Kama maisha ni mchezo, basi kuna jambo muhimu sana unalopaswa kulijua kabla ya kuingia kwenye mchezo huu. Na jambo hilo ni una mpango wa kucheza kwa muda mrefu kiasi gani?
Hili ni muhimu kwa sababu, usipokuwa makini kwenye muda, utajikuta unafupisha mchezo wako mwenyewe.
Kwa mfano kwenye mchezo wa riadha, kuna mbio fupi labda za mita 100 na zipo mbio ndefu za kilomita 20 na kuendelea. Sasa unaanzaje mbio zako, inategemea na urefu unaokwenda kukimbia. Kama mbio ni fupi, unahitaji kuanza na kasi ya juu kabisa. Lakini kama mbio ni ndefu, unahitaji kuanza na kasi ndogo huku mwili wako ukijenga na kutunza nguvu ya kumaliza mbio hizo. Sasa kama wewe utaanza mbio ndefu kwa kasi ya ajabu. Hutafika mbali.

Hivi ndivyo ilivyo kwenye maisha, bila ya kujua umbali tunaokwenda, tunajizuia wenyewe kufika mbali.
Na kwenye hili la umbali wa kwenda kwenye maisha, linahusisha maisha yetu kwa ujumla, kazi zetu, biashara zetu na hata mahusiano yetu na wengine.
Kwa mfano kama lengo lako ni kupata fedha za haraka tu, zipo njia nyingi za kuweza kutimiza hilo. Lakini sehemu kubwa ya njia hizi, zinakuzuia kupata fedha zaidi baadaye. Hivyo utapata fedha sasa, lakini baadaye hutaweza kupata tena fedha zaidi. Hapa ni pale unapofanya vitu ambavyo baadaye vinakujengea sifa mbaya. Vinaweza visiwe kinyume na sheria, lakini vikawa vinakuharibia hasa kwa baadaye.
SOMA; Mambo 15 Ya Kung’ang’ania Bila Ya Kujali Watu Wanasema Nini.
Kitu kingine cha kuzingatia kwenye mwendo na umbali wa maisha yetu ni nguvu zetu. Ni rahisi kufanya kazi zaidi bila hata ya kupumzika kwa siku kadhaa, lakini baada ya hapo ukatumia siku nyingi kwenye uchovu na hata kuumwa kitu ambacho kikakurudisha nyuma zaidi.
Hata kwa upande wa ulaji, upande wa watu unaokubali wawe na wewe na hata hatari unazochukua. Jiulize je hizo zinaendana na ule umbali wa maisha unaotaka kwenda?
Kwa kifupi, chochote unachotaka kufanya kwenye maisha yako, jiulize je unaweza kuendelea kukifanya kila mara kwa miaka 50 ijayo na matokeo yakaja kama ulivyotegemea? Pia jiulize je miaka 50 ijayo ukiangalia nyuma utajivunia kwa kufanya hicho unachotaka kufanya? Kama jibu ni hapana, au kama huwezi kusema ndiyo bila ya wasiwasi, basi jua hakikufai kufanya na usikifanye.
Kuwa makini na kila unachofanya leo, kinaweza kuwa kikwazo kikubwa kwako kwa siku za mbeleni.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog