Ukiwaangalia watu wengi kwa mtindo ambao wanaendesha maisha yao, ni rahisi sana kusema watu hao hata wafanyaje hawataweza kufanikiwa kwenye maisha. Unaweza ukajiuliza swali hapa nimejuaje kama hawawezi kufanikiwa?

Sikiliza nikwambie.  maisha ya mafanikio ni kama sayansi kama zilivyo sayansi zingine, hata kama hujui lakini ndivyo ilivyo. Hakuna swala linaitwa kubahatisha, ni matokeo ya kufanya vitu vya aina fulani ndiko kuna kupa mafanikio yako uyatakayo.

Kwa hiyo hili swala sio la uwe mtabiri au upige ramli ndio ujue kwamba utafanikiwa au hautafanikiwa. Mwendo wako au  ‘life style’  yako inaweza ikawa tochi kwako na kwa wengine kujua ni kweli utafanikiwa au utaishia kwenye ndoto tu.

Najua umenielewa lakini naomba nikwambie kwa msisitizo kwamba,  yapo maisha ambayo ukiyaishi  huwezi kufanikiwa. Utahangaika sana kutafuta mafanikio na utayumba huku na huko lakini wapi utabaki pale pale ulipo.

Kwa kuwa wewe ni rafiki yangu, nataka nikupe siri, kwamba ipo namna ambayo unatakiwa uishi ili weze kufanikiwa. Yapo mambo ambayo unatakiwa uyatumie na mengine usiyatumie ili ufanikiwe maishani mwako.

Leo hii kupitia makala haya nataka nikuonyeshe mambo matatu tu, ambayo mambo hayo usipoyatumia vizuri huwezi fanikiwa. Nimesema ni mambo matatu, sio mengi, lakini mambo haya yanawaangusha wengi. Mambo haya ni kama haya yafuatayo:-

vitabu softcopy

Muda.

Idadi kubwa ya watu ni wabovu sana katika matumizi ya muda wao. Wengi wanatumia muda wao katika vitu ambavyo badala viwape faida wanatumia muda katika vitu ambavyo viwanangusha moja kwa moja.

Nitakupa mfano hapa, moja ya matumizi mabovu kwa sasa ya muda yapo kwenye mitandao ya kijamii, matumizi mengine ya muda mabaya yapo kwenye kufatilia habari za umbea au kuiga hadithi zisizo na msingi wowote zinazofanana na hizi.

Unaposhindwa kuwa na matumizi yoyote ya muda mzuri, andika umeshidwa. Historia ya dunia inaonyesha wote wanaoutumia muda hovyo maisha yao ni ya kushindwa. Hakuna ambaye alifanikiwa kwa kuwa na matumizi ya hovyo ya muda wake.

Ni wajibu wako kuanzia sasa kama unataka kufanikiwa, kujijengea utaratibu wa kutumia muda wako vizuri. Kinyume cha hapo utakuwa unatafuta balaa lako la kushindwa. kama huna cha kufanya soma, jifunze shule ya maisha na vipo vitu vingi vya kujifunza, lakini usipoteze muda.

Soma; Jenga Utamaduni Wa Kutafakari Mambo Haya Kila Wakati Utafanikiwa.

Nguvu.

Mbali na matumizi ya muda ambapo watu wengi wanatumia muda wao vibaya sana kama ambavyo tayari tumeshasema, lakini pia wapo watu wanatumia nguvu zao vibaya. Si maanishi nguvu nyingine, namaanisha nguvu hizi za mwili.

Wapo watu badala ya kufanya kazi, wanatumia nguvu zao kubishana na watu hovyo au wanatumia nguvu zao kufanya kazi zisizo  za msingi ambazo zinawapotezea nguvu zao bure ambazo zingewasaidia kuzalisha zaidi.

Unapopoteza nguvu ambazo kiuhalisia zingekusaidia wewe kuweza kufanikiwa, unakuwa ni mtu ambaye unajitafutia balaa lingine la kuweza kushindwa kwenye maisha yako. Unatakiwa kuwa makini sana na nguvu zako.

Kila wakati ujue nguvu zako zinahitajika kuweza kuzalisha kitu fulani cha manufaa. Hilo unatakiwa uliweke akilini mwako na ujue moja kwa moja kwamba nguvu zako hazitakiwi kupotea potea hovyo, zinahitajika kutumika kwa faida.

Soma; Fursa Adimu Ambayo Ikienda Hairudi Tena. 

Uzingativu.

Pia watu wengi wanapotezwa kwenye ramani ya mafanikio kwa sababu wanakuwa ni watu ambao hawana uzingativu wa kutosha. Akili zinakuwa hazitulii sehemu moja, akili zao zinakuwa zipo sehemu nyingi sana.

Utakuta mtu  yupo ofisini akili zake zote zipo nyumbani, na akiwa nyumbani tena akili zake zinarudi ofisini. Unapokuwa unakosa au kupoteza uzingativu ujue kabisa unakuwa unajiingiza katika hali ya kushindwa.

Unapaswa kujua kama ni kazi unayoifanya, unatakia kuweka akili zako zote hapo. Usiyumbe na wala kupepesa macho  kwingine kwa kufanya hivyo, tambua kabisa utaweza kujenga uwezo mkubwa wa kufanikiwa na kufikia mafanikio makubwa.

Kwa kumalizia niseme hivi, kama kuna kitu unakifanya na unaona kabisa kinakupotezea muda, nguvu na uzingativu, ujue kabisa kitu hicho hakiwezi kukupa mafanikio achana nacho, kwani usipotumia mambo hayo matatu vizuri, utakwama tu.

Fanyia kazi  mambo haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.

Kwa makala nyingine nzuri za mafanikio na maisha tembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kwa kina.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; http//www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com