Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu tutakwenda kufanya makubwa sana.

Asubuhi ya leo tutafakari; HAKUNA KESHO…
Yapo mambo mengi ambayo huwa tunapanga kuyafanya, lakini hatufiki hatua ya kuyafanya.
Tunapanga vizuri kabisa na kujua kila hatua ya kupiga na kuchukua, lakini inapofika wakati wa kufanya, inakiwa vigumu kufanya.

Na moja ya sababu zinazopelekea watu hatufanyi kile ambacho tumepanga kufanya ni KESHO.
Kesho imekuwa kaburi la ndoto za wengi,
Kesho imekuwa kikwazo cha mafanikio ya wengi.
Na kesho imekuwa sababu kubwa ya watu kutokupiga hatua kubwa.

Pale inapofikia wakati wa kuchukua hatua, halafu mtu ukajiambia nitafanya kesho, au nitaanza kesho, ndipo tunapoanza kujipoteza.
Unapoamini kesho utakuwa tayari kuliko leo, unakuwa umechagua kuipoteza leo.
Cha kushangaza sasa, hiyo kesho nayo unaipoteza kwa kuamini kesho yake utakuwa tayari zaidi.

Chochote ambacho unapanga kufanya rafiki, anza kufanya hata kama bado hujawa tayari.
Kama tu umeshapanga utafanya, basi fanya.
Ukishaanza kujiambia lakini nitafanya kesho basi jiambie hivi kwa msisitizo, HAKUNA KESHO.
Hakuna kesho, bali una leo ya kufanya, kwa sababu hakuna yeyote kati yetu mwenye uhakika wa kuwa na kesho, lakini leo, kila mmoja wetu anayo.

Anza kuchukua hatua sasa, fanya kile ulichopanga kufanya, hata kama ni kwa hatua ndogo sana. Na unapojishawishi kwamba utafanya kesho, jikumbushe HAKUNA KESHO, kwa sababu huna uhakika na hiyo kesho.
Wapo wengi jana walisema kesho, lakini leo hii hawapo kabisa au kama wapo basi hawapo kwenye hali ya kuweza kuchukua hatua.
Ni leo, fanya leo.

Uwe na siku bora ya leo rafikim ya kufanya leo yale uliyopanga kufanya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha