Hongera rafiki yangu kwa kumaliza juma namba nane la mwaka huu 2018. Ni imani yangu kwamba limekuwa juma bora na la kipekee sana kwako, umeweza kupiga hatua na hata kujifunza pia.

Karibu kwenye makala yetu ya #TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya juma tunalokuwa tumemaliza. Kwa juma namba nane tulilomaliza, yapo mazuri ambayo nimejifunza na kukutana nayo, ambayo kwa kukushirikisha hapa utaweza kuchukua hatua pia.

Kabla hatujaingia kwenye TANZO ZA JUMA, kwenye makala iliyopita ya TANO ZA JUMA #7 Nilitoa zawadi ya vitabu viwili vya James Allen ambavyo naomba nikufahamishe kwamba zawadi zile zimeshapata wenyewe. Niwashukuru sana wale wote waliochukua hatua haraka kuhakikisha hawakosi hazina ile bora kabisa kutoka kwa James Allen.

Karibu sasa kwenye TANO ZA JUMA, lakini kabla, tuanze na neno, neno la kutuwezesha kuuona ulimwengu kwa namna nyingine, ili tuweze kuyaelewa yale tunayoyafanya au kukutana nayo.

#NENO; SABABU MBILI ZA WATU KUKUCHEKA.

Kwenye maisha, wapo watu wengi sana ambao watakucheka. Labda ni kwa kile ulichosema au unachofanya. Wengi wanapochekwa, hukata tamaa na kuona hawawezi na hawafai pia. Hivyo huacha kabisa kile ambacho wanafanya na kurudi kwenye maisha ya kawaida, kitu ambacho kinaua ndoto zao.

Sasa zipo sababu mbili za watu kukucheka;

Sababu ya kwanza ni kama unachekesha, kama umeongea au kufanya kitu ambacho kinachekesha, basi watu watacheka. Kama unafanya vituko, watu hawawezi kujizuia, watacheka.

Sababu ya pili ni kama hawakuelewi, kama watu hawaelewi kile ambacho umeongea au unafanya, watakucheka. Na hapa ndipo kundi kubwa la watu wanaocheka lipo. Kwa sababu kila ambaye alikuja na wazo la kufanya mambo makubwa, alichekwa. Mwanzilishi wa simu alichekwa, waliotengeneza ndege kwa mara ya kwanza walichekwa, wanasayansi wakubwa kama kina Newton na Einstein walichekwa kwa nadharia zao na hata Viongozi wakubwa wa kifalsafa na kiimani kama Yesu, Mohamad na wengine walichekwa sana wakati wanaanza na maono yao.

Hivyo basi, watu wanapokucheka, chagua ni kwa sababu ipi kati ya hizo mbili, kama ni kwa sababu unachekesha basi endelea, maana kuwapa watu kitu cha kucheka ni jambo jema pia. Na kama ni kwa sababu hawakuelewi, endelea kufanya, itafika hatua na watakuelewa, kama wote waliochekwa huko nyuma walivyokuja kueleweka baadaye. Kwa vyovyote vile, usiache kufanya unachofanya, na wala usiogope kusema unachotaka kusema kwa sababu watu wanakucheka. Watu kukucheka hakuna uhusiano wowote na wewe kuacha, ni wao wenyewe.

#1 KITABU NILICHOSOMA; EVOLUTIONARY ENLIGHTMENT.

Juma namba nane nimesoma vitabu viwili, na kimoja ni cha kiroho, ambacho wakati naanza kukisoma nilikutana na vitu vikubwa sana ambavyo sijawahi kupata nafasi ya kuvifikiri wala kuvitafakari. Kadiri nilivyokuwa ninaendelea kusoma, nilikuwa najiambia kitabu hichi sitawashirikisha wasomaji, kwa sababu kwanza ni kigumu, kinahitaji utulie sana uweze kuelewa, na pili kinagusa eneo ambalo wengi hawapendi liguswe, imani.

Imani zetu za kidini zimekuwa ni moja ya magereza makubwa sana ambayo tumejiweka. Ukiwakuta watu wanabishana ni dini ipi bora, labda kati ya Uisilamu na Ukristo, au ndani ya Ukristo ni dhehebu lipi bora, au wapi walio bora, waliookoka au ambao hawajaokoka, utashangaa namna ambavyo sisi binadamu tunatumia uwezo wetu mkubwa na wa Kiungu tulionao kwa mambo yasiyo ya msingi.

Karibu kila dini inakubaliana kwenye jambo hili moja, kwamba sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, na hili linamaanisha kwamba, uwezo tulionao, ni mkubwa mno kuliko ambavyo tunautumia. Tunahangaishwa na mambo ya dunia kama kula, kujamiiana na kulala, mpaka siku za maisha yetu zinaisha.

Lakini baadaye nilisema kitabu hichi kina nguvu sana ya kuwafungua watu, na nikasema nitawashirikisha wasomaji wangu, nikiwa na imani wapo watakaoelewa na kuchukua hatua, na wengine hawataelewa na kuendelea na maisha yao kama yalivyo, hivyo hakuna ubaya.

Mwandishi na mwalimu wa kiroho Andrew Cohen  kupitia kitabu hichi cha EVOLUTIONARY ENLIGHTMENT anatushirikisha jinsi ambavyo tunaweza kufikia uamsho wa kiroho, jinsi tunavyoweza kutumia ile nguvu kubwa ya Kiungu iliyopo ndani yetu, tukaishi maisha yetu halisi na kuwa na maisha bora sana.

Ni mambo magumu na yenye kuhitaji utulivu kuyaelewa. Wiki hii nitaweka makala nzima ya uchambuzi wa kitabu, nitaomba uipate uisome kama mara tatu hivi, wakati unasoma, sahau kila kitu kuhusu dini na imani yako kwa muda, ifanye akili yako kuwa wazi nasoma kama ndiyo unajifunza imani kwa mara ya kwanza. Ninakuhakikishia yapo mengi sana utakayojifunza.

Nimeshirikisha na kitabu kizima kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA, hivyo ukiwepo unaweza kukipata na kujisomea. Eneo la kiroho, ni eneo ambalo nimekuwa nalifanyia kazi kwa ngazi ya kujifunza na kuishi misingi ya kiroho kila siku, na ni eneo ambalo kila mmoja wetu anahitaji kulifanyia kazi, maana wengi wanaozungumza mafanikio, huwa wanazungumzia kwenye mali na mambo ya nje tu. Mimi ninapozungumzia mafanikio, ninaanzia ndani, na ndani kukishakuwa vizuri, basi nje kutakuwa kuzuri kwenyewe.

#2 MAKALA YA WIKI; MANENO MAKALI KWA WACHEZA KAMARI NA MICHEZO YA KUBAHATISHA.

Kujifunza na kujijenga kiroho kumekuwa kunanisaidia sana, la sivyo kuna vitu huwa navifikiria ambavyo ningekuwa navitekeleza, basi ningekuwa najiweka kwenye hali ngumu kila wakati. Kwa mfano kama miaka miwili imepita, wakati hii michezo ya kubashiri matokeo ya michezo na kushinda fedha inaanza, niliandika makala ya kuelezea kwa kina kwa nini michezo hii ni ya hovyo sana na inapaswa kudhibitiwa na mtu yeyote mwenye akili asishiriki kabisa. Lakini miaka inaenda, siyo tu haijadhibitiwa, bali kumekutokea mlipuko mwingine wa michezo hii ya kubahatisha na kamari ambao ni wa kutisha. Sasa hivi imekuja michezo ya kucheza kwa simu, hivyo mtu popote alipo, anaweza kucheza na kwa kiasi kidogo sana, cha shilingi mia tano au elfu moja, anaahidiwa kushinda mamilioni ya fedha. Na siyo tu kuahidiwa, bali anashawishiwa, kupitia matangazo na watu wanaohojiwa kwamba wameshinda, wakionekana ni watu wa kawaida sana na hivyo kila mtu kuona na yeye anaweza kushinda.

Sasa turudi kwa nini nimekuambia ukuaji wa kiroho unanisaidia eneo hili, ninavyoona namna watu na akili zao wanaingia kwenye huu mtego wa kuamini kwamba wanaweza kutoka kifedha kupitia bahati nasibu na kamari, nilijiambia kwamba nikigundua mtu anacheza hii michezo, sitaki hata kuongea naye, kwa sababu anakuwa amekosa umakini mkubwa sana. Lakini nilipofikiria hilo kiroho, nikaona ni kughafilika kwangu tu. Hivyo nitaendelea kujitahidi kutoa elimu hii, lakini naona namna ambavyo wengi hawaelewi. Kwa mfano mtu mmoja wa karibu nilipokuwa namwambia aache kushiriki michezo hii akaniambia kwani mia tano ni kitu gani, kila siku nikitenga elfu 2 ya kucheza mara nne, kuna siku nitashinda tu. Dah, hapo nilichoka kabisa.

Sasa wiki hii niliandika makala yenye maneno makali kidogo kuhusu wachezaji wa michezo hii, wakiamini ni njia ya kufanikiwa kifedha. Pia niliweka makala hii kwenye mtandao wa jamii forums na huko watu walikuwa na maoni mengi ya kutoa na mengi ni yale yale ya kusema kwamba siyo kitu kibaya.

Niendelee kusisitiza tu, michezo hii ina athari kubwa sana kwa kila mmoja wetu na hata taifa kwa ujumla. Kama unasoma hapa na umewahi kucheza, basi usirudie tena. Na kama unamjua yeyote anayecheza michezo hii, basi mshauri aache.

Makala niliyoandika ni hii; Kama Umewahi Kucheza Kamari Au Bahati Nasibu Nina Maneno Makali Kwako, Yasome Na Yatakusaidia.  (https://amkamtanzania.com/2018/02/23/kama-umewahi-kucheza-kamari-au-bahati-nasibu-nina-maneno-makali-kwako-yasome-na-yatakusaidia/) kama bado hujaisoma isome, pia itume kwa watu wote wa karibu kwako, utawasaidia kuepukana na utapeli na wizi huu wa wazi wazi.

vitabu softcopy

#3 NILICHOJIFUNZA WIKI HII; TABIA NANE ZA WATU WALIOSTAARABIKA.

Mwishoni mwa juma la nane nilikuwa natafuta njia bora ya kumshauri na kumsaidia ndugu. Nina ndugu yangu wa karibu ambaye kuna changamoto anapitia kwenye maisha yake, zipo wazi lakini inakuwa vigumu kwake kuzitatua. Sasa kitu kimoja ambacho nimejifunza, hasa kwa sisi ambao sehemu kubwa ya kazi zetu ni kuwashauri na kuwasimamia watu, ni vigumu sana kumshauri ndugu yako wa karibu. Hivyo nimekuwa najaribu kuongea na ndugu huyu, kwa vitu ambavyo viko wazi lakini anafanya moyo wake kuwa mgumu, ni kitu ambacho kinamuumiza. Na kibaya zaidi ni kwamba, kila mtu kwenye familia ananiangalia mimi kama mtu wa kumsaidia ndugu huyu kumaliza changamoto zake.

Hivyo nilijikuta kwenye mtandao nikitafuta njia bora ya kumshauri ndugu, ambaye anapitia changamoto mbalimbali kwenye maisha yake binafsi. Ndipo nilipokutana na barua ya Anton Chekhov aliyoandika March mwaka 1886, akiwa na umri wa miaka 26, kwa kaka yake Nikolai aliyekuwa na umri wa miaka 28, ambaye alikuwa anapitia changamoto mbalimbali kwenye maisha yake.

Kwenye barua hii alieleza mengi ya jinsi kaka yake huyo anapaswa kuyachukulia maisha, lakini sehemu niliyoipenda zaidi ni sifa nane za watu waliostaarabika alizomweleza kaka yake.

Na hapa naziweka kwa ufupi, nitakupa kiungo uzisome zaidi kwa kina.

Zifuatazo ni sifa nane za watu waliostaarabika;

  1. Wanawaheshimu wengine, ni wapole na waelewa. Hawapati hasiri kali kwa mambo madogo madogo, wanayachukulia kama yalivyo, hawawasemi wengine vibaya.
  2. Wana huruma kuliko ombaomba au paka, wanapogundua tabia zao ni tatizo kwa wengine, wanajirekebisha mara moja.
  3. Wanaheshimu mali za wengine, na hivyo wanalipa madeni wanayodaiwa.
  4. Ni wawazi na wanaogopa uongo kama ukoma. Hawadanganyi hata kwa mambo madogo kabisa. Wanajua jinsi ya kunyamaza, na muda mwingi wanakaa kimya.
  5. Hawajifanyi kuonekana duni ili waonewe huruma na wengine, hawalalamikii wengine, hawasemi watu hawanielewi.
  6. Hawajisumbui na vitu visivyo na maana kwao, hawahangaiki na sifa za kijinga. Wanapofanya kazi ndogo, hawakazani kuitangaza kwa kila mtu. Hawajisifii kwa wengine, kwa vitu ambavyo wao wanavyo na wengine hawana.
  7. Kama wana kipaji, wanakiheshimu. Wapo tayari kuacha mapumziko, kuacha kuhangaika na wanawake, kuachana na pombe kwa ajili ya kufanyia kazi kipaji walichonacho. Pia wapo makini sana na kile wanachofanya.
  8. Wanajali kuhusu uzuri, usafi na mwonekano wao. Hawakubali kuishi kwenye eneo ambalo ni chafu, au kurundika uchafu kwenye chumba wanachoishi. Hawalii chakula jikoni kwa kuwa na haraka au kuona hawana muda wa kupakua na kula chakula mezani.

Hizo ndiyo sifa nane za watu waliostaarabika, sasa rafiki yangu hebu jifanyie tathmini, ni sifa ngapi kati ya hizo nane wewe unazo, kisha jipe alama juu ya nane, kama una sifa tano basi jipe alama 5/8. Pia ziandike sifa hizi eneo ambalo unaweza kuzipitia mara kwa mara na kazana uwe nazo. Nimeziona kuwa sifa nzuri ambazo mtu ukiziishi, maisha yako yatakuwa bora sana.

Unaweza kuisoma zaidi barua hiyo kwenye kiungo hichi; http://www.lettersofnote.com/2013/07/every-hour-is-precious.html

Kitu kingine kilichonivutia zaidi kwa mwandishi wa barua hii,  Anton Chekhov alikuwa ni mwandishi mwenye mafanikio makubwa sana, daktari wa binadamu na pia maisha yake alipitia changamoto nyingi. Unaweza kusoma zaidi historia yake hapa; https://en.wikipedia.org/wiki/Anton_Chekhov

#HUDUMA NINAZOTOA; PERSONAL COACHING.

Kipo kitu kimoja, ambacho watu wanaofanikiwa sana maeneo yanayohitaji nidhamu wanakijua ila wengi hawakijui. Ukiangalia wachezaji wenye mafanikio makubwa kwenye kila aina ya mchezo, Ronaldo na Messi kwenye mpira, Serena William kwenye tenis, Tiger Woods kwenye golf, Floyd Mywether kwenye masumbwi, Kobe Bryant kwenye mpira wa kikapu, wote wana msaada wa kitu kimoja, wana makocha ambao wanawafundisha na kuwasimamia kwenye kufanya mazoezi mpaka wanakuwa bora sana.

Ukiangalia pia wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji wakubwa, wote wana watu ambao wanawasimamia kwa karibu, watu ambao wanawaambia pale wanapokosea na kuwasimamia kutekeleza yale waliyopanga. Lakini utashangaa watu wengi ambao ndiyo wanakazana kufanikiwa, wanaamini hawahitaji mtu wa kuwasimamia, wanaamini wanaweza kuweka malengo na mipango na wakaitekeleza tu.

Kinachotokea sasa, januari ya kila mwaka wanaweka malengo na mipango mikubwa, ila mpaka mwezi januari unaisha, wanajikuta hakuna walichofanya na mwaka unaisha hakuna hatua kubwa wamepiga. Hii ni kwa sababu, kupanga ni rahisi, ila kutekeleza ni kugumu. Sasa kama huna wa kukusimamia kwa karibu kwenye utekelezaji, ukikutana na ugumu unaacha na kurudi kufanya yale uliyozoea.

Ni baada ya kuona changamoto hii ikiwarudisha wengi nyuma ndipo nilipoandaa na kuja na program hii ya PERSONAL COACHING ambapo kwa mwezi mmoja, tunafanya kazi mimi na wewe kwa karibu, nakusimamia kwenye kile ambacho unahitaji kupiga hatua kwenye maisha yako.

Hii ni nafasi nzuri kwako rafiki yangu, kuchagua eneo moja ambalo unahitaji kulifanyia kazi lakini kila mara umekuwa unashindwa kupiga hatua au unarudi nyuma, kisha tunaweka mipango ya pamoja ya kufanyia kazi mwezi mzima na ninakufuatilia kwa karibu kwa mwezi huo.

Sasa nachukua nafasi hii kukujulisha kwamba zipo nafasi nne tu za coaching kwa mwezi wa tatu tunaokwenda kuanza kwenye juma hili la 9 la mwaka 2018. Hivyo kama unahitaji nafasi hii, tuwasiliane sasa ili kuzipata.

Gharama ya coaching ni shilingi laki moja(100,000/=) kwa mwezi. Karibu kwenye coaching program tufanye kazi kwa pamoja ili uweze kupiga hatua. Kama unataka nafasi hizi za mwezi wa tatu, niandikie mara moja kwa wasap namba 0717396253 ili tuweze kupanga yale unayokwenda kufanyia kazi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; JINSI YA KUIJUA AKILI ILIYOTULIA.

“Nothing, to my way of thinking, is a better proof of a well ordered mind than a man’s ability to stop just where he is and pass some time in his own company.” – Seneca

Hivi umeshagundua kwamba zama tunazoishi sasa ni zama za ajabu sana, zama ambazo akili zetu haziwezi kutulia kabisa? hebu jiulize ni mara ngapi unashika simu yako kwa siku, hapo hata hujapigiwa au hata kutumia ujumbe wowote muhimu. Bali unajikuta unaishika ukizurura kwenye mitandao ya kijamii na kufanya mambo mengine ambayo siyo muhimu?

Yaani sasa hivi mtu akiwa eneo ambalo hawezi kutumia simu, anapotoka tu, cha kwanza anakimbilia simu kama vile kuna nyumba inaungua moto. Angalia hata watu ambao wamepotezana miaka mingi, halafu wakaja kukutana, dakika chache za mwanzo wataongea, lakini baada ya hapo, kila mtu anainamia simu yake na utashangaa ukimya unaotawala hapo.

Seneca, mwanafalsafa mstoa anatuambia kwamba kujua akili iliyotulia ni kuangalia uwezo wa mtu kukaa pale alipo bila ya kufanya chochote au kuwa na yeyote. Hivyo kila siku, tenga muda fulani wa kutuliza akili yako, kaa sehemu peke yako, mbali na simu yako, na usifikirie chochote kuhusu kazi au maisha yako, tuliza akili yako kwa muda, inaweza kuwa dakika tano, nusu saa au hata saa moja. Zoezi hili litakusaidia kupata udhibiti wa akili yako na kuweza kufanya maamuzi bora.

Nikutakie kila la kheri kwenye juma hili la 9, likawe juma la kufanya makubwa ili mwaka huu 2018 ukawe mwaka wa kipekee sana kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog