DARASA LA JUMAPILI.

MADA; UWEKEZAJI KWENYE SOKO LA HISA.

Karibuni wanamafanikio kwenye darasa letu la jumapili ya leo ambapo tunakwenda kujifunza na kujadili kwa kina kuhusu uwekezaji kwenye soko la hisa.

Hii ni moja ya njia muhimu za uwekezaji ambayo wengi wamekuwa wanashindwa kuitumia kutokana na kukosa maarifa sahihi ya kushiriki kwenye uwekezaji huu.

Kwenye darasa hili tutakwenda kujifunza kuhusu uwekezaji kwenye soko la hisa na hatua za kuchukua ili kuwa mwekezaji kwenye soko hili.

Darasa letu litakuwa na vipengele vifuatavyo;

  1. Maana ya uwekezaji.
  2. Aina za uwekezaji.
  3. Uwekezaji kwenye soko la hisa.
  4. Soko la hisa la Dar es salaam.
  5. Faida za kuwekeza kwenye soko la hisa.
  6. Hasara na changamoto kwenye uwekezaji wa soko la hisa.
  7. Mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa kwenye uwekezaji wa hisa.
  8. Mjadala, maoni na maswali na majibu.

Karibuni kwenye darasa tujifunze na tuweze kuchukua hatua za kuwa wawekezaji wazuri.

 

 

  1. Maana ya uwekezaji.

Uwekezaji ni njia ya kutengeneza kipato ambayo siyo ya moja kwa moja.

Zipo njia kuu mbili za kutengeneza kipato;

Moja; njia ya moja kwa moja, hapa inabidi uwepo wewe na uweke nguvu, akili, ujuzi na uzoefu wako ndiyo ulipwe. Mfano wa njia hizi ni kuajiriwa, kuwa na biashara ambayo unaiendesha wewe moja kwa moja. Hutalipwa kwenye kazi kama huonekani, na kama biashara yako inategemea uwepo wako ndiyo iende, usipokuwepo biashara haiendi na hupati kipato.

Mbili; njia isiyo ya moja kwa moja, hii ni njia ambayo unatengeneza kipato wakati wewe haupo moja kwa moja. Hapa unakuwa umetengeneza mfumo ambao wewe unaingiza kipato bila ya kuwepo moja kwa moja au kufanya kazi moja kwa moja. Mfano wa njia hizi ni kuwa na biashara kubwa ambapo kuna mifumo na watu wanaiendesha na haihitaji uwepo wako wa moja kwa moja. Njia nyingine ni uwekezaji, ambapo unaweka fedha zako sehemu ambapo zinazalisha faida wakati wewe unaendelea na mambo yako mengine.

Sasa tutakubaliana bila ya shaka yoyote kwamba kila mtu angependa kutengeneza kipato ambacho siyo cha moja kwa moja. Nani ambaye hapendi kutengeneza fedha huku akiwa amelala? Hii ni ndoto ya kila mtu. Na njia ya uhakika ya watu kufikia hili ni kupitia uwekezaji.

Sababu nyingine kwa nini unahitaji kutengeneza kipato ambacho siyo cha moja kwa moja, ni kwamba rasilimali mbili tunazotegemea sana yaani MUDA na NGUVU zina ukomo. Hata ungeweza kufanya kazi kiasi gani, kuna masaa 24 tu kwa siku, huwezi kuongeza zaidi ya hapo, hivyo kama unatengeneza kipato kwa masaa unayofanya kazi, tayari una ukomo. Pili kwenye nguvu, kila mtu anajua, ufanyaji wako wa kazi ukiwa na miaka 30 na ukiwa na miaka 60 ni tofauti kabisa, nguvu zinapungua kadiri umri unavyokwenda.

Hivyo kila mtu ambaye yupo makini na hali yake ya kifedha, kwa sasa na kwa baadaye, anapaswa kuwa na mfumo wa uwekezaji.

 

 

  1. Aina za uwekezaji.

Zipo aina nyingi za uwekezaji, na aina hizi zinaweza kugawanywa kwenye makundi makuu matatu.

KUNDI LA KWANZA; UWEKEZAJI WA UMILIKI.

Huu ni uwekezaji ambapo wewe mwekezaji unamiliki sehemu ya kile ambacho umewekeza. Uwekezaji huu unaweza usiwe salama sana, lakini pia unaweza kuleta faida kubwa. Pia uwekezaji huu unaleta faida kwa njia ya ongezeko la thamani na riba au gawio.

Uwekezaji ulipo kwenye kundi hili ni kama;

  • UWEKEZAJI KWENYE HISA
  • UWEKEZAJI KWENYE BIASHARA
  • UWEKEZAJI KWENYE MALI NA MAJENGO
  • UWEKEZAJI KWENYE VITU VYA THAMANI kama madini, picha n.k

KUNDI LA PILI; UWEKEZAJI WA KUKOPESHA.

Hii ni aina ya uwekezaji ambapo unatoa fedha zako na kukopesha kampuni au taasisi itumie kwenye shughuli zake kisha inakulipa wewe riba. Faida kwenye uwekezaji huu inatokana na riba pekee, uwekezaji haupandi thamani yoyote.

Uwekezaji uliopo kwenye kundi hili ni kama;

  • UWEKEZAJI KWENYE HATIFUNGANI
  • UWEKEZAJI KWENYE AKAUNTI ZA BENKI, kwa kuweka akiba yako benki na benki ikakupa riba.

KUNDI LA TATU; UWEKEZAJI AMBAO NI SAWA NA FEDHA.

Hii ni aina ya uwekezaji ambayo ni sawa na fedha taslimu, yaani kwa kufanya uwekezaji huu, inakuwa rahisi kupata fedha zako ukilinganisha na aina nyingine za uwekezaji.

Uwekezaji uliopo kwenye kundi hili ni UWEKEZAJI KWENYE MIFUKO YA UWEKEZAJI. Hapo unanunua vipande kwenye mifuko hiyo na faida unaipata kwa ukuaji wa thamani ya vipande. Na pale unapohitaji kuuza vipande vyako na kupata fedha taslimu, taasisi inayoendesha mfuko huo wa uwekezaji ina wajibu wa kukulipa fedha zako mara moja kulingana na thamani ya vipande wakati unauza. Haitegemei kupatikana kwa wateja kama ilivyo kwenye uwekezaji mwingine.

 

 

  1. Uwekezaji kwenye soko la hisa.

Uwekezaji kwenye soko la hisa ni aina ya uwekezaji wa umiliki.

Kupitia uwekezaji huu unakuwa na nafasi ya kumiliki sehemu ya kampuni au taasisi ambayo unakuwa umenunua hisa zake.

Kwa mfano kama mimi naanzisha kampuni, ambayo inahitaji mtaji wa laki moja, lakini mimi nina elfu 50, naweza kualika watu wengine wachangie mtaji uliobaki, na wao kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni hiyo kulingana na kiasi walichochangia.

Sasa pale kampuni inapofanya kazi, na faida ikapatikana, pia itagawanywa kulingana na uwekezaji ambao kila mtu amepata. Na iwapo kampuni itapata hasara basi walioweka mitaji nao wanakuwa wamepata hasara. Kampuni ikifa, walioweka mtaji wanakuwa wamepoteza mtaji wao.

Unaponunua hisa, unakuwa sehemu ya umiliki wa kampuni, japo huiendeshi moja kwa moja, bali fedha yako inaingia kwenye kuendesha shughuli za kampuni na faida inapopatikana, na wewe unalipwa faida pia.

Uwekezaji huu wa kwenye hisa unaweza kufanya kwenye kampuni binafsi, pale ambapo watu mnajuana na kuaminiana kiasi cha kuwa tayari kufanya biashara pamoja.

Pia unaweza kuufanya kwenye kampuni za umma, hizi ni kampuni ambazo zinasimamiwa kisheria kuuza hisa zake kwa wananchi na hivyo kunakuwa na matakwa wanayopaswa kutekeleza ili kulinda mitaji ya wawekezaji.

  1. Soko la hisa la Dar es salaam.

Soko la hisa la Dar es salaam, DAR ES SALAAM STOCK EXCHANGE (DSE) ndiyo taasisi yenye dhamana ya kusimamia uwekezaji kwenye hisa. Soko la hisa ndiyo linasimamia makampuni yote ambayo yameruhusiwa kuuza hisa zao kwa umma. Pia ndiyo chombo kinachosimamia uuzaji na ununuaji wa hisa baina ya wawekezaji.

Soko la hisa ni kama lilivyo soko jingine lolote, ila tu watu hawaendi na kupanga vitu vyao wanavyouza. Badala yake kuna watu wana hisa wanamiliki na kuna watu wanataka kununua hisa, hivyo wanakutana kwa ajili ya kuuza na kununua.

Ushiriki wa mwekezaji kwenye soko la hisa ni kupitia mawakala wa soko la hisa ambao wamedhibitishwa kisheria(brokers). Hawa ndiyo wanaouza na kununua hisa kwa niaba yako kwa sababu ndiyo wanaoshiriki kwenye soko moja kwa moja.

Iko hivi, hatuwezi watu wote kupata nafasi ya kushiriki moja kwa moja kwenye kuuza na kununua hisa. Hivyo kuna mawakala wachache, ambao tunawatumia.

Kwa mfano kama unataka kununua hisa, unaenda kwa wakala, unamwambia hisa gani unataka kununua na kiasi gani, unaweka fedha kwake, kisha yeye anaweka dau kwenye soko la hisa, kwamba ninahitaji hisa kiasi fulani, kama yupo muuzaji anayeuza basi anamuuzia. Kadhalika kwenye kuuza, kama unauza hisa zako, unamwambia wakala, unauza hisa kiasi gani, yeye anaweka taarifa sokoni na akipatikana mteja zinauzwa.

Wakati wa kuuza na kununua hisa pia unaweza kumwambia wakala kwamba nataka kununua hisa lakini bei isizidi hii, basi yeye ataweka dau sokoni na akijitokeza wa kuuza anakununulia. Hata kwenye kuuza pia, unaweza kusema sitaki bei iwe chini ya hapa, na yeye atasema bei ya kuuza.

Ukitaka kuelewa hili vizuri, pata picha ya gulioni au mnadani, pale mtu anatangaza anauza kitu na bei yake ni kiasi fulani, au anataka kununua kitu na ana kiasi fulani. Hivyo ndivyo soko la hisa linavyoendeshwa pia.

3.2 HATUA ZA USHIRIKI KWENYE SOKO LA HISA LA DAR ES SALAAM.

Kwa wawekezaji ambao ni wageni, zifuatazo ni hatua za kushiriki kwenye soko la hisa la Dar.

Moja; unafungua akaunti yako ya uwekezaji, unaweza kufungua kwa wakala wa soko la hisa. Kama upo dar kuna mawakala wengi, mfano SOLOMON ambao wapo jengo la ppf mtaa wa samora posta. Pia kuna orbit securities waliopo jembo la golden jubilee mtaa wa ohio posta. DES pia walikuwa na njia ya kufungua akaunti kwenye tovuti yao, ambayo kwa siku za karibuni sijaona ikifanya kazi, link ya maelezo ya njia hiyo ni hii; http://dse.co.tz/content/taarifa-kwa-umma

Mbili; unachagua wakala ambaye utanunua hisa kupitia yeye. Siyo lazima ununue kwa wakala mmoja pekee, lakini mara nyingi unakuwa na akaunti kwa wakala pia.

Tatu; unachagua hisa unazotaka kununua, kisha unamwambia wakala, unalipa kulingana na bei ya hisa, fedha unaweka kwa wakala. Yeye anakwenda sokoni na kununua hisa, kisha kukupa taarifa akishakamilisha. Baada ya kununua hisa unapewa cheti cha umiliki wa hisa.

Nne; kwenye kuuza pia unakwenda kwa wakala na cheti chako cha hisa, unamwelekeza ni kiasi gani cha hisa unauza, anaweka sokoni, zikinunuliwa anaweka fedha kwenye akaunti yako.

Kwa taarifa za hisa zinazopatikana kwenye soko la hisa la dar, pamoja na mawakala tembelea tovuti ya soko la hisa la dar ambayo ni www.dse.co.tz

  1. Faida za kuwekeza kwenye soko la hisa.

Zipo faida nyingi za kuwekeza kwenye soko la hisa. Hizi ni baadhi;

  1. Kutengeneza kipato ambacho siyo cha moja kwa moja, unapata fedha bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Kwa lugha nyingine, fedha yako inakufanyia kazi huku wewe ukiwa unaendelea na mambo mengine.
  2. Kukua kwa thamani ya hisa kunafanya uwekezaji wako kukua zaidi. Kama ulinunua hisa wakati hisa moja ni shilingi 500 baada ya miaka kadhaa hisa hiyo ikafika shilingi 2000 uwekezaji wako unakuwa umekua.
  3. Ni nafasi ya kushiriki kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, ambao unachangiwa na shughuli mbalimbali za uwekezaji.
  4. Ni rahisi kununua na unaweza kuanza na kiasi kidogo. Mfano hisa nyingi unaweza kununua kuanzia hisa 100 na kuendelea. Kitu ambacho ni rahisi kufanya kwa kipato kidogo ukilinganisha na uwekaji kama kwenye ardhi na majengo unaokutaka uwe na mtaji mkubwa kidogo.
  5. Ni rahisi kuuza pia, hasa pale hisa inapokuwa inafanya vizuri.
  6. Ni rahisi kutawanya uwekezaji wako, kwa kununua hisa za aina tofauti kutoka sekta tofauti hivyo sekta moja ikiwa na changamoto na hisa zake kushuka, hupati hasara.
  7. Unaweza kutumia hisa zako kama dhamana ya kupata mkopo kwenye baadhi ya taasisi za kifedha, hivyo inakusaidia.

 

  1. Hasara na changamoto kwenye uwekezaji wa soko la hisa.

Kila chenye faida basi kina hasara na changamoto zake. Na uwekezaji wa hisa una changamoto zake pia. Na changamoto kubwa kabisa ni kutokutabirika kwa soko la hisa, bei inaweza kupanda na kushuka muda wowote na hivyo uwekezaji huu umekuwa siyo salama sana, hasa kwa wale wanaotaka faida ya haraka.

Hasara na changamoto nyingine za uwekezaji kwenye hisa ni kama ifuatavyo;

  1. Hisa zinaposhuka thamani, mwekezaji anapata hasara kwa mtaji aliowekeza kushuka thamani. Kama ulinunua hisa 10 wakati hisa moja ikiwa shilingi 500, maana yake ulilipia shilingi elfu tano. Kama wakati unataka kuuza baadaye zimeshuka thamani na kufika hisa moja shilingi 300, kwa hisa kumi ulizonazo, utakuwa na shilingi elfu tatu tu, hivyo umepata hasara.
  2. Kampuni uliyonunua hisa zake ikifilisika, wanahisa ni watu wa mwisho kulipwa na hivyo kama hakuna kilichobaki kwa ajili ya kulipwa, unakuwa umepata hasara.
  3. Inahitaji kujitoa sana katika uwekezaji huu ili kuuelewa vizuri na kuweza kunufaika nao. Kuna vitu vingi vya kujifunza, unapaswa kufuatilia mwenendo wa makampuni, mwenendo wa soko na mwenendo wa uchumi kwa ujumla.
  4. Ni uwekezaji unaonyanyasa sana hisia, hasa pale soko linapokuwa limechangamka. Kwa mfano kama umeona hisa za kampuni fulani bei yake inapanda, unaingiwa na tamaa ya kuzinunua ili usipitwe na fursa hiyo. Baadaye hisa hizo hizo zikianza kushuka, unaingiwa na hofu ya kupata hasara na hivyo kukimbilia kuuza. Usipokuwa makini unajikuta umenunua hisa kwa bei kubwa na kuuza kwa bei ndogo, kitu ambacho ni hasara.
  5. Kama unawekeza wewe kama mtu binafsi, jua unapambana na timu za wawekezaji ambao ni wataalamu na wana uzoefu, hawa wanaweza kuliendesha soko kwa namna ambayo wewe utafanya makosa na wao wakanufaika.

 

  1. Mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa kwenye uwekezaji wa hisa.

Kwa haya tuliyojifunza kwenye uwekezaji wa hisa, yapo mambo muhimu sana ya kuzingatia kama unataka kuwa mwekezaji kwenye hisa na kufanikiwa. Na haya ni muhimu sana kama unawekeza wewe mwenyewe kama mtu binafsi.

  1. Usijaribu kutabiri soko.

Hili ni zoezi ambalo litakuingiza kwenye hasara kubwa. Hakuna mtu anayeweza kuitabiri kesho, hivyo kununua hisa kwa kuamini unautabiri zitapanda bei haraka, unajidanganya.

  1. Wekeza kwa mipango ya muda mrefu.

Kama unataka kufanikiwa kwenye uwekezaji wa hisa, chagua hisa unazoona zipo kwenye sekta nzuri kibiashara, kisha kaa nazo kwa muda mrefu. Muda mrefu hapa nazungumzia miaka zaidi ya kumi. Kwa muda mrefu, soko la hisa limeonesha kuleta matokeo mazuri, angalau ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka. Lakini kwa muda mfupi huwezi kutabiri.

  1. Usijaribu kuchuuza hisa (share trading)

Wapo watu wamekuwa wakifikiria kununua hisa zinaposhuka bei, na kuziuza mapema zinapopanda bei. Hili ni zoezi lenye hasara kubwa, kwanza huwezi kutabiri lini zitapanda, na zaidi ukiondoa gharama za tozo kwenye kuuza na kununua, hubaki na faida yoyote.

  1. Usikubali hisia zikutawale kwenye maamuzi ya kununua au kuuza hisa.

Ukishatawaliwa na hisia, unafanya maamuzi mabovu. Usinunue kwa sababu kila mtu ananunua, na usiuze wakati kila mtu anauza. Utakuwa salama zaidi kama ukiweza kwenda kinyume na hisia za wengi. Warren Buffet anasema wakati kila mtu ananunua wewe uza, na wakati kila mtu anauza wewe nunua. Hapo ndipo unaweza kupata faida.

  1. Jielimishe kila mara kuhusu uwekezaji na uchumi kwa ujumla.

Kufanikiwa kwenye uwekezaji wa hisa kunakutaka uwe na uelewa wa msingi kuhusu fedha na uwekezaji, pia kuelewa namna uchumi unavyoenda. Hii itakusaidia kujua hisa zipi ununue na wakati gani wa kuuza ili usichelewe sana na ukapata hasara.

 

  1. Mjadala, maoni na maswali na majibu.

Hongera mwanamafanikio kwa kufuatilia kwa karibu darasa hili la uwekezaji kwenye soko la hisa.

Tumejifunza yale muhimu na ya msingi kabisa kwenye uwekezaji wa soko la hisa. Hatujaweza kugusia kila kitu, kwa sababu uwekezaji una wigo mpana, lakini kwa haya tuliyojifunza yanatosha kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.

Karibuni sasa kwa maswali, maoni na hata michango zaidi kuhusu uwekezaji kwenye hisa.

Unaweza kuchangia chochote kulingana na uelewa au uzoefu wako.

Pia unaweza kuuliza chochote ambacho hujaelewa au ungependa kupata ufafanuzi zaidi.

Karibuni sana wote.

SWALI; Daniel Sitoni Kambei: Dr mimi nilijaribu kuwekeza kwenye hisa katika benki ya MecoBank, 2015 lakini januari,  serikali ilifunga benki hii na nilijikuta njia panda. Sijui hatima yake itaishia vipi ila mimi nimeamua kuwekeza asilimia ya kila pesa inayopita mkononi mwangu sasa hivi. Wakati huo nikifikiri kuchukua hatua nyingine katika nyanja ya uwekezaji ambao ni muhimu sana kwa mafanikio bora. Asante kocha kwa darasa zuri jioni ya leo. Mungu akubariki usonge mbele zaidi kusaidia wengi kama mimi.

JIBU: Pole Daniel kwa changamoto hiyo, hizo ndiyo changamoto za uwekezaji. Ili kuwa salama zaidi, wekeza kwenye kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa, hizi zinafuatiliwa kwa ukaribu zaidi na kabla mambo hayajaharibika unaweza kujua na kuchukua hatua ili usipate hasara. Kwa mfano makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko, kila mwaka yanapaswa kutoa hesabu za fedha zilizokaguliwa na mkaguzi wa fedha. Hii inakusaidia kuona mwenendo wa kampuni husika.

SWALI; Raymond: Asante sana Kocha Makirita kwa somo hili, nimekuwa mwanafunzi wa kuendelea kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji na Hisa

Kuna sehemu juu umegusia Uwekezaji wa Thamani na ukataja Picha hapa Kidogo ningeomba msaada kufahamu zaidi umekaaje?

Natanguliza shukrani za dhati.

JIBU: Karibu sana Raymond, kwa wenzetu wana mfumo wa kununua picha na michoro ya kale ambayo huwa inapanda thamani kadiri muda unavyokwenda. Kwa mfano mchoro wa da vinci au picaso ambao alichora kwa mkono wake unauzwa ghali sana, na mtu anaweza kununua na kukaa nao kwa lengo la kuja kuuza baadaye kwa faida zaidi.

SWALI; Ebbi ludoga: Swali langu kocha ni hivi, ni kwa muda gani mawakala wanatumia kulipa Pesa kwa mwekezaji baada ya mwekezaji  kuuza hisa  zake.

JIBU; Karibu Ebbi, kulipwa ni mpaka hisa ziuzwe, hivyo inategemea inachukua muda gani hisa kupata mteja sokoni. Lakini zikishauzwa unapaswa kuwekewa fedha yako mara moja pale taratibu zinapokamilika.

SWALI; FELIX MICHAEL MUSHI: Asante Dr. Ni Uwekezaji UPI madhubuti na unaolipa vizuri kati hisa, hatifungani na uwekezaji kwenye ardhi majengo?

JIBU; Karibu Felix, leo tumejadili uwekezaji wa hisa pekee, kila uwekezaji una faida na hasara zake, hivyo hakuna ambao ni bora zaidi ya mwingine, ila inashauriwa kuchanganya uwekezaji. Kuwa na sera yako ya uwekezaji ambapo unatenga kiwango cha kuwekeza kwenye hisa, hatifungani na hata majengo.

SWALI; John Matiku: Nashukuru kwa darasa zuri sana, binafsi nafuatilia kwa kiasi ila taarifa kuhusu hisa na soko lake japo sijafanya maamuzi ya kuwekeza kwenye hisa kwani bado naona kwa nchi zetu hizi kuna fursa zaidi ya kutengeneza faida kwa uwekezaji mwingine kuliko kwenye hisa! Japo nakubaliana kuwa kwa njia ya akija na kwa dhana ya utawanyaji uwekezaji ni uamuzi bora na sahihi.

JIBU; Karibu John, ni kweli soko letu la hisa bado halijachangamka sana ukilinganisha na nchi nyingine. Lakini pia bado watu wananufaika sana, kwa sababu yapo makampuni makubwa sana ambayo yanacheza vizuri na hili soko ya yanapata faida kubwa. Hata moja ya sababu za kutaka makampuni ya simu yajiorodheshe kwenye soko la hisa ni kutaka faida wanayonufaika nayo wachache, iende kwa wananchi pia. Hivyo ni muhimu kutawanya uwekezaji kwa kupitia soko la hisa pia, hasa kwa manufaa ya badaye na siyo ya sasa.

SWALI;  Godfrey Mbise: Cheti/Vyeti vya umiliki Wa hisa nilivyowahi kuona vimeandikwa ordinary share, je zipo hisa ambazo si za kawaida?

JIBU; Karibu Godfrey, ndiyo yapo madaraja ya hisa na haya yanapima kiasi cha uwekezaji na nguvu ya kufanya maamuzi kwenye kampuni. Kwa mfano ordinary shares hizi ni hisa za kawaida kabisa ambapo mtu unamiliki hisa na kupewa taarifa ya kile kinachoendelea kwenye kampuni, lakini huna nguvu ya kufanya maamuzi yoyote juu ya uendeshaji wa kampuni husika. Kampuni inaweza kuwa na madaraja mengine yanayowapa watu nafasi ya kushiriki kwenye maamuzi ya uendeshaji wa kampuni, kama kupiga kura na kadhalika.

SWALI; Alphonce Lukengelo Ngavatula: Asante! Uwekezaji huu kwangu ni mpya. Nitapataje kujiunga na uwekezaji huu?

JIBU: Kama ndiyo unasikia leo kwa mara ya kwanza, basi ushauri wangu kwako ni endelea kujifunza zaidi kwanza, kabla hujaingia kuwekeza. Soma vitabu, soma makala na fuatilia soko la hisa. Emilian Busara ana vitabu vizuri kuhusu uwekezaji, vipate uvisome.

SWALI;  Aliko Musa: Asante Sana Kocha Dr. Makirita

Nashukuru sana kwa somo lako zuri sana kwangu mimi, NIMEJIFUNZA MENGI SANA. Moja kati ya lengo langu kubwa la mwaka 2017. Ni kusoma vitatu vya Uwekezaji kwa bidii kuliko vitabu vingine. Yaani kama kila pointi nikikuuza inazaa vitu vingi sana hapa.

Nimejifunza kuwa biashara na uwekezaji vinakwenda pamoja, na UMEELEZA HAPO JUU. Mambo ya kuzingatia uliyoyasema sitayapuuzia hata kidogo. Wawekezaji wengi wenye mafanikio makubwa Kwenye Majengo, wamewekeza pia kati HISA NA VIPANDE.

Nina changamoto moto kubwa ya kuulewa uwekezaji kwa sasa.

Kila nikiona Uwekezaji akilini inakuja HATE+LOVE. na kitabu cha mentor Wangu Warren Buffet kiitwacho Warren BUFFET portfolio cha Robert Hagstrong. Ndio kitabu nimekiona the best kwangu mimi mchanga Katika Uwekezaji. Japo wengi wanaisifia THE ESSAYS OF WARREN BUFFET.

Binafsi nitakusumbua sana kuhusu uwekezaji. Na wengine hapa ndani msichoke NINAPOKUJA NA MASWALI. Asanteni.

Sasa Index, best gainers, losers, vile vya DSE siwezi kuhusianisha na elimu ninayoipata Kwenye vitabu, SIJUI UNANISAIDIAJE?

JIBU; Karibu sana Aliko, endelea kujifunza, na hayo yote utaona jinsi yanavyoendana na yale unayojifunza. Kwa mfano index ni kielelezo cha soko kwa ujumla, losers na gainers ni zile hisa zinazopanda na zinazoshuka na kadhalika.

SWALI; Alfred Mwanyika: Asante Coach kwa somo zuri. Naomba kuuliza swali,  kupanda au kushuka kwa bei ya hisa kwa kampuni husika husababishwa na nini? Na ni nani hukokototoa thamani ya hisa za makampuni hayo? Na wanakokotoa vip?

JIBU; Karibu sana Alfred, kinachosababisha kupanda na kushuka kwa bei za hisa, inaweza kuwa mwenendo wa kampuni husika, au nguvu ya uchumi. Kama kampuni inafanya vizuri, inapata faida na kutangaza gawio kubwa, basi hisa zake zinapanda bei kwa sababu wengi wanazitaka. Na kama haifanyi vizuri watu hawazikimbilii na hivyo thamani kuwa chini. NANI ANAPANGA BEI YA HISA, na mimi nikuulize nani anapanga bei ya maembe? Vyote ni sawa, leo ukichukua embe linalouzwa 500 na kuuza elfu 3 hakuna atakayenunua, kadhalika, wakati wa msimu wa maembe bei zitakuwa chini, wakati ambao siyo wa msimu, bei zinapanda. Hivyo nguvu ya uchumi kwenye DEMAND NA SUPPLY ndiyo inaendesha soko. Na hisia za watu pia.

SWALI; Godfrey Mbise: Je makampuni yanalazimika kulipa Gawio? Kama ndiyo kwa utaratibu gani?

JIBU; Kulipa au kutolipa gawio ni maamuzi ya kampuni na siyo matakwa ya kisheria. kila kampuni huwa ina mwongozo wake wa uwekezaji (prospectus) na huo ndiyo unaeleza namna gani wawekezaji wananufaika kwa kumiliki hisa za kampuni husika. kampuni inaweza kuamua kuweka faida kwenye kuongeza thamani ya hisa, kama inataka kukuza mtaji, au ikatoa gawio.

SWALI; Aliko Musa: Na kitu kingine ambacho nimejifunza diversification IS the protection from ignorance.

Kuna mentor mwingine anasema wekeza Kwenye HISA ZA KAMPUNI TATU TU NA SI ZAIDI YA HAPO.

Buffet anasema wekeza kampuni tano hadi kumi. Na wawekezaji wa kijiji au jamii ya Ben Graham wanasema wekeza kampuni si zaidi ya 15. Kwa wote hao wanauita FOCUS investment.

Yupo profesa wa Mambo ya fedha (professor of finance) anasema kuwekeza kwa diversification ni kupoteza muda kwa soko la hisa linabanwa na kanuni Kali za kiuchumi

JIBU; Kuhusu kutawanya uwekezaji, kila mtu anaweza kuwa na maoni wake. kuna ambaye atakuambia weka mayai yako kwenye kikapu kimoja halafu kichunge, lakini kwenye uwekezaji wa hisa, nguvu yako kama mwekezaji kwenye maamuzi ya kampuni ni mdogo. hivyo usalama wako ni kutawanya uwekezaji, hutapata hasara moja kwa moja, labda uchumi wa nchi ufe kabisa, kitu ambacho siyo rahisi. Makampuni makubw atu nchini marekani yamekufa, hivyo huwa na hisa kwenye kampuni moja au chache, ni kujiweka kwenye hatari isiyo na msingi.

SWALI; Goodluck Moshi: Hongera sana Kocha kwa somo zuri.

Je kuna uwezekano kampuni ikawa inafanya vizuri kuliko kiujumla sekta iliyopo hiyo kampuni husika?

Napenda kujua hasa kati ya sekta na kampuni katika ufanyaji vizuri nani ndiyo focal point katika kufanya maamuzi?

JIBU; Karibu Goodluck, ndiyo kampuni inaweza kufanya vizuri kuliko sekta. Lakini katika kufanya maamuzi ya uwekezaji, angalia zaidi sekta kabla ya kuangalia kampuni moja moja. Anza na sekta inayofanya vizuri, kisha ndani ya sekta ndiyo unaangalia kampuni ipi inafanya vizuri.

SWALI; Yusuph Yusuph: Asante sana coach kwa somo la leo

>Hapo kwenye uwekezaji soko la hisa,

kama kampuni ikipata hasara, inabidi na waliowekeza hisa wapate hasara, kwa maana ya hisa kushuka thamani kulingana na mtu alivyowekeza hisa zake?

Na Kama hisa zimeshuka thamani, na mwekezaji akauza hisa zake atapata hasara.

Hapa naona kama kuna vitu viwili

Kuna kampuni kupata hasara na kuna thamani ya hisa kushuka kama nimeelewa au sio coach uniweke sawa,   naomba ufafanuzi.

>Hawa mabroker wanapataje faida kutokana na kazi yao wanayofanya iwapo mimi naenda kwao kununua/kuuza hisa zangu,

>Hapo kwenye faida za kuwekeza kwenye soko la hisa

Nafikiri itakuwa na maana zaidi kama hizo hisa zako zitakuwa nyingi kwa kuweka dhamana ya mkopo, tofauti na mwenye hisa kidogo.

>Kwenye hasara na changamoto za uwekezaji huu wa hisa ulizoorodhesha, kumbe unapambana na watu wazoefu ambao wanakutengenezea mazingira ya kufanya makosa.

Na kwa mazingira ya sasa ndio maana watu walisita sana kununua hisa za voda,

Japokuwa umetoa  muongozo wa nn tufanye ili uwekezaji huu uwe wa faida, Unadhani ni sehemu muafaka ya kuwekeza, kwa nini tusiangalie uwekezaji ambao hauna changamoto nyingi, nini ushauri wako.

JIBU; Karibu Yusuph, ndiyo umeelewa sahihi, kuna kupanda na kushuka kwa bei, na kuna kampuni kupata hasara au kufa zote zinapelekea mwekezaji kupata hasara. Kwa mfano kama kampuni huwa inatoa gawio, ikipata hasara haiwezi kutoa gawio. Mabroker wanakata gharama zao kwenye kila hisa unazouza au kununua. Wengi gharama zao ni 2.5% ya thamani ya hisa unazonunua au kuuza. ndiyo maana kuuza na kununua mara kwa mara unapata hasara. Ndiyo, itakuwa na manufaa kama una hisa nyingi kuliko chache. Ndiyo, unapambana na wataalamu, hasa kama mbinu yako ni kununua bei chini na kuuza bei juu, lakini ukiwekeza kwa muda mrefu(buy and hold), hilo halikuathiri. Ndiyo, soko la hisa ni sehemu mwafaka ya kila mtu kuwekeza, na kila mtu anapaswa kuwekeza kwenye soko la hisa, ila usiwe ndiyo uwekezaji pekee, badala yake sambaza uwekezaji wako. Na kwa kumalizia, hakuna uwekezaji ambao hauna changamoto.

SWALI; Tumain Jonas: Asante sana kocha, Dkt. Makirita Aman kwa darasa bora sana la Leo . Binafsi nimejifunza mengi sana kupitia darasa la leo.

Swali langu ni kwamba; unapauza hisa zako kwa faida unakatwa kodi kulingana na fsida iliyopatikana. Je, ukipata hasara kwenye upande wa kodi unasamehewa au hilo  ikoje hapo?

JIBU; Ndiyo, unakatwa kodi kwa faida iliyopatikana, inaitwa capital gain tax, kodi ya ongezeko la mtaji. ukipata hasara hakuna kodi unayokatwa.

SWALI;  Moses Mahenge: Ahsante sana kocha, nimechelewa lakini nimelipitia darasa na nimejifunza mengi, Swali kwa wale ambao tumeamua kuwekeza kupitia UTT tunakuwa kundi lipi? Wawekezaji wa moja kwa moja au UTT ni kama wakala? Na je, UTT AMIS hawezi kufilisika au anaweza kufilisika na kwa nini?

JIBU; Karibu Moses, utt ni mfuko wa uwekezaji, INVESTMENT FUND, wao wanakusanya mitaji ya wawekezaji na kuwekeza wao kama wao, kulingana na wataalamu walionao na sera zao za uwekezaji.

SWALI; Martin Ditrich Tindwa: Asante kocha kwa somo zuri sana swali kwenye kufungua akaunti kwa ajili ya kununua hisa unafungua akaunti kwa kila broker au ukifungua kwa mmoja inatumika kote hiyohiyo.