Hivi umewahi kuwa na wazo zuri la kufanyia kazi, ambalo unajua linaweza kukuwezesha kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako. Lakini ukawa hulifanyii kazi, kwa sababu mbalimbali ambazo umekuwa unajipa. Halafu siku moja ukaja kukutana na mtu mwingine tayari anafanyia kazi wazo lile na anapata matokeo mazuri. Unajisikiaje katika hali hiyo? Ni maumivu makubwa sana, unajua kabisa kama ungechukua hatua ungekuwa na wewe umeweza kufika pale walipofika wengine.

Hii ndiyo sababu nakuambia wazo ambalo hulifanyii kazi ni maumivu makubwa sana. Hata kama wazo ni zuri kiasi gani, kama hutalifanyia kazi, litakuletea maumivu na kukujengea hofu kubwa kwenye maisha yako.
Na huhitaji kuwa mkamilifu ndiyo uchukue hatua, huhitaji hata kuwa tayari ndiyo uchukue hatua. Unapopata wazo na kuona ni wazo zuri, anza kulifanyia kazi, anza kuchukua hatua, anzia pale ulipo.
SOMA; UKURASA WA 1071; Acha Kujitengenezea Mateso…
Na ili iwe rahisi kwako, anzia pale ulipo, anza na kile unachopenda kufanya.
Kama unapenda kujenga, jenga zaidi,
Kama unapenda kuandika, andika zaidi.
Kama unapenda kukimbia, kimbia zaidi,
Kwa chochote unachofanya au kupenda kufanya, zipo fursa za kufanya zaidi, zitumie hizo kwa mawazo ya kupiga hatua uliyonayo.
Wazo lolote ulilonalo, unalipa thamani kwa kuchukua hatua. Wazo hata liwe zuri kiasi gani, bila ya kulifanyia kazi, bila ya kuchukua hatua, litaishia kuwa halina thamani na litakuletea maumivu na hofu.
Usisubiri kuwa mkamilifu, usisubiri kuwa tayari A.N.Z.A.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog