You have power over your mind – not outside events. Realize this, and you will find strength. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu 2018 tutakwenda kufanya makubwa sana.

Asubuhi ya leo tutafakari NGUVU YAKO IKO KWENYE ENEO HILI MOJA…
Kila kiumbe hai kina nguvu ya kipekee ambayo inakiwezesha kiujbe hicho kuweza kuendelea na maisha kwenye dunia hii yenye changamoto.
Nyoka nguvu yake ipo kwenye sumu yake,
Simba nguvu yake ipo kwenye uimara wake,
Chui nguvu yake ipo kwenye mbio zake,
Popo nguvu yake ipo kwenye usikivu wake,
Mbuyu nguvu yake ipo kwenye ukubwa wake na udogo wa majani.

Na sisi binadamu, nguvu yetu ipo kwenye eneo moja muhimu sana ambalo ni akili na mawazo yetu.
Hatuwezi kubadili kila tunachokutana nacho, na hatuwezi kuifanya dunia iende kama tunavyotaka, lakini tunaweza kubadili mawazo yetu na yakaendana na jinsi dunia inavyokwenda.

Nguvu yako ipo kwenye akili yako na siyo kwenye mambo yanayotokew nje. Ukigundua hili na kulitumia vizuri, utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako licha ya magumu unayokutana nayo kwenye maisha.
Kila unapokutana na ugumu au changamoto, kumbuka nguvu yako iko wapi na itumie. Kama viumbe wengine wanavyotumia nguvu zao kuyamudu maisha, nawe pia tumia nguvu yako ambayo ni akili na mawazo yako.

Nakutakia siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha