Watu wengi wamekuwa wanapanga kufanya makubwa, na wengine wanaanza hata kufanya, wakiwa na hamasa kubwa mwanzoni, ila haiwachukui muda wanakata tamaa. Wanakuwa wanataka sana kuendelea, ila wakiangalia mbele hawaoni matumaini hivyo kukosa kabisa nguvu ya kuendelea.

Kwa yeyote yule anayekata tamaa kwenye jambo lolote kwenye maisha, basi cha kwanza kabisa anakuwa amejisababishia yeye mwenyewe. Yeye mwenyewe anakuwa ametafuta njia ya kumkatisha tamaa. Na dunia ina wema sana kwenye mambo kama hayo, huwa haikosi njia za kukukatisha tamaa.

Mambo ya Kawaida

Kwa mfano, unataka kufanya mambo makubwa, unawajua watu wanaokuzunguka hawajawahi kufanya hayo makubwa unayowaza kufanya, ila unawaendea kuwaomba ushauri, unakuwa unategemea wakupe ushauri gani? Wengi watakupa ushauri wa kukukatisha tamaa, kukuambia achana na hayo, haiwezekani, utashindwa na maneno mengine ya aina hiyo.

Hii inafanana pia na mtu ambaye ana maono makubwa, ila anaanzia chini kabisa, lakini anajilinganisha na wale ambao wameshapiga hatua kubwa kwenye kile anachofanya, anawaona wapo mbali sana na yeye hawezi kufika kwenye ngazi hiyo, anashindwa kuendelea.

Inawezekana pia mtu anasikiliza tabiri za watu mbalimbali, ambao wanatabiri mambo yatazidi kuwa magumu kwa siku zijazo. Mtu ambaye alipanga kufanya makubwa, kwa kusikia utabiri huo ambao siyo mzuri, anaona hana haja ya kuanza kwa sababu mambo yatazidi kuwa magumu.

SOMA; UKURASA WA 1007; Tamaa Ya Kukata Tamaa Na Kuacha…

Rai yangu kwako rafiki yangu, usitafute njia za kujikatisha tamaa, zipo nyingi na zimekuzunguka, zikwepe haraka sana. Ukishakuwa na ndoto kubwa kwenye maisha yako, kazi yako ya kwanza ni kuilinda ndoto hiyo, hakikisha chochote kinachotishia ndoto hiyo hakisogei karibu na ndoto yako, mtu yeyote au hali yoyote isiwe kikwazo kwa ndoto yako. Endelea kuiamini, endelea kuifanyia kazi na usikubali chochote kikurudishe nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog