting. – Epictetus

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu kwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari TATIZO SIYO TUSI UNALOTUKANWA, TATIZO NI TAFSIRI YAKO KWA TUSI HILO…
Huwa tunapata hasira pale watu wanapotuambia maneno mabaya, matusi au maneno ambayp tunaona ni ya dharau kwetu.
Na hasira yetu inaweza kuwa kubwa kiasi cha kutaka kuchukua hatua ili kuwaonesha watu hao kwamba hawapo sahihi.

Lakini ukiangalia kwa undani, utaona kwamba tatizo siyo tusi au neno baya alilosema mtu. Bali tatizo ni tafsiri yako wewe kwenye tusi au neno hilo.

💥Kwa mfano kama mtu akakutukana, lakini iwa sauti ndogo na hukusikia amesema nini, bado utapata hasira?
💥Vipi kama mtu akikutukana kwa lugha ambayo huielewi, je utakasirika? Kakutukana, lakini hujui kama amekutukana, hapo utakuwa huna cha kukasirikia.

💥Pia kama mtu anajulikana kwamba ana matatizo ya akili, je akikutukana bado utakasirika?
💥Je vipi kama anayekuambia neno hilo baya au tusi ni mtoto mdogo, ambaye hata haelewi maana yake, yeye alisikia tu watu wanalitamka na yeye katamka, je bado utapata hasira?

Unaona rafiki, katika hali hizo hapo juu, huwezi kukasirika hata kidogo, japo neno uliloambiwa ni lile lile, ambalo ni tusi, ambalo ni neno la dharau.
Hii inaonesha wazi kwamba, tatizo kubwa, kinachotupa hasira siyo lile tusi tunalotukanwa, bali tafsiri yetu kwenye tusi hilo.
Pale unapoanza kuchambua, kwa nini ameniambia hivi, amenionaje, amenichukuliaje, na kadhalika ndiyo yanachochea hasira ambazo mwishoni huwa haziishii vizuri.

Hivyo rafiki, mtu akikutukana, au kukuambia maneno ya dharau, fikiria hivi;
👉🏼hujasikia
👉🏼huelewi lugha aliyotumia
👉🏼ana matatizo ya akili
👉🏼ni mtoto asiyeelewa lolote.
Ukifikiria hayo na bado ukapata hasira, basi happ tatizo ni lako binafsi na siyo la mwingine.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha